• Nairobi
  • Last Updated May 7th, 2024 6:36 PM
Kang’ata kujua hatma yake ya ugavana leo Jumatatu

Kang’ata kujua hatma yake ya ugavana leo Jumatatu

NA RICHARD MUNGUTI

MWANIAJI wa Ugavana Murang’a kwa tikiti ya chama cha United Democratic Alliance (UDA) Dkt Irungu Kang’ata atajua hatma yake leo Jumatatu baada ya jopo la kuamua mizozo ya uteuzi kuelezwa alijibatilishia siku ya kuwasilisha karatasi zake kwa afisa msimamizi wa uchaguzi katika kaunti hiyo Saumu Omar Chirchir.

“Uidhinishwaji wa Dkt Kang’ata kuwania ugavana unafaa kufutiliwa mbali kwa vile alijitengea siku ya kuwasilisha stakabadhi kutoka Juni 6 hadi Juni 7, 2022 kinyume cha sheria,” wakili Peter Wanyama alieleza jopo hilo la IEBC linaloongozwa na Bw George Mburugu.

Mpigakura Bw Thomas Waithaka amesema hakuna uteuzi uliofanywa Juni 6, 2022 na ule uliofanywa siku ile kumpa idhini Dkt Kang’ata hautambuliwi kisheria.

Dkt Kang’ata alipata pigo mara ya kwanza wakati mwaniaji mwenza Dkt Winnie Njeri Mwangi alikuwa amekosa kujiuzulu na kumwacha kwenye mataa.

Dkt Mwangi alikawia kujiuzulu kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi anakosomesha.

“Uteuzi wa Juni 7, 2022 wa Dkt Kang’ata unakinzana na sheria na hautambuliwi hivyo anafaa kung’atuliwa,” alisema Bw Wanyama.

Wakili Peter Wanyama anayeomba Seneta Irungu Kang’ata azuiliwe kuwania Ugavana Murang’a. PICHA | RICHARD MUNGUTI

Lakini Dkt Kang’ata alipinga hayo akisema aliidhinishwa na Bi Chirchir kwa mujibu wa sheria na kuomba jopo litupilie kesi hiyo mbali.

Na wakati huo huo uteuzi wa Dkt Julius Malombe kuwania Ugavana kaunti ya Kitui kwa tikiti ya chama cha Wiper umepingwa huku manaibu wa ugavana wakidaiwa kuwa watu wa familia ya kinara wa chama hicho Bw Kalonzo Musyoka.

“Suala hili la uteuzi wa mwaniaji wa kiti cha Wiper limetiwa kizugumkuti na uteuzi wa watu wa familia ya Musyoka kuwa manaibu wa Dkt Malombe na Balozi Kiema Kilonzo,” Wakili Eric Mutua anayemwakilisha Kilonzo alidokeza mbele ya jopo hilo.

Jopo hilo linaloongozwa na Bw George Mburugu liliwaamuru mawakili Mutua, Issa Mansur (anayemwakilisha Dkt Malombe) na Kevin Kinengo Katisya anayewakilisha chama cha Wiper wawasilishe tetezi zao zote kufikia leo saa tano asubuhi kabla ya kesi hiyo kusikizwa saa nane unusu alasiri.

Bw Kilonzo amepinga uteuzi wa Dkt Malombe akisema asili mia 98 ya wapiga kura katika kaunti ya Kitui iliyo na vituo 1,454 vya kupigia kura hawakushiriki.

Bw Kilonzo amesema chama cha Wiper kiliteua vituo vinane tu kaunti nzima ya Kitui kuendeleza zoezi hilo la uteuzi wa mwaniaji kiti cha Ugavana mnamo Juni 3,2022 baada ya kuamriwa na mahakama kuu irejelee zoezi hilo katika muda wa masaa 72.

“Wiper kilimteua moja kwa moja Dkt Malombe kuwania kiti cha Ugavana Kitui na wala hakuna uteuzi uliofanywa kwa mujibu wa katiba ya chama cha Wiper na uamuzi wa Jaji Christine Meoli wa mahakama kuu, ”Bw Kilonzo anasema katika afidaviti yake.

Lakini Dkt Malombe amekanusha madai hayo ya mpinzani wake akisema “uteuzi ulifanywa kwa mujibu wa sheria na kamwe jopo hilo halipasi kuuvuruga.”

Dkt Malombe aliyemteua Bw Augustine Kanani ambaye ni binamu wa kinara wa Wiper Bw Kalonzo amesema alimshinda Bw Kilonzo na kuteuliwa kupeperusha bendera ya Wiper katika kinyang’anyiro cha Ugavana Kitui.

Gavana Charity Ngilu atatetea kiti hicho kwa tikiti ya chama cha Narc.

  • Tags

You can share this post!

Joho asihi wanasiasa wa Mombasa kuungana ‘kwa manufaa...

PAUKWA: Madhila aondoka kwa Kizito mzito wa moyo

T L