• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:55 AM
PENZI LA KIJANJA: Eti anataka umzalie kabla akuoe? Toroka!

PENZI LA KIJANJA: Eti anataka umzalie kabla akuoe? Toroka!

NA BENSON MATHEKA

VALENTINO imepita na baadhi ya waliotarajia raha walipata mishtuko. Kwa Grace, mshtuko aliopata ulikuwa kinyume na matarajio yake.

“Hebu fikiria, mtu kukupendekezea umzalie mtoto kabla ya kuoana. Eti date ya siku ya wapendanao, unayotarajia ahadi ya kujenga uhusiano wenu, mtu anakuambia umfanyie favor ubebe mimba yake umzalie mtoto kama hakikisho unampenda. Kama hilo ndilo hakikisho la mapenzi, acha kanuke!” Grace asema kwa hasira na uchungu.

Inaeleweka, japo kujipata katika hali kama yake sio jambo geni.Ni mtego ambao baadhi ya vipusa wamekuwa wakiangukia na kujipata wakiwa wamama singo bila kupanga baada ya wanaume waliotaka kufurahisha kuwatema na kuwasahau huku wakiwasingizia mambo kuwanyanyasa akili.

Hebu msikilize Ciru, mwanadada mwenye umri wa miaka 26: “Ilikuwa siku ya wapendanao mwaka 2022 Jose aliponiomba nimzalie mtoto. Nilikuwa mtu wake kwa miaka mitatu na kwa kufikiria ni mwaminifu zaidi nikakubali. Miezi saba nikiwa na mimba aliikana mimba yangu na kunitema kama ganda la muwa akidai nilikuwa ninamcheza na mimba haikuwa yake. Ilikuwa mbaya, lakini nikajipa moyo na kwa sasa ninaishi na mtoto wangu. Siwezi na sitawahi kuamini mwanamume tena,” asema Ciru ambaye kwa bahati nzuri ana mapato ya kumtunza mtoto wake.

Lakini inamuuma kwamba baada ya kumtema, mwanamume huyo alioa mwezi uliofuatia kuonyesha kwamba kwa muda wote waliokuwa pamoja, alikuwa na mpenzi mwingine na alichotaka kwa kumtaka abebe mimba ni kumtesa tu.

“Aliambia rafiki yake kwamba alitaka kuniacha na kitu cha kumkumbuka na ndio sababu alinishawishi kupata mimba yake,” asema.

Wanaume kama hao wametumbukiza vipusa wengi kwenye mateso na masononeko makuu hasa wasio na uwezo wa kuwapa watoto wao malezi mema.

“Ndio maana kesi za wanawake kuwashtaki wanaume wakitaka watunze watoto zimeongezeka. Vipusa wanapaswa kuepuka wanaume wanaoshabikia uroda bila kinga au wanaowataka kuwazalia watoto kabla ya kuoana rasmi,” asema mshauri wa mahusiano ya mapenzi Triza Kili katika makala aliyochapisha mtandaoni.

Anasema wanaume wengi wa siku hizi hawataki kuwajibika na kazi yao ni kutumia vipusa na kuwatupa wakipata mimba hasa wale wasio na mapato ya kutunza watoto wao.

“Ikiwa mwanamume anataka umzalie mtoto, mwambie akulipie mahari kwanza, kuwa na cheti za ndoa na ukiamua kumzalia kabla ya kukuoa rasmi, kuwa tayari kubeba mizigo wa kulea mwanao. Hawa wanaume wa siku hizi watakutumia na kukuacha unapowahitaji zaidi, kuwa mjanja,” Kili anashauri vipusa.

  • Tags

You can share this post!

UJAUZITO NA UZAZI: Tatizo la ‘colic’ kwa mtoto...

MALEZI KIDIJITALI: Mafunzo ya malezi dijitali kwa wazazi...

T L