• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 7:52 PM
Serikali ya Ruto ni ‘chafu’, serikali za kaunti zisiige nyayo zake, Raila aambia magavana 

Serikali ya Ruto ni ‘chafu’, serikali za kaunti zisiige nyayo zake, Raila aambia magavana 

NA SAMMY WAWERU

KINARA wa upinzani Raila Odinga amehimiza serikali za kaunti kuwa na misimamo dhabiti katika uongozi, ili kuafikia malengo ya ugatuzi. 

Akihutubu katika Kongamano la Ugatuzi 2023, Uasin Gishu mnamo Alhamisi, Agosti 17 kiongozi huyo wa Azimio la Umoja aliisuta serikali ya kitaifa akisema haipaswi kuwa kielelezo kwa serikali za ugatuzi.

Bw Raila alitaja ufisadi kama mojawapo ya masuala yanayopaka tope serikali ya Dkt William Ruto, hivyo basi kaunti zinapaswa kuwa na msimamo imara.

“Serikali za ugatuzi zisiige nyayo za serikali kuu. Ina dosari nyingi sana, ikiwemo kukumbwa na kashfa za ufisadi, ufujaji wa mali ya umma na matumizi mabaya ya mamlaka,” kiongozi huyo wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) aliambia magavana.

Raila ni miongoni mwa wanasiasa na viongozi mashuhuri nchini waliotetea kupitishwa kwa Katiba ya sasa, iliyounda serikali za ugatuzi.

Akiainisha tija na manufaa tele yanayotokana na ugatuzi, Waziri Mkuu huyo wa zamani alisema mfumo huo wa kiutawala unapaswa kutatua matatizo yanayokumba Wakenya.

“Baadhi ya changamoto zinazozingira wananchi ni za tangu serikali ya Mkloni, na serikali za ugatuzi zikipigwa jeki zina uwezo kuziangazia,” akasema.

Malalamishi ya madiwani (MCA) kuhusu nyongeza ya mshahara na marupurupu, Raila alisema ni suala linalopaswa kutathminiwa akihoji ni nguzo muhimu kufanikisha ugatuzi.

Kiongozi huyo wa upinzani, hata hivyo, alitaja mishahara minono katika sekta mbalimbali za umma na matumizi mabaya ya raslimali za umma, kama kero kuu kwa taifa na ni jambo linalochochea serikali kusalia mateka wa madeni.

Kongamano hilo la Makala ya Kumi na yenye kauli mbiu “Miaka Kumi ya Ugatuzi: Maisha ya Sasa na ya Baadaye”, lilifunguliwa rasmi Jumatano, Agost 16 na Rais William Ruto.

Mkutano huo wa ugatuzi, umeleta pamoja viongozi wa serikali, upinzani, na asasi mbalimbali za umma na sekta za kibinafsi kujadili kuboresha serikali za kaunti.

 

 

  • Tags

You can share this post!

Man-City waangusha Sevilla na kuongeza taji la UEFA Super...

Sakaja aimarisha ukusanyaji mapato Nairobi

T L