• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
SHINA LA UHAI: Ripoti yaonyesha mzigo na janga kuu la kansa nchini

SHINA LA UHAI: Ripoti yaonyesha mzigo na janga kuu la kansa nchini

NA PAULINE ONGAJI

KWA kila Wakenya watatu wanaobainishwa kuugua kansa, wawili kati yao hufariki, idadi inayowakilisha takriban asilimia 70.

Hii ni kulingana na ripoti ya uchambuzi wa takwimu za kitaifa za usajili wa maradhi ya kansa ya mwaka wa 2021 na 2022.

Hii ni mara ya kwanza nchini kwa takwimu za kansa kutolewa kutoka kwa sajili ya kitaifa ya kansa kupitia mfumo wa kitaifa wa usajili wa kansa nchini (NACARe-KE system), tofauti na awali ambapo data kuhusu maradhi haya zilitegemewa kutoka Global Cancer Observatory Globocan, mtandao unaotoa takwimu na makadirio ya kansa ulimwenguni.

Uchambuzi huo unaonyesha kwamba kaunti 10 zinawakilisha asilimia 63 ya idadi ya kansa miongoni mwa wanawake na asilimia 61 idadi ya kansa miongoni mwa wanaume nchini kote kila mwaka, huku visa 42,116 vipya vya kansa na vifo 27,092 vikiripotiwa kila mwaka.

Aina za kansa ambazo zimekithiri humu nchini katika kipindi hiki ni pamoja na kansa ya matiti kwa asilimia 15.1, kansa ya lango la uzazi ambayo inawakilisha asilimia 13.3 na kansa ya umio inayowakilisha asilimia11.8. Kansa za tezi kibofu na utumbo zinawakilisha asilimia 10.1 na 7.1 mtawalia.

Uchambuzi wa aina za kansa zilizokithiri nchini

Kansa ya matiti

Nairobi, Nakuru, Nyeri, Machakos na Kiambu ndizo kaunti tano za kwanza zilizo na idadi kubwa ya visa vya kansa ya matiti nchini. Katika kipindi hiki, Kaunti ya Nairobi ilisajili visa 140, Nakuru ikaandikisha visa 96, Nyeri visa 83, Machakos visa 69 na Kiambu visa 63.

Kansa ya lango la uzazi

Imeorodheshwa ya pili miongoni mwa aina za kansa zinazoathiri sana Wakenya, na ndio inayosababisha vifo vingi kutokana na maradhi haya miongoni mwa wanawake nchini. Aina hii ya kansa imeathiri sana Kaunti za Nakuru, Machakos, Nairobi, Kiambu na Kakamega. Katika kipindi hiki, visa 82 viliripotiwa katika Kaunti ya Nakuru, 74 katika kaunti ya Machakos, 66 katika Kaunti ya Nairobi, 52 katika Kaunti ya Kiambu, na 47 katika Kaunti ya Kakamega na Kitui.

Kansa ya umio

Kansa hii imeorodheshwa nambari nne miongoni mwa kansa zilizokithiri humu nchini na ambayo imehusishwa na uwezekano finyu wa kupona. Imekithiri sana katika Kaunti za Kakamega, Nyeri na Nakuru. Kaunti za Kakamega ilisajili visa 77, Nyeri visa 75 na Nakuru visa 65.

Kansa ya tezi kibofu

Kansa ya tezi kibofu inaorodheshwa nambari moja miongoni mwa kansa zilizokithiri sana miongoni mwa wanaume, huku Kaunti za Nairobi, Machakos na Nakuru zikiongoza kwa idadi ya wagonjwa. Kati ya watu 642 walioripotiwa kuugua, 64 walikuwa kutoka Kaunti ya Nairobi, 58 kutoka Kaunti za Machakos na Nakuru.

Kansa ya utumbo

Kaunti ya Nakuru ilikuwa na visa vingi vipya vya kansa ya utumbo ambapo iliwakilisha asilimia 12, na kufuatwa na kaunti za Nairobi na Kiambu na asilimia 11 na 8 mtawalia. Kaunti ya Nakuru ilisajili visa 54 vya aina hii ya kansa, huku Nairobi ikirekodi visa 48 na Kiambu visa 38.

Vifo kutokana na kansa

Kansa ya umio ndio inayoongoza miongoni mwa aina ya saratani zinazosababisha vifo vingi nchini huku ikiwakilisha asilimia 15.6. Kwa upande mwingine, kansa ya lango la uzazi inawakilisha asilimia 10.4, kansa ya matiti, asilimia 9.6 na kansa ya ini inawakilisha 9.1.

Jinsia

Wakilinganishwa na wanaume, wanawake ndio walioathirika pakubwa na maradhi ya kansa ambapo asilimia 53 ya wagonjwa wa kansa ni wanawake, ikilinganishwa na wanaume ambao ni asilimia 47.

Huduma ya matibabu ya kansa

Licha ya janga hili ambalo limeonekana kuibuka kutokana na maradhi haya, kaunti 28 kati ya 47 zilizopo, hazina vituo vya kutibu kansa. Ni kaunti 19 pekee nchini zilizo na vituo vilivyoidhinishwa kutoa matibabu ya kansa.

Nchini kuna vituo 68 vilivyoidhinishwa kutoa matibabu ya kansa nchini kote, na kati ya hivyo, ni 12 pekee vya umma, idadi inayowakilisha asilimia 18. Vituo vitano ambavyo ni sawa na asilimia 10 ni vya kidini, huku asilimia 52 vilivyosalia vikiwa vya kibinafsi.

Mgonjwa akipitishwa kwa mashine ya MRI Scanner. PICHA | FOTOSEARCH

Kaunti tatu zinazoongoza kwa idadi ya vituo vya kutoa matibabu ya maradhi haya ni Nairobi ambayo ina hospitali 17 ambapo mbili pekee ni za umma. Kaunti ya Uasin Gishu ni ya pili ikiwa na vituo vinane ambapo ni kimoja pekee ndicho cha umma, na Kisumu ambayo ina vituo saba na kimoja pekee ndicho cha umma.

Kati ya vituo hivyo 68, 48 vinaorodheshwa miongoni mwa vile vinavyotoa huduma za matibabu sahili ya tibakemia. Hii ni asilimia 69.

Kwa upande mwingine, 16 kati yavyo ambayo ni asilimia 24, vinatambuliwa kama vituo vya viwango vya kati. Vitano ambavyo vinawakilisha asilimia 7 pekee vinatambuliwa kama hospitali kubwa za kutoa matibabu ya kansa.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Majangili kaskazini mwa Bonde la Ufa ni...

Bayern watandika Wolfsburg na kurejea kileleni mwa jedwali...

T L