• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 10:50 AM
BENSON MATHEKA: Majangili kaskazini mwa Bonde la Ufa ni janga kubwa linalohitaji hatua ya upesi

BENSON MATHEKA: Majangili kaskazini mwa Bonde la Ufa ni janga kubwa linalohitaji hatua ya upesi

NA BENSON MATHEKA

VISA vya mashambulio yanayoendelezwa na majangili kaskazini mwa Bonde la Ufa havifai kuchukuliwa kama uhasama unaotokana na ushindani wa rasilmali tena.

Ujasiri ambao majangili hao wamedhihirisha kwa kupuuza onyo la serikali na wanavyozidisha mashambulio unaonyesha kuna hatari kubwa inayonukia.

Mwelekeo ambao mashambulizi hayo yamechukua haufai kuachiwa wazee wa jamii kuyatatua. Katika visa viwili vilivyotokea ndani ya wiki mbili, majangili wamevamia shule na kuzichoma na kufyatulia risasi magari kwenye barabara.

Visa hivyo viliripotiwa huku serikali ikiongeza maafisa wa usalama wakiwemo polisi wa akiba waliopewa mafunzo na onyo la Waziri wa Usalama Prof Kithure Kindiki kuwa serikali itawakabili vikali na kuwaangamiza.

Katika ziara yake ya mwisho eneo hilo, majangili hao waliwasha moto hatua chache kutoka alikokuwa akihutubia mkutano wa amani, kitendo ambacho, kwa hakika ni ishara ya kudharau mamlaka. Watu wasio na hatia wameuawa na majangili hao wanaoonekana kubadilisha mbinu kila wakati serikali inapotangaza kuwakomoa.

Ujasiri wao na wanavyotekeleza mashambulizi unaonyesha wanapata mafunzo na maagizo au kuelekezwa na mtu au watu walio na ufahamu wa masuala ya kivita.

Hali ilivyo kwa sasa ni kuwa majangili hao hawafai kuchukuliwa kama wahalifu wa kawaida tena. Juhudi zote zinapaswa kuwekwa haraka iwezekanavyo, na kwa vitendo ili kuwaangamiza kabla ya hali kugeuka kuwa janga na kusababisha maafa makubwa zaidi nchini.

Makundi yanayohangaisha raia katika baadhi ya nchi huanza kama magenge ya wahalifu wa kawaida kabla ya kubadilika kuwa majeshi ya waasi ambayo yangeshughulikiwa mapema na kuepuka hasara wanayosababisha.

Raia wasio na hatia wanauawa na majangili hao, mamia ya watu wametoroka na wanaendelea kutoroka makwao, shule zimefungwa na miradi ya maendeleo imekwama na hakuna dalili zingine kwamba janga linanukia.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Serikali ya Ruto itahadhari isirudie...

SHINA LA UHAI: Ripoti yaonyesha mzigo na janga kuu la kansa...

T L