• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
SHINA LA UHAI: Ukosefu wa visodo tishio kiafya kwa wasichana

SHINA LA UHAI: Ukosefu wa visodo tishio kiafya kwa wasichana

NI asubuhi katika shule ya msingi ya Mitaboni iliyoko Kaunti ya Machakos, lakini licha ya kijibaridi na upepo mkali unaovuma, wanafunzi ni wachangamfu.

Furaha yao inatokana na kuwa leo hii wana wageni kutoka mashirika kadhaa ambayo yameungana kuja kutoa msaada wa visodo vya kusafishwa na kutumiwa upya (reusable) kwa wanafunzi wasichana tokea gredi ya nne hadi darasa la nane.

Wanafunzi wengi katika shule hii ni kutoka familia maskini ambapo kwa wale wa kike, suala la kumudu kununua visodo hapa ni sawa na muujiza.

Mmoja wa watakaonufaika kutokana na msaada huu ni Lillian, mwanafunzi wa darasa la nane katika shule hii. Miaka michache iliyopita, Lillian alikuwa miongoni mwa wasichana wengi nchini ambao hawangeweza kumudu kununua visodo kila mwezi.

“Nakumbuka nilipoanza kushuhudia hedhi nilikumbwa na hofu na mambo yalikuwa mabaya hata zaidi kwani wazazi wangu walikuwa maskini na hawangeweza kuninunulia visodo,” asimulia.

Kwa hivyo, kuambatana na mafunzo aliyokuwa amepokea shuleni, alianza kukusanya matambara na vipande vya nguo kuukuu kutumia kudhibiti damu wakati huu wa mwezi.

“Hata niliogopa kutembea nikiwa shuleni kwa hofu kwamba vitambaa ambavyo nilikuwa nimevipachika kwenye chupi vingeanguka au damu ingevuja na kuonekana kwenye sare yangu, na hivyo kuniabisha,” aongeza.

Lakini sasa kwa Lillian na wasichana wengine shuleni humu wanaweza kuendelea na shughuli zao bila bila hofu kutokana na ufadhili wa mashirika kadhaa ambayo yamekuwa yakiungana kutoa bidhaa hizi kwa wanafunzi.

Kwa wasichana wengi nchini hasa kutoka maeneo maskini, bado uwezo wa kufikia visodo vifaavyo ni ndoto.

Takwimu zinaonyesha kwamba katika eneo la Afrika Mashariki, asilimia 80 ya wasichana hawawezi kumudu visodo.

Aidha, utafiti unaonyesha kwamba wawili kati ya wasichana watatu hawawezi kumudu bei ya bidhaa hizi.

Uchunguzi zaidi unaonyesha kwamba asilimia 65 ya wanawake na wasichana humu nchini hawana uwezo wa kununua visodo.

Sodo na kalenda. PICHA | MAKTABA

Tatizo hili limeathiri pakubwa uwezo wa wasichana kwenda shuleni. Utafiti unaonyesha kwamba takriban wasichana milioni moja hapa Kenya hukosa kwenda shuleni kila mwezi kwa sababu ya ukosefu wa visodo.

“Ni tatizo ambalo tulishuhudia hapa shuleni miaka michache iliyopita ambapo idadi ya wasichana waliokuwa wakikosa kuja shuleni kwa siku kadhaa kwa mwezi ilikuwa juu. Hii ilikuwa kabla ya mashirika mbalimbali kujitokeza na kuanza kutoa msaada wa visodo kwa wasichana wetu,” aeleza Teresia Ndulu Mutisya, mwalimu wa sayansi na ushauri nasaha katika shule ya msingi ya Mitaboni.

Lakini hatari kubwa zaidi ya kukosa visodo hasa miongoni mwa wasichana ni ile ya kiafya.

Kunao wanaolazimika kutumia kwa pamoja na wenzao bidhaa za hedhi huku wengine wakitumia vitambaa vikuukuu na matambara kudhibiti damu wakati huu.

Kulingana na Dkt Martin Muhoro, mshauri mkuu wa masuala ya kimatibabu katika kampuni ya kuunda dawa na bidhaa za kiafya ya Novatis, kutozingatia usafi wakati wa hedhi kuna madhara mengi ya kiafya.

“Usafi huu haumaanishi tu kuoga. Usafi huu unahusisha kutumia visodo vinavyofaa na kuvibadilisha kwa wakati ufaao,” aeleza.

Mtaalamu huyu anasema kwamba kuna hatari za kiafya zinazotokana na kutozingatia masuala haya.

“Hatari hizi ni kama vile kukumbwa na maambukizi ya mfumo wa mkojo na ule wa uzazi. Maambukizi haya yaweza sababisha utasa na matatizo wakati wa kujifungua,” aongeza.

Dkt Muhoro pia asema kwamba matumizi ya bidhaa zisizofaa kudhibiti damu wakati wa hedhi, au kutumia visodo kwa muda mrefu, hutoa mazingira mwafaka kwa bakteria kuota kwenye sehemu ya uke.

“Kwa mfano, staphylococcus aureus ni bakteria ambazo zaweza kuingia ukeni na kusababisha toxic shock syndrome; hali hatari inayotokana na maambukizi ya aina fulani ya bakteria,” asema.

Lakini pia ukosefu wa bidhaa hizi umewaweka wasichana wengi katika hatari ya kudhulumiwa kimapenzi, kushika mimba za mapema na hata kuambukizwa virusi vya HIV na maradhi mengine ya zinaa.

Kulingana na Gilbert Ang’ana, mkuu wa shirika la uhisani la Rotary Club of Athi River, kuna uhusiano mkubwa kati ya ukosefu wa visodo na mimba za mapema, vile vile maambukizi ya virusi vya HIV na magonjwa mengine ya zinaa.

“Ukosefu wa visodo huwalazamisha wasichana kuhangaika na hivyo kutumia mbinu yoyote ile kuweza kudhibiti hedhi wakati huu wa mwezi. Hii huwaweka katika hatari ya kunaswa na wanaume ambao huwashawishi kushiriki nao tendo la ndoa ili wawanunulie bidhaa hizi,” afichua.

Mapema mwaka huu 2022, Wizara ya Afya ilifichua kwamba kati ya Januari na Februari 2022, walishughulikia zaidi ya visa 45,000 vya mimba zisizotarajiwa miongoni mwa wasichana walio katika umri wa kati ya miaka 10 na 19.

Aidha, taarifa hiyo ilionyesha kwamba kila wiki wasichana 98 kati ya miaka 10 na 19 wanaambukizwa virusi vya HIV kupitia dhuluma za kimapenzi.

Kulingana na Bw Ang’ana suluhu ni kuhakikisha kwamba hakuna msichana anayekosa bidhaa za hedhi.

“Ndoto hii itatimia tu ikiwa washikadau wanaohusika na masuala ya afya ya hedhi watahakikisha kwamba kila msichana hapa nchini ana uwezo wa kufikia visodo wakati huu wa mwezi,” asema.

  • Tags

You can share this post!

Ngome za Raila zadumisha amani, utulivu

Wabunge na maseneta kufanya kikao cha kwanza Septemba 8

T L