• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
TAHARIRI: Serikali ilijikwaa kwa kutangaza likizo fupi

TAHARIRI: Serikali ilijikwaa kwa kutangaza likizo fupi

KITENGO CHA UHARIRI

JANGA la corona lilipoikumba nchi mwaka 2020, shule zilifungwa kwa miezi sita.

Zilipofunguliwa upya, serikali iliamua kufidia muda uliopotea kwa kuunda ratiba ya masomo iliyo na mapumziko ya siku chache.

Badala ya kufunga kwa mwezi mzima, mbali na ile likizo ya kwanza ya wiki saba, mtindo umekuwa ni kwenda wiki moja pekee.

Ratiba hii imekuwa ikiwaumiza wazazi upande wa karo.

Mzazi kulipa karo mara nne ndani ya mwaka mmoja si jambo dogo.

Lakini mzigo mkubwa zaidi umekuwa kwa watoto, ambao wamekuwa wakisukumwa kuwa madarasani karibu mwaka mzima. Hali hii imefanya wanafunzi kutomakinika, na kuhitaji shughuli nyingine za kuwaondolea shinikizo hizo.

Ndio sababu tunaunga mkono wito wa chama cha Walimu wa Shule za Upili na Vyuo vya Kadri (KUPPET) kwamba serikali ifadhili spoti na shughuli nyingine kama michezo ya kuigiza.

Kutoka nje ya darasa kutawapa nafasi ya kuchangamka na ari mpya ya kuendelea na masomo.

Kwa kuwa hilo halijafanyika, wakuu wa wizara ya Elimu wapaswa kufikiria namna ya kukabiliana na matukio kama yanayoshuhudiwa sasa.

Kuchomwa kwa mabweni na mijengo mingine shuleni, kwa upande mmoja kunatekelezwa na wanafunzi.

Lakini pia kuna uwezekano kuwa walimu na hata wafanyibiashara wa saruji na bidhaa nyingine za ujenzi wanahusika.

Badala ya serikali kuchunguza kwa makini matukio haya na kuja na suluhu ya muda mrefu, wizara ya Elimu ililemewa na presha ya wanafunzi na kubuni likizo fupi.

Awali, likizo hiyo ilikuwa iwe ya wanafunzi wa shule za msingi.

Baadaye, serikali ikawatengea na watoto wa shule za upili likizo yao.Kitendo hiki ni kizuri kwa kuwa wanafunzi wanahitaji mapumziko hayo.

Hata hivyo, ni hatari na inaweza kutumiwa vibaya na wanafunzi siku za usoni.

Wizara ya Elimu ina watu waliosomea saikolojia ya watoto. Tulitarajia kwamba wangetumia hekima na mbinu mbadala kukabiliana na shinikizo hizo.

Kuwatengea wanafunzi likizo eti kwa kuwa wanachoma shule, kutawafanya watekeleze uovu mkubwa zaidi siku zijazo, ili wapate wanachotaka.

You can share this post!

Maskini jeuri wakataa chakula kwa sababu ya siasa

Farasi ni watatu 2022 – Wetang’ula asisitiza

T L