• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 8:46 PM
Farasi ni watatu 2022 – Wetang’ula asisitiza

Farasi ni watatu 2022 – Wetang’ula asisitiza

JUMA NAMLOLA na BRIAN OJAMAA

KINARA wa Ford Kenya Moses Wetang’ula sasa anadai kuwa kinyang’anyiro cha kuelekea uchaguzi wa 2022 ni mbio baina ya farasi watatu wala si wawili jinsi ambavyo imekuwa ikidaiwa na baadhi ya wanasiasa nchini.

Bw Wetang’ula alisema mmoja wa viongozi wa muungano wa One Kenya Alliance, ndiye atakuwa Rais mnamo 2022, akipuuza kuwa ni Naibu Rais au Kinara wa ODM Raila Odinga ndio wako katika nafasi bora ya kutwaa wadhifa huo.

Kando na Bw Wetang’ula, viongozi wengine wa OKA ni Musalia Mudavadi (ANC), Gideon Moi (Kanu), Kalonzo Musyoka (Wiper) na Cyrus Jirongo wa UDM.

Seneta huyo wa Bungoma alisema kuwa OKA itamzindua mwaniaji wake wa Urais mnamo Disemba na kwa sasa wana wataalamu ambao wanaendelea kutathmini umaarufu wa kila mgombeaji ili kuibuka na aliyebora zaidi.

“Sisi kama viongozi wa OKA, tutatembelea kila pembe ya taifa hili kusaka uungwaji mkono na pia kuwaarifu raia kuhusu manifesto yetu, sera na ajenda,” akasema.

Alikanusha kuwa viongozi wa kundi hilo ni vikaragosi wa Rais Uhuru Kenyatta na kufichua kuwa kila mara wamealikwa ikuluni, kiongozi wa nchi amekuwa akiwasihi wadumishe umoja wao ndipo iwe rahisi kwao kushinda kiti cha urais.

Aidha alipuuza madai kuwa wanatumia magari ya serikali kuendesha kampeni zao na mikutano yao iliyofaa kuandaliwa katika Kaunti ya Vihiga wikendi iliyopita haikufutwa na serikali.

“Mpango wetu ulikuwa turejee Nairobi baada ya Kongamano la Wajumbe lililoandaliwa Kakamega. Binafsi sina gari la serikali na iwapo Kalonzo au Raila wanayo, basi pengine ni kwa sababu wanalipwa pensheni,” akaongeza.

Mbunge huyo wa zamani wa Sirisia pia alipuuza madai kuwa Seneta wa Baringo Gideon Moi ndiye amekuwa akifadhili muungano huo.

Kwingineko, Tume ya Kutatua Mizozo ya vyama vya Kisiasa imesimamisha mkutano wa wajumbe wa chama cha Ford Kenya.

Hatua hiyo inatokana na kesi iliyowasilishwa na Bw Crispinus Barasa, aliyetaka kongamano hilo lisimamishwe.

Mwenyekiti wa tume hiyo, Bi Desma Nungo, alitoa uamuzi huo na kutaja kuwa ombi la Bw Barasa ni la dharura, linalostahili kushughulikiwa kwa haraka.

“Tunaposubiri kusikizwa kwa pande zote husika, natoa maagizo kwamba, mkutano mkuu wa wajumbe (NDC) wa chama cha Ford Kenya usifanywe hadi pande zote zisikilizwe,” ikasema taarifa hiyo ya maagizo.

Mkutano huo ulikuwa umepangwa kufanywa Jumamosi, Novemba 6 katika Ukumbi wa Bomas, Nairobi.Agizo hilo la kutoendelea na kongamano hilo la kitaifa linazuia chama cha Ford Kenya, Naibu Katibu Mkuu Millicent Abudho na watu wengine wawili.

“Tume hii inaamuru kwamba pande zote mbili zishiriki kwenye mkutano kwa njia ya Zoom Novemba 15, kuthibitisha kuwa maagizo haya yalitekelezwa,” akasema Bi Nungo.

Mzozo ndani ya chama cha Ford Kenya umesababisha kuzuka makundi mawili.

Kundi moja linaongozwa na Bw Wetangula, jingine likiwa chini ya Mbunge wa Kanduyi, Wafula Wamunyinyi.

You can share this post!

TAHARIRI: Serikali ilijikwaa kwa kutangaza likizo fupi

Waathiriwa wa njaa kupewa pesa

T L