• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 10:50 AM
TAHARIRI: Tuendee nishani nyingi zaidi Tokyo Olimpiki

TAHARIRI: Tuendee nishani nyingi zaidi Tokyo Olimpiki

KITENGO CHA UHARIRI

UMESALIA mwezi mmoja na takribani majuma mawili kabla ya Michezo ya Olimpiki kuanza jijini Tokyo, Japan.

Maadamu msafiri ni aliye bandarini, maafisa wa shirikisho la mchezo wa riadha nchini (AK) kwa ushirikiano na kamati ya kitaifa ya Olimpiki (NOC-K) wanafaa waweke mikakati madhubuti ya kuhakikisha kuwa kikosi cha Kenya kinazoa medali nyingi zaidi iwezekanavyo katika michezo hiyo iliyoahirishwa mwaka jana kutokana na janga la virusi vya corona.

Jinsi ilivyo desturi, Kenya inatarajiwa kutia fora katika mbio za mita 800, 1,500, 3,000 kuruka viunzi na maji pamoja na marathon kwa upande wa wanaume na wanadada.

Hata hivyo, hakuna hakika iwapo taifa hili litang’aa katika mbio za masafa ya mita 5,000 na 10,000 ambazo aghalabu wanariadha wake wakijitahidi sana kwa upande wa wanaume huwa wanazoa nishani ya shaba tu. Hata hivyo, yapo matumaini ya kuridhisha kwa upande wa wanawake hasa katika mita 5,000.

Vilevile mbio za masafa mafupi mathalani za mita 400, 200 na 100 huwa ni nadra sana taifa hili kutoka na kitu -aghalabu huwa linatoka mikono mitupu.

Kwa hakika hilo halifai maadamu tunaamini kuwa nchi hii ina vipawa vingi vinavyoweza kushiriki na kung’aa katika mbio hizo za masafa mafupi. Si kwamba hatujawahi kuzoa medali nzuri katika mbio hizo hususan za mita 400, la hasha.

Jagina marehemu Daniel Rudisha ambaye ni baba yake mshikilizi wa rekodi ya dunia katika mbio za mita 800, David Rudisha, aliwahi kung’aa sana katika masafa hayo katika enzi zake. Hata marehemu Nicholas Bett, majuzi aliwahi kuizolea Kenya dhahabu katika mbio za mita 400 kuruka viunzi.

Hii ina maana kuwa vipawa vya kupambana na mataifa majabari katika vivumbi hivyo kama vile Amerika, Jamaica na nchi za Karibi, vipo, ila tu tumekosa kuzinduka usingizini na kuvichochea.

Kwa hivyo, ni ombi letu kuwa huku macho yetu yakielekezwa zaidi kwa watimkaji wa mbio za masafa ya kadri, vilevile, wakurupukaji wa mbio fupi kama hizo zilizotajwa hapo juu, wapewe kila aina ya msukumo ili wafane.

Kwa mantiki hiyo, tusisahau kuwatia shime na makali tosha wakimbiaji wetu wa mita 10,000 hasa upande wa wanaume ili wafufue fahari yetu iliyotoweka katika masafa hayo.

You can share this post!

CHOCHEO: Chunga ‘mboch’ asijepasha joto kitanda chako

Wazee watakasa madhabahu ya Agikuyu