• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 6:55 AM
TALANTA: Mwanamitindo chipukizi

TALANTA: Mwanamitindo chipukizi

NA RICHARD MAOSI

NYOTA ya binti mdogo Quinn Anna Njoki kutoka Kaunti ya Nakuru inaendelea kung’aa.

Yeye ni mmojawapo ya washiriki nguli katika maonyesho ya urembo wa jukwaani na uanamitindo.

Quinn alianza kujifunza uanamitindo akiwa na umri wa miaka minne nyumbani kwao kwa usaidizi na uangalizi wa mamake Bi Jane Kung’u.

Kuanzia hapo alijiboresha kisha akaanza kushiriki mashindano ya ulimbwende ndani na nje ya eneo la Bonde la Ufa. Hata hivyo, mara ya kwanza haikuwa rahisi kwani alikuwa mwenye aibu nyingi usoni.

“Motisha kubwa inatokana na juhudi zangu kujiamini na pale mashabiki wangu wanapojumuika kunipigia upatu kila mara ninapojitosa jukwaani kufanya mazoezi au kushindana,” asema.

Mwanzoni mwaka wa 2001, Quinn aliteuliwa kuwakilisha Kenya katika michuano ya urembo, ambayo iliyoratibiwa kufanyika Bara Uropa katika jimbo la Batumi, ila hakufanikiwa kusafiri kutokana na mchamko wa homa ya corona iliyokuwa imezagaa kote ulimwenguni.

Hata hivyo, tukio hili halikumkatiza tamaa kwani alielekeza juhudi zake zote kwenye mashindano ya humu nchini .

Anajizatiti kuendelea kupata umaarufu na kwa wakati huo huo kujibidiisha akilenga jina lake linabakie katika madaftari ya kumbukumbu kwa miaka mingi ijayo ambapo siku hizi anajihusisha na miradi ya kuwainua wasiojiweza katika jamii.

Quinn ambaye ni mwanafunzi wa shule ya msingi ya Wizkidds anasema kuwa talanta yake imemsaidia kutangangamana na watu wenye ushawishi mkubwa , na lengo lake kuu ni kufuata nyayo za Lupita Nyong’o.

Aidha, amemudu kujianzishia brandi ya maji ambapo lengo lake kuu ni kuhakikisha kuwa familia maskini, hususan wale wanaotokea katika mitaa ya mabanda wanapata maji safi ya kunywa.

Quinn anaongeza kuwa uanamitindo umemsaidia kujieleza kwa urahisi mbele ya hadhira.Aidha, amemudu kushiriki katika tasnia ya uigizaji bila woga na vilevile kukuza uelewa na ubunifu wake.

“Kwa ustadi wa hali ya juu ninalenga kujiendeleza katika ulingo wa uanamitindo na vilevile kushiriki katika kampeni za kutetea haki za watoto,”asema.

Kwa siku nyingi Quinn anasema ameanzisha miradi ya kupalilia talanta za watoto wa mitaani ambao wana vipaji vya uanamitindo, ili kuwashughulisha waweze kujitambua na kujikubali.

Anasema kwamba nia yake kubwa ni kubadilisha mtazamo wa wanajamii kuhusu stadi ya uanamitindo ambayo bado haijapata mashiko.

Quinn anawashauri wazazi kutoa muda kwa watoto wao ili waweze kuandama ndoto zao kwa kuvilea vipaji walivyo navyo.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru aelekea Pwani kuzindua miradi mikuu

TAHARIRI: Washambuliao wanahabari nao wakabiliwe

T L