• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 10:50 AM
Thailand yahalalisha bhangi licha ya sheria kali za mihadarati

Thailand yahalalisha bhangi licha ya sheria kali za mihadarati

NA MERCY KOSKEI

SERIKALI ya Thailand imelegeza sheria zake za bangi na kuhalalisha matumizi ya bidhaa hiyo huku watumiaji wakiruhusiwa kumiliki na kukuza zao hilo mashambani.

Mabadiliko haya yamejiri baada ya uhalalishaji wa kihistoria wa bangi kama matumizi ya dawa nchini Thailand, ambapo sheria za kupinga dawa za kulevya zinajulikana kuwa na adhabu kali kwa wahalifu.

Kulingana na Waziri wa Afya wa taifa hilo, Bw Anutin Charnvirakul serikali inatumai kuwa biashara ya ndani ya bangi itakuza kilimo na utalii huku ikihimiza wananchi kuipanda.

Alisema kuwa ni fursa kwa wananchi na serikali kupata mapato ya bangi, akiongeza kuwa inatarajiwa kutumiwa kwa ajili ya matibabu na ‘burudani isiyo dhuru’.

“Tayari tumeondoa ile dhana ya kuwa bidhaa hii ni dawa ya kulevya, watu watakaopata fursa kulima bangi watakuwa wanafanya biashara mbalimbali na pia kuiongeza thamani kusaidia maisha yao”, alisema waziri huyo

Wizara ya afya ya umma ya Thailand ilitangaza kuwa bangi itaondolewa kwenye orodha ya mihadarati iliyopigwa marufuku.

Hapo awali, nchi hiyo ilikuwa na msimamo mkali kuhusu dawa za kulevya, huku watu waliokutwa na bangi wakikabiliwa na kifungo cha hadi miaka kumi gerezani na faini kubwa.

Hata hivyo, ingawa kumiliki na kuuza bangi ni halali serikali imeonya dhidi ya kuvuta bangi hadharani kwani kunaweza kusababisha mhusika kukamatwa.

Wanaokiuka sheria hiyo, watatozwa faini ya baht 25,000 ($780) sawa na Sh107, 562 thamani ya pesa za Kenya na kufungwa jela hadi miezi mitatu.

Kwa sasa bangi inatolewa kwa namna mbalimbali za kuvutia watumiaji, huku serikali ikitangaza kuwa inataka watu wanaofika Thailand kuhisi vizuri na sio kulewa.

Tayari, maelfu ya wafungwa waliokabiliwa na mashtaka ya matumizi ya bangi Thailand wameachiliwa huru.

  • Tags

You can share this post!

Vihiga Queens waelekeza macho yote kwa CECAFA

Wazee wa Kaya wadai kumiliki shamba la Mackenzie

T L