• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Tiketi zinavyoweka Ruto mbele ya Raila

Tiketi zinavyoweka Ruto mbele ya Raila

NA KAMAU WANDERI

MWANIAJI wa urais wa muungano wa Azimio-One Kenya, Bw Raila Odinga, anakabiliwa na kibarua kigumu kukabili uasi ambao umeanza kujitokeza katika muungano huo na ngome yake ya Luo Nyanza, kuhusu utata unaokumba shughuli za mchujo wa vyama.

Tayari baadhi ya wagombeaji wa nyadhifa tofauti katika eneo la Luo Nyanza wametangaza kutoridhishwa na hatua ya Bw Odinga kuwapa watu wanaoonekana kuwa washirika wake wa karibu uteuzi wa moja kwa moja katika chama cha ODM.

Kwa mfano, katika Kaunti ya Homa Bay, aliyekuwa gavana wa Nairobi, Dkt Evans Kidero, ameeleza kutoridhishwa na hatua ya Bw Odinga kumpa uteuzi wa moja kwa moja Mwakilishi wa Kike, Gladys Wanga, kuwania ugavana kwenye uchaguzi wa Agosti.

Katika Kaunti ya Kisumu, baadhi ya wawaniaji wameeleza uwepo wa njama za kumpa Gavana Anyang’ Nyong’o uteuzi wa moja kwa moja kutetea nafasi hiyo Agosti.

Njama hizo pia zimetajwa kuwepo katika Kaunti ya Siaya, ikielezwa kuwa ODM inapanga kumpa Seneta James Orengo uteuzi wa moja kwa moja kuwania ugavana.

Ijapokuwa malalamishi kama hayo pia yamejitokeza katia chama cha UDA kinachoongozwa na Naibu Rais William Ruto, wadadisi wanasema kuwa kinyume na Bw Odinga, Dkt Ruto amekuwa akijaribu kudhibiti malalamishi ya wagombeaji wanaoraiwa kuwaachia wenzao baadhi ya nafasi walizolenga kuwania.

“Ingawa hali hiyo inaendelea katika mirengo yote miwili mikuu ya kisiasa (Azimio na Kenya Kwanza), kiwango cha wawaniaji wanaojitokeza kueleza kutoridhika katika mrengo wa Azimio ni kikubwa. Kinaya ni kuwa, wengi wao wanajitokeza katika ngome ya Bw Odinga. Ni hali ambayo haipaswi kushuhudiwa katika wakati huu, kwani anapaswa kufanya kila awezalo kuhakikisha kuwa amedhibiti malalamishi hayo,” asema Bw Wycliffe Muga, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Mdadisi huyo anasema kuwa ikilinganishwa na Dkt Ruto, Bw Odinga ana kibarua kigumu sana kwani mbali na ngome yake, baadhi ya vyama shirika wa muungano vya Azimio-One Kenya vimeeleza “kubaguliwa” kwenye uendeshaji wa shughuli za muungano huo.

Chini ya mwavuli wa vuguvugu la Mwanzo Mpya, vyama hivyo vimetishia kujiondoa katika Azimio ikiwa “havitaheshimiwa”.

Baadhi ya vyama hivyo ni Maendeleo Chap Chap (cha gavana Alfred Mutua wa Machakos), Muungano Party, Chama Cha Uzalendo (CCU) kati ya vingine.

Kwenye kikao na wanahabari, Dkt Mutua alisema kuwa lazima vyama hivyo viheshimiwe na vyama vikubwa kama Jubilee, ODM na Wiper katika uendeshaji wa muungano huo, kwani “vilikuwa miongoni mwa waanzilishi wake”.

Ijapokuwa Bw Odinga aliandaa kikao na viongozi wa vyama hivyo na kuwaahidi kushughulikia matakwa yao, wadadisi wanasema malalamishi hayo yanaashiria kibarua kikubwa alicho nacho, hasa baada ya shughuli za mchujo kukamilika.

“Kimsingi, kila mwanasiasa analenga kuhakikisha amefaidika kisiasa binafsi pamoja na washirika wake. Lengo lao pia ni kuhakikisha wanaruhusiwa kuwasimamisha wagombea katika ngome zao kupitia vyama hivyo ili kuimarisha usemi na ushawishi wao kisiasa. Ni hali itakayowasaidia kupata mgao wa serikali Agosti, ikiwa muungano huo utaibuka mshindi kwenye uchaguzi huo,” asema Bw Dismus Mokua, ambaye ni mchanganuzi wa siasa.

Mdadisi huyo anaeleza kuwa, ikizingatiwa bado kuna nafasi ya wanasiasa kujiondoa kutoka mrengo mmoja wa kisiasa hadi mwingine, ni wakati mwafaka wa Bw Odinga kuchukua tahadhari za mapema kuhakikisha baadhi ya washirika wake hawamhepi na kuhamia katika mirengo mingine tofauti.

“Lazima abuni mkakati kudhibiti malalamishi hayo, hasa uchaguzi mkuu unapokaribia, kwani uwepo wa migawanyiko utazua taswira mbaya na kutia doa sana kampeni zake,” akasema Bw Mokua.

Baada ya malalamishi mengi kuibuka, wataalamu waliozungumza na ukumbi huu wamefichua kuwa Dkt Ruto anajitahidi awezavyo kukwepa migawanyiko katika zizi lake. Ameripotiwa kuhakikisha kuwa kila mwaniaji hasa katika ngome yake ya Rift Valley, anaalikwa kuhutubia umma kwenye mikutano yake ya kisiasa kama njia ya kudumisha uwazi na demokrasia katika chama.

  • Tags

You can share this post!

Dhehebu ‘jipya’ katili laendeleza ukeketaji wa watoto...

JUNGU KUU: Ukosoaji wa Ruto wamletea presha

T L