• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Ufugaji mbwa wa ulinzi wamlipa tangu aache kazi ya matatu

Ufugaji mbwa wa ulinzi wamlipa tangu aache kazi ya matatu

NA SAMMY WAWERU

KIJIJI cha Mugoya, kilomita tano kutoka mji wa Embu, Akilimali inakutana na Martin Gathungu akihudumia mbwa wake.

Boma lake lenye ukubwa robo ekari, licha ya kuwa na ua wa nyaya, Gathungu anaridhia wanyama hao kudumisha usalama.

“Mgeni anapotutembelea, lazima niwafungie,” asema.

Anafunga kwa nyororo jibwa linaloonekana kuwa na ukali, likibweka mfululizo. Gathungu analisifia kuwa jasiri, kakamavu na rafiki unapozoeana nalo, hulka muhimu katika ulinzi.

Kizimbani, mbwa mwingine anahisi uwepo wa mgeni na kutuma onyo.

“Huyu naye ni Rottweiler, ambaye ni bora kuimarisha usalama,” aelezea.

Ufugaji mbwa, ni biashara aliyoanzisha ugonjwa wa Covid-19 ulipoingia nchini mwaka 2020.

Martin Gathungu ni mfugaji wa mbwa eneo la Mugoya, Kaunti ya Embu. PICHA | SAMMY WAWERU

Alikuwa katika sekta ya uchukuzi, ambayo ilisambaratika kufuatia mikakati na sheria zilizowekwa kuzuia msambao wa virusi vya corona.

Akiwa amewekeza kwenye sekta hiyo kwa muda wa miaka kumi, alikuwa amemiliki matatu tatu. Zilihudumu kati ya Tharaka Nithi, Embu na Nairobi.

“Gari lililokuwa likiniingizia Sh5,000 kwa siku, mapato yalishuka hadi baina ya Sh500 – 1,000, madereva nyakati nyingine wakikosa kuingia kazini,” akumbuka, akilalamikia ugumu wa biashara hiyo kipindi cha corona.

Gathungu anasimulia kwamba hakuwa na budi ila kuyaegesha, kwa kile anataja kama “kuanza kula akiba yake kuyaweka mafuta au yanapoharibika”.

Ni baba wa watoto wawili, na anasema tangu utotoni mwake aliridhishwa na majibwa ya askari.

Kuafikia hamu yake, miezi kadha aliyoegesha matatu aliamua kujaribu ufugaji.

“Nilifanya utafiti mitandaoni, nikaanza na aina ya German shepherd,” adokeza.

Mtaji

Aidha, alinunua mbwa wa kike na kiume wote wakimgharimu Sh60,000. Hali kadhalika, alifanya ujenzi wa makazi.

Anaelezea kwamba walijifungua vilebu watatu, kila mmoja akiuza Sh20,000.

“Awamu ya pili, nilifuga Rottweiler ambapo nilinunua mmoja wa kike Sh80,000,” asema.

Huduma za kujamiisha alikodi kutoka kwa mzalishaji mwenza, na mwaka mmoja baadaye alijifungua watoto 14.

Kila mmoja, kulingana na Gathungu alimuingizia Sh30,000.

Miaka miwili baadaye, amegeuka kuwa mfugaji hodari na zaidi ya yote mzalishaji vilebu; biashara anayosisitiza hajutii kamwe kuingilia.

Ana makazi mawili, kila moja likiwa na ukubwa wa futi 10 kwa 10. Wakati wa mahojiano na mjasirimali huyu, alikuwa na jumla ya German shepherd 17 ambapo 10 wakiwa waliokomaa na waliosalia ni wadogo.

Rottweiler alikuwa na mmoja, aina ya maltese majuzi akijifungua vilebu wanne.

“Biashara yangu ni ya kujamiisha na kuzalisha. Wanapofikisha miezi miwili au mitatu, ninawauzia wafugaji kwa minajili ya ulinzi na wengine ‘vipenzi’,” akasema.

Mbwa mdogo aliyesajiliwa chini ya East Africa Kennel Club huuza zaidi ya Sh60,000, huku ambaye hajaandikishwa Sh30,000.

Mbwa huzaa siku 58 – 68 baada ya kujamiishwa, Gathungu, 37, akisema wake hujifungua kati ya vilebu 3 – 14.

Magonjwa sugu kwa mbwa ni Homa ya Matumbo ya Salmonella na virusi vya Parvo.

Wataalamu wanaonya kuhusu Parvo kwa vilebu walio chini ya miezi sita, hasa ikiwa mama mzazi hakuwa amechanjwa.

“Ni muhimu kuwapa mbwa chanjo ya DHLP kila mwaka,” ashauri Dkt Peter Akunda, mtaalamu wa mbwa.

Pia ipo haja ya kukabili kupe na viroboto.

You can share this post!

Esse Akida atuzwa kiatu cha dhahabu kwa kuibuka mfungaji...

Shabana yawika baada ya ushindi

T L