• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 7:50 AM
Mivutano Azimio inavyohujumu mipango ya Raila kuingia Ikulu

Mivutano Azimio inavyohujumu mipango ya Raila kuingia Ikulu

NA CHARLES WASONGA

VUTA nikuvute ndani ya muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya huenda ikavuruga ndoto ya mgombeaji wake wa urais Raila Odinga za kushinda katika uchaguzi mkuu mwaka huu.

Huku ikisalia miezi minne kabla ya Wakenya kuelekea debeni Bw Odinga angali anakabiliwa na kibarua cha kushughulikia matakwa chungu nzima kutoka na chama cha Wiper, kwa upande mmoja, na vyama vingine vidogo katika muungano huo, kwa upande mwingine.

Hata baada ya muungano huo kusajiliwa rasmi katika Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa mapema wiki hii, chama cha Wiper kingali kinapinga mambo kadhaa yaliyomo kwenye mkataba uliobuni muungano na muundo wa baraza kuu la uongozi.

Kwa mfano, chama hicho kinachoongozwa na makamu wa rais wa zamani Kalonzo Musyoka kinapinga sehemu ya mkataba huo inayosema kuwa vyama tanzu haviwezi kujiondoa kutoka Azimio miezi sita baada ya kusajiliwa kwake.

Pili, Bw Musyoka anapinga hatua ya Bw Odinga kuongeza idadi ya wanachama wa baraza kuu la muungano huo kutoka watu saba hadi 12 ili kujumuisha wawakilishi kutoka vyama vingine.

Bw Musyoka amekuwa akiendeleza dhana kuwa Azimio ni muungano wenye mirengo mitatu mikuu; ODM, Jubilee na washirika wake na uliokuwa muungano wa One Kenya Alliance (OKA).

Lakini kundi la viongozi wa vyama vingine wakiongozwa na Gavana Alfred Mutua (Machakos) na Kivutha Kibwana (Makueni) walilalamikia kile walichodai ni kutengwa katika kitovu cha kufanya maamuzi katika Azimio huku wakitishia kujiondoa.

Bw Odinga alilazimika kufanya mazungumzo na kundi hilo ambalo lilibuni muungano mdogo kwa jina Mwanzo Mpya likidai ndilo nguzo ya Nne katika muungano wa Azimio.

Hii ni baada ya Dkt Mutua, ambaye ni kiongozi wa chama cha Maendeleo Chap Chap, kutishia kujiunga na muungano wa Kenya Kwanza unaoongozwa na Naibu Rais William Ruto.

Kwa upande mwingine, kiongozi wa chama cha United Democratic Movement (UDM) Gavana Ali Roba ameisuta ODM kwa kile alichotaja kuwa ni uchu wake wa kutaka kudhibiti shughuli zote za Azimio na kuvitenga vyama vingine.

“Tunaiambia ODM ikome kabisa kujifanya kama kiranja wa vyama vyote ndani ya Azimio. Watu kama Bw (Edwin) Sifuna wakome kabisa kudharau vyama vingine kama UDM. Hata hivyo, ninataka kumhakikishia Raila kwamba

kelele za watu kama Sifuna hazitazuia kuendelea kumfanyia kampeni ili aingie Ikulu,” Bw Roba akasema Jumatano jijini Nairobi alipotoa vyeti vya uteuzi kwa wagombeaji mbalimbali wa UDM.

Miongoni mwa waliopewa vyeti vya uteuzi ni aliyekuwa Mbunge wa Rarieda Nicholas Gumbo atakayepambana na Seneta wa Siaya James Orengo katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Siaya; anakotoka Bw Odinga. Bw Gumbo na aliyekuwa msemaji wa polisi Charles Owino waligura ODM na kujiunga na UDM baada ya ODM kumpa Bw Orengo tiketi ya moja kwa moja.

Kadhalika, mvutano kuhusu nafasi ya mgombeaji mwenza wa Bw Odinga imeibua migawanyiko wa kimawazo katika muungano huo wa Azimio.

Hadi Ijumaa wiki hii, viongozi wa Wiper walikuwa wakishikilia kuwa sharti nafasi hiyo ipewe Bw Musyoka kwa sababu, mbali na Bw Odinga, yeye ndiye kiongozi mwenye tajriba kubwa zaidi katika muungano huo.

Hii ni tofauti na dhana ya awali kwamba nafasi hiyo ilitengewa eneo la Mlima Kenya ili kunasa sehemu kubwa ya kura milioni tano kutoka eneo hilo na hivyo kuvuruga hesabu za Dkt Ruto.

Wanasiasa kutoka eneo hilo wanaopigiwa upatu kutunikiwa nafasi hiyo ni aliyekuwa Mbunge wa Gatanga Peter Kenneth, kiongozi wa Narc Kenya Martha Karua na Waziri wa Kilimo Peter Munya.

Lakini naibu kiongozi wa chama cha DAP-K, Ayub Savula Ijumaa alisema vyama vyote tanzu katika Azimio sharti vishirikishwe katika harakati ya kusaka mgombea mwenza.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru atakavyodhibiti serikali ya Raila

Red Devils wafufuka Spurs na Arsenal wakila marungu

T L