• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
UJAUZITO NA UZAZI: Kiungulia kwa mama mjamzito na njia za kukipunguza

UJAUZITO NA UZAZI: Kiungulia kwa mama mjamzito na njia za kukipunguza

NA MARGARET MAINA

[email protected]

KIUNGULIA cha ujauzito ni miongoni mwa matatizo wanayokumbana nayo wanawake wengi wanapobeba mimba.

Kiungulia ni hali inayosababisha mtu ajihisi kuungua au kama kwamba kuna kitu kinawaka moto katika sehemu ya katikati mwa kifua.

Tatizo hilo huwapata wajawazito mara nyingi katika miezi mitatu ya mwisho ya ujauzito, lakini pia wapo akina mama wajawazito wanaokabiliwa na kiungulia miezi ya mwanzo ya mimba.

Ili kuelewa namna ya kuzuia kiungulia kisitokee, ni bora kwanza tufahamu kiungulia kinasababishwa na nini wakati wa mimba.

Kiungulia hutokea wakati kiwambo (au valvu) kilichopo kati ya tumbo na umio kinapolegea na kushindwa kuzuia asidi ya tumbo isipenye na kurejea katika umio.

Mimba huongeza kiungulia kwa sababu homoni ya progesterone hulegeza kiwambo hicho. Hivyo, asidi inayozalishwa tumboni hasa baada ya kula hurejea katika umio na kuleta kiungulia.

Kiungulia hutokea katika miezi mitatu ya mwisho ya mimba kutokana na fuko la uzazi kuwa kubwa na kubana utumbo mdogo na tumbo. Mbano huo wa tumbo husababisha vilivyoko tumboni kusukumwa upande wa umio.

Kwa kawaida kutokula vyakula vyenye kusababisha asidi na gesi tumboni, hupunguza kiungulia.

Vyakula hivyo ni kama vinywaji vyenye gesi ya kaboni, vyakula vyenye kiasi kikubwa cha asidi kama vile jamii ya maharagwe kama maharagwe, kunde, mbaazi na kadhalika, nyanya, vyakula vyenye viungo, matunda kama machungwa na juisi ya machungwa, chokoleti, vyakula vyenye mafuta mengi, na hata kitunguu saumu. Lakini pia inategemea mtu inabidi ujichunguze na kuona ni vyakula gani ukila unapata kiungulia na gesi.

Zifuatazo ni njia za kuzuia kiungulia:

Kutumia baadhi ya dawa salama zinazozuia kiungulia na gesi wakati wa ujauzito. Muhimu ni kupata ushauri wa daktari ili ujue unafaa kutumia dawa gani ya kuondoa kiungulia ambayo ni salama wakati wa ujauzito.

Hakikisha unakula kiasi kidogo cha chakula na usile ukashiba sana. Kwa kuwa mama mjamzito huwa anasikia njaa mara kwa mara na anahitajia kula vyema ili aujenge vizuri mwili wake na wa mtoto au watoto, basi ni bora chakula chake ukigawe katika sehemu kadhaa ndogo, na ale mara kadhaa, badala ya kula sana wakati mmoja. Kwa kufanya hivyo, tumbo halijai sana na hivyo kusaidia kuzuia asidi isipande juu ya tumbo na kusababisha kiungulia na gesi.

Jitahidi usinywe maji mengi sana baada ya chakula au wakati wa kula, kwani husaidia kuzalisha asidi tumboni kwa haraka na kuleta kiungulia.

Unaweza kula ubani au ukatafuna gamu baada ya kula. Ubani hutengeneza mate na mate hupunguza asidi.

Jitahidi usilale tu mara baada ya kula. Subiri kama muda wa nusu saa hivi upite ndipo ulale. Unapolala, usilaze kichwa moja kwa moja bila mto. Egemeza kichwa chako kwenye mto ili kuzuia asidi isirejee juu ya tumbo na kusababisha kiungulia.

Unapohisi kiungulia, kunywa angalau maziwa glasi moja au mtindi.

Na kama hali hiyo haijatoweka, kunywa maji ya moto glasi moja yaliyowekwa kijiko kimoja cha asali.

You can share this post!

Namna ya kuondoa harufu mbaya kwenye viatu

Sngura wa siasa wasiojua baridi

T L