• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 9:50 AM
Namna ya kuondoa harufu mbaya kwenye viatu

Namna ya kuondoa harufu mbaya kwenye viatu

NA MARGARET MAINA

[email protected]

HARUFU mbaya katika viatu na vifaa vya kuhifadhia kama vile mifuko ya mazoezi na mikoba inaweza kuwa kero kuu.

Harufu hii husababishwa na bakteria na aina fulani za kuvu.

Kuna njia kadhaa za ubunifu za kuondoa harufu za kunuka.

Tatizo la mtu kunuka miguu na viatu kutoa harufu mbaya huwa kero kwa mtu mwenyewe na watu wengine.

Mtu anapovaa viatu vya kufunika muda mrefu na itokee labda mtu yupo kazini asubuhi hadi jioni na tena amevaa soksi, husababisha joto ndani ya viatu.

Jasho kutoka miguuni linaingia mpaka kwenye soksi na viatu vyenyewe, na sababu hewa inakua haipiti miguuni, hapo ndipo viatu na miguu vinaanza kunuka.

Pia kwa wengine hali hii inatokana na kutofua soksi, na kutosafisha viatu mara kwa mara na kuacha fangasi miguuni bila kutibia kwa muda mrefu.

Kuondoa tatizo la harufu mbaya miguuni na kwenye viatu wala sio kazi kubwa. Ni kuzingatia tu usafi wa miguu na viatu.

Kila jioni mtu mwenye tatizo hili anatakiwa aoshe miguu yake vizuri akitumia maji ya ufufutende na sabuni yenye dawa kama Dettol, hasa katikati ya vidole, kisha akaushe vizuri, na kuiacha ipate hewa.

Usirudie kuvaa soksi bila kuzifua kwanza kwa sababu harufu mbaya itakolea. Na hakikisha unavaa soksi ambazo zimekauka vizuri kwa sababu zikiwa na ubichi zitaongeza matatizo zaidi.

Usirudie kuvaa viatu hivyo hivyo mara kwa mara. Mtu mwenye tatizo la kutoa harufu kwenye miguu na viatu, anatakiwa awe na angalau viatu jozi tofauti ili akivaa moja leo kesho anavaa nyingine huku ile jozi nyingine akiwa ameianika pahala pakavu penye hewa ya kutosha ili kukausha unyevu nyevu ndani ya viatu. Kufanya hivyo kunasaidia sana kupunguza harufu.

Ili kuondoa harufu kwenye viatu, ni vizuri viatu vikasafishwa vizuri na kuachwa vikauke. Viatu vinavyoweza kufuliwa kama raba ni vizuri kufanya hivyo mara kwa mara na kuachwa juani vikauke. Viatu vingine kama vya ngozi, utaviosha kwa kuchukua baking soda au poda ambapo unanyunyuzia ndani ya viatu kisha unavianika hata kwa muda wa saa moja au zaidi, kisha vitoe uvikung’ute na uvisafishe kwa ndani kwa kitambaa kikavu na uviache vipate hewa. Baking powder inasaidia sana kutoa harufu.

Unaweza pia ukaweka Dettol ya maji kidogo au maji ya ndimu kwenye pamba kisha unatumia kusafisha viatu kwa ndani. Ukimaliza weka maganda ya ndimu au chungwa ndani ya viatu, au tea bags au maua ya jasmini, au maua yoyote yenye harufu nzuri. Ukishafanya hivyo, weka viatu katika sehemu yenye hewa safi na kivuli kwa muda mrefu ili kusaidia kuondoa harufu mbaya.

Kama una fangasi miguuni, tafuta dawa na uzitibu mara moja kwani ni hatari. Bila kufanya hivyo, harufu mbaya itazidi miguuni na inaweza hata ikasababisha miguu kuoza.

Paka poda (poda za watoto) miguuni kusaidia miguu kuwa mikavu kabla ya kuvaa viatu hasa katikati ya vidole.

You can share this post!

Kibarua kigumu mrithi wa Natembeya akianza kazi

UJAUZITO NA UZAZI: Kiungulia kwa mama mjamzito na njia za...

T L