• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
VYAMA: Malenga Wamilisi, wasanii waliotopea katika utunzi mpevu wa mashairi

VYAMA: Malenga Wamilisi, wasanii waliotopea katika utunzi mpevu wa mashairi

NA CHRIS ADUNGO

MALENGA Wamilisi ni kundi la wasanii linajumuisha watunzi wa mashairi wenye umilisi katika utanzu huu wa fasihi.

Kundi hili lilibuniwa na walimu Elisha Otoyi, Momanyi Henry Rioba, Alfred Lobawoi na Timothy Omusikoyo Sumba mnamo Februari 2021.

Pindi baada ya kuasisiwa, wapenzi wa Kiswahili walifurika kundini nao wakaleta ndugu na marafiki zaidi. Wingi huo wa washairi ulilipa kundi uthabiti wa hali ya juu na bado linazidi kukita mizizi, kustawi na kunawiri. Ama kweli elfu huanza na moja! Sawa na makundi mengine ya kupigia Kiswahili chapuo, kundi hili linalenga kukuza vipaji vya watunzi chipukizi na kuwaboresha waandishi waliobobea.

Linaazimia pia kutunga na kuandika diwani za ushairi, hadithi za umilisi (kwa watoto), riwaya, tamthilia na hadithi fupi. Madhumuni mengine ya kundi hili linalojivunia zaidi ya wanachama 100 kufikia sasa, ni kukitetea Kiswahili nchini Kenya na kuchangia makuzi yake kote ulimwenguni.

Watunzi hupakia mashairi yao kwenye kundi la mtandaoni la ‘Malenga Wamilisi’ ili kuburudisha na kufunza hadhira zao. Masuala ibuka yanayogonga vichwa vya habari katika sekta ya elimu pia hujadiliwa kundini kwa sababu robo tatu ya wanachama ni walimu na wanataaluma wanaojihusisha na masuala ya elimu kwa namna moja au nyingine.

Kundi hili pia ni ukumbi wa maswali mwafaka ambayo hujibiwa papo kwa hapo na wanachama. Mizaha na utani pia hupenyezwa kiasi fulani. Hakuna dawa nzuri kuliko kichekesho!

Mbali na usawa wa kijinsia, uwakilishi wa kimaeneo pia umezingatiwa. Hali hiyo imewezesha kundi kuchota mawazo na maarifa kemkem kutoka kwa jamii na tamaduni mbalimbali. Wanachama wote ni sawa pasipo kujali rangi, tabala wala imani.

Baadhi ya kazi za kundi hili ambazo tayari zimechapishwa ni: Malenga wa Afrika, Wosia na Mashairi Mengine, Malenga wa Kenya (Gredi ya 1, 2, 3), Malenga wa Kenya (Gredi ya 4, 5, 6), Tasnia ya Ushairi, Wasifu wa Timothy Sumba na Game of Wits (Antholojia ya Kiingereza).

  • Tags

You can share this post!

Ujenzi wa kituo cha kisasa kutoa mafunzo na huduma za...

Rotich aonya wapinzani mita 800 akielekea Botswana kujinoa

T L