• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Ujenzi wa kituo cha kisasa kutoa mafunzo na huduma za kilimo Kabete kuanza

Ujenzi wa kituo cha kisasa kutoa mafunzo na huduma za kilimo Kabete kuanza

NA SAMMY WAWERU

UJENZI wa kituo cha kisasa kitakachokuwa kikitoa mafunzo ya kilimo katika Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN), bewa la Kabete unatarajiwa kuanza mwishoni mwa mwezi huu wa Aprili.

Kampuni ya pembejeo ya Elgon Kenya mwaka 2021, ilitia saini mkataba wa makubaliano na UoN kujengea chuo hicho ambacho hasa ni taasisi ya teknolojia ya kisasa.

Kituo hicho kinalenga kunoa wanafunzi, kutoa mafunzo kwa wakulima, kupitia mifumo ya kisasa kuendeleza kilimo.

Vilevile, kitakuwa kikiandaa maonyesho ya kilimo, yatakayojumuisha kutoa mafunzo ya matumizi ya pembejeo, taratibu bora kitaalamu kuendeleza kilimo na kuonyesha vifaa, mashine na mitambo ya kileo kuboresha zaraa.

“Tunasubiri Halmashauri ya Jiji na asasi husika za ujenzi kutoa vibali, ujenzi uanze mwishoni mwa mwezi huu – Aprili,” Mkurugenzi Mkuu Elgon Kenya, Dkt Bimal Kantaria akaambia Taifa Leo.

Kampuni hiyo itatoa ufadhili kufanya ujenzi. Bajeti, shughuli hiyo inakadiriwa kugharimu kati ya Sh40 – 50 milioni.

Bewa la UoN Kabete ni tajika katika utoaji mafunzo ya ufugaji na kilimo.

Wakati huohuo, Elgon Kenya imetangaza kiwanda cha kutengeneza fatalaiza kulingana na mahitaji ya shamba la mkulima kinatarajiwa kuanza kutoa huduma hivi karibuni.

“Tunasubiri Shirika la Kutathmini Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBS) kukagua sampuli za mbolea, ili tuanze kuhudumia wakulima,” akadokeza Dkt Kantaria.

Fatalaiza maalum itakuwa ikiundwa baada ya mkulima kupimiwa udongo wa shamba lake, kubaini virutubisho vinavyohitajika kuuboresha.

Kampuni hiyo ina maabara ya kisasa kupima udongo, kiwango cha asidi na laimu (pH).

“Kiwango anachohitaji mkulima tutakuwa tukimtengenezea,” afisa huyo akasema, akiridhia hatua hiyo kwa kile alitaja kama “itakayoletea afueni sekta ya kilimo nchini”.

Elgon Kenya ni msambazaji mkuu wa pembejeo za kilimo; mbegu, mbolea na dawa, Afrika Mashariki na Kati.

  • Tags

You can share this post!

Siku Kibaki alikosa sahani katika hafla ya Moi

VYAMA: Malenga Wamilisi, wasanii waliotopea katika utunzi...

T L