• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:50 AM
Wakazi wa Kawangware wapumua hewa safi kwa mara ya kwanza katika miaka mingi

Wakazi wa Kawangware wapumua hewa safi kwa mara ya kwanza katika miaka mingi

Na FRIDAH OKACHI

Hewa safi katika mitaa ya Kawangware na Kangemi imeanza kushuhudiwa huku Kaunti ya Nairobi ikijiandaa kwa Mvua ya El Nino kwa kuhakikisha kwamba mabomba ya kupitisha maji safi yanazibuliwa.

Kwa wakazi wa Kawangware na Kangemi wanaoishi karibu na Mto Nairobi, hali ni tofauti; wale wasio na shughui za kila siku wakihusika  kusafisha mto huo ili kuepuka uvundo ambao umekuwa ukiwakosesha usingizi.

Teresia Wairimu ambaye ni mkazi wa mtaa huo, amesema kuwa shughuli hiyo imemnufaisha kwa kuwa hewa imebadilika ikilinganishwa na hapo awali.

“Zamani nilikuwa natamani kuhama,hewa ilikuwa chafu lakini sikuweza sababu sikuwa na pesa za kuhama. Kazi sipati kila siku na nikisema nipande huko juu, sitaweza kulipa Sh4,000 kwa mwezi,”  Wairimu akaambia Taifa Leo.

Wairimu, anakiri kwamba licha ya kusubiri kwa muda mrefu, maombi yao yamejibiwa, wakifurahi kuona mabadiliko chanya yakifanyika.

Mwenyeketi wa shirika la kijamii la Maumau linaloshughulikia mazingira, Pius Wahu Namasaka, alisema shirika lao limekuwa likihusisha vijana na wazee kwenye eneo hilo kuhakikisha wanaishi kwenye sehemu ya  mazingira safi.

Hata hivyo, shirika hilo limekuwa likitafuta vijana na wazee ambao hawana kazi na kuwashirikisha, jambo analojivunia.

Namasaka aliongezea kuwa licha ya vijana kutoka eneo hilo kusafisha mto huo, ni bora washikadau katika maeneo mengine kuhakikisha mto huo unasafishwa ili kuondoa rangi ya maji hayo ambayo yamengeuka kuwa majano.

Miaka ya awali maji hayo yalitumika kwenye shughuli za nyumbani.

Wamiliki wa nyumba katika eneo hilo ambao wako karibu na Mto Nairobi, ndani ya mita kumi kutoka kwenye mto huo, wamehimizwa  kuondoka.

Wanachama wa shirika la Maumau linaloshughulika na mazingira wakifanya usafi katika Mto Nairobi. Picha zote|Fridah Okachi

Mbunge wa Dagoretti Kaskazini Beatrice Elachi alishirikisha mamlaka ya rasilimali – water resources authority  kuwasaidia wakazi hao kwenye shughuli ya usafishaji wa Mto Nairobi ambao ulikuwa na samaki za kuliwa, maji ya kutumika nyumbani na kivutio cha watalii.

Watalii walitembelea sehemu hiyo kufahamu vipi maji hayo yanapita kwenye mtaa wa mabanda.

Elachi anawaonya wale wanaoishi karibu na mto huo, kuondoka na kupa mto huo nafasi wakati mvua itakapoanza kunyesha.

Mto huo ambao umesafishwa kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa, kwenye  uzinduzi wa kuendeleza kusafisha mto huo na mamlaka ya rasilimali ya maji, imewataka wamiliki wa nyumba kukosa kuachilia majitaka kwenye mto huo.

Mamlaka ya rasilimali ya maji mjini Nairobi, ina matumaini kuwa samaki waliokuwa kwenye maji hayo watarejea na maji hayo kutumika tena upya iwapo kampuni za hapa nchini zitawacha kuruhusu kemikali kupita kwenye mto huo.

Utafiti unaonyesha kuwa mtaa wa Mathare, Kawangware na Kibera umeathirika na uchafuzi wa mto. Idadi ya watu wanaoishi karibu na mto huo ni zaidi ya 200,000.

  • Tags

You can share this post!

Tanzania yaishiwa na dola za Marekani miezi michache baada...

Tumeitwa Haiti kwa sababu dunia nzima inajua sisi hatucheki...

T L