• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:50 AM
Tanzania yaishiwa na dola za Marekani miezi michache baada ya kuikejeli Kenya

Tanzania yaishiwa na dola za Marekani miezi michache baada ya kuikejeli Kenya

NA WANDERI KAMAU

TANZANIA imeanza kununua dhahabu kutoka kwa raia wake, ili kuongeza hifadhi yake ya fedha za kigeni, imesema Benki Kuu ya taifa hilo kwenye taarifa.

Benki hiyo ilieleza mpango wake wa kuanza kununua dhahabu mwishoni mwa Agosti.

Kinaya ni kuwa, hatua hiyo inajiri miezi michache baada ya Rais Samia Suluhu wa taifa hilo kuikejeli Kenya kimafumbo kwa uhaba wa dola za Amerika nchini.

Mnamo Ijumaa, Septemba 29, 2023, Gavana wa benki hiyo, Emmanuel Tutuba, alisema wanapanga kununua tani sita za dhahabu kutoka kwa wachimbaji wadogo, wale wa kiwango cha kadri na wafanyabiashara wengine kufikia mwishoni mwa mwaka huu.

Alisema kuwa tayari, wamefanikiwa kununua na kuuza kilo 418 za madini hayo muhimu.

“Benki hii inanunua dhahabu kwa pesa za Tanzania kutoka kwa wachimbaji dhahabu na wafanyabiashara wengine,” akasema gavana huyo kwenye taarifa.

Mnamo Machi, Bi Suluhu aliikejeli Kenya kwa kutokuwa na kiwango cha kutosha cha dola, akisema Tanzania ndilo taifa lenye uchumi thabiti katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Akihutubu wakati wa Siku ya Kimataifa ya Wanawake, kiongozi huyo aliwaambia Watanzania kufurahia hali ya uchumi wao, kwani uko katika hali nzuri kuliko majirani wake.

“Watanzania, msiruhusu yeyote kumdanganya. Tuko katika hali nzuri kiuchumi kuliko majirani wetu. Hifadhi yao ya dola haiwezi kudumu kwa wiki moja, wakati yetu inaweza kukaa kwa hadi miezi minne. Wako hapa wakituomba dola ili kununua mafuta,” akasema Bi Suluhu.

Kauli ya Rais Suluhu ilijiri siku kadhaa baada ya Waziri wa Fedha, Prof Njuguna Ndung’u, kuwaambia Wakenya kujitayarisha kwa hali ngumu ya kiuchumi mwaka huu.

Hapo awali, gazeti moja nchini Tanzania lilikuwa limeripoti kwamba benki za Kenya zilikuwa zimemaliza hifadhi zake za dola, na zilikuwa zikiiomba Tanzania.

  • Tags

You can share this post!

Kinaya Kenya Kwanza ikipeana ardhi ya chuo licha ya...

Wakazi wa Kawangware wapumua hewa safi kwa mara ya kwanza...

T L