• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Wakristo Mwea wadaiwa kukumbatia ushirikina, nyuki wakitumika kuhangaisha watu

Wakristo Mwea wadaiwa kukumbatia ushirikina, nyuki wakitumika kuhangaisha watu

Na MWANGI MUIRURI

MUUNGANO wa Makasisi wa dini asili katika Kaunti ndogo ya Mwea iliyoko Kaunti ya Embu umekemea wengi wa wenyeji kwa kukumbatia ushirikina licha ya kujihusisha na Ukristo.

Mwenyekiti wa muungano huo Askofu Stephen Njagi, akiongea katika mtaa wa Makutano alisema kwamba nyingi za jamii za eneo hilo licha ya kujihusisha na injili ya Kikiristo, ni washirikina.

Mwaka wa 2015, serikali ya Kaunti ya Embu ilikuwa imependekeza mikakati kutoza ushuru sekta ya ushirikina lakini makasisi wakaungana pamoja kupinga wakisema hiyo ilikuwa sawa na kuhalalisha uchawi.

Askofu Njagi aliteta kuwa washirikina katika kaunti hiyo hutoa huduma zao hadharani na ada zao huwa za chini hivyo basi kuvutia wengi.

“Inafedhehesha kwamba Wakristo wengi katika eneo pana la Mbeere Kusini na Kaunti ya Embu kwa ujumla wamekumbatia nguvu za giza. Kwa wengi, Mungu ni wa kuabudiwa Jumapili lakini katika maisha yao ya siku zingine, uchawi ndio nguvu zao,” akasema.

Askofu Njagi alikerwa na hali ambapo visa vya nyuki kuvamia wenyeji wakiwa wametumwa kiuchawi vimezidi eneo hilo.

“Kila kuchao tunazidi kushuhudia visa ambapo nyuki huvamia raia na hata vituo vya polisi wakisaka washukiwa wa visa tofautitofauti,” akasema.

Mkuu wa Kaunti ndogo ya Mwea Bi Jane Manene alisema kwamba visa vya aina hivyo ni vya kawaida eneo hilo.

“Mimi siamini ushirikina lakini haya mambo ya nyuki kuvamia watu na kasheshe kuzuka eti ni ishara za uchawi yamekuwa kawaida,” akasema.

Askofu Njagi aliteta kuwa “watoto wetu wanashawishika kuwa nguvu za giza huzua afueni kwa changamoto za kimaisha kama wizi”.

Hata hivyo, Askofu Njagi aliwataka wenyeji wawekeze imani yao kwa maombi na wakome kutoa mali yao kwa wachawi ili kujipa afueni za kimaisha.

 

[email protected]

 

  • Tags

You can share this post!

Akothee awakemea wanaodai mumewe mzungu ‘amesota’  

Mbunge afichua kanisa Nairobi waumini hushiriki ngono bila...

T L