• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:50 AM
Walio wanene kupindukia kwenye hatari ya kuvunjika miguu ovyo

Walio wanene kupindukia kwenye hatari ya kuvunjika miguu ovyo

NA MWANDISHI WETU

UNENE kupindukia miongoni mwa wanaume umehusishwa na matatizo tele ya kiafya. Wanaume wanene kupita kiasi wanaandamwa na matatizo kama vile shinikizo la damu, maradhi ya moyo, kisukari, kuishiwa hamu ya mapenzi, na hata kupungua kwa nguvu za kiume.

Lakini utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Chicago nchini Amerika umebaini kuwa wanaume wanene kupindukia pia wana mifupa dhaifu (osteoporosis) – hali ambayo inawaweka hatarini kuvunjika miguu ovyo.

Kwa mujibu wa watafiti hao, wingi wa mafuta mwilini unasababisha madini muhimu inayofanya mifupa kuwa migumu kupungua.Wanasema kuwa ugonjwa wa osteoporosis umeshika kasi zaidi miongoni mwa wanaume wanene kuliko wanawake.

Katika ripoti yao iliyochapishwa katika jarida la Journal of Clinical Endocrinology and Metabolism, watafiti hao wanashauri madaktari kuwapima watu wanene kubaini ikiwa wana ugonjwa huo ili wapate matibabu ya haraka.

“Tofauti na itikadi ambayo imekuwepo kwamba watu wanene wana mifupa migumu, ukweli ni kwamba mifupa yao ni dhaifu,” inasema ripoti hiyo.

Wataalamu hao walifanyia uchunguzi mifupa ya watu wanene 10,814 nchini Amerika na kubaini kuwa idadi kubwa hawakuwa na madini yanayofanya mifupa kuwa migumu.

Aidha, watafiti waligundua kuwa wanaume wembamba wana mifupa migumu ikilinganishwa na wanene.

Wataalamu wanashauri kuwa maziwa, mtindi, mboga, samaki, nafaka na vyakula vingine vilivyo na vitamini D vinasaidia kufanya mifupa kuwa migumu.

Ili kukwepa unene kupindukia, wanashauri wanaume kufanya mazoezi, kuepuka kuvuta sigara na ubugiaji wa pombe.

Aidha kuepuka michezo na shughuli zinazofanya mtu kuanguka kwa urahisi ni njia mojawapo ya kupunguza uwezekano wa kuvunjika kwa mifupa kwa waathiriwa.

  • Tags

You can share this post!

Utaratibu usio na maumivu makali wa kuondoa uvimbe wa...

CHARLES WASONGA: Juhudi ziwekwe kupunguza uagizaji chakula...

T L