• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
CHARLES WASONGA: Juhudi ziwekwe kupunguza uagizaji chakula kutoka nje

CHARLES WASONGA: Juhudi ziwekwe kupunguza uagizaji chakula kutoka nje

Na CHARLES WASONGA

SERIKALI inafaa kupiga jeki uzalishaji wa nafaka, kama vile ngano, ambayo huagizwa kwa wingi kutoka nje ili kupunguza changamoto inayosababishwa na misukosuko katika mataifa ambako Kenya hununua zao hili.

Kwa mfano, wakati huu kuna uwezekano mkubwa kwamba bei ya bidhaa zinazotengenezwa kutokana na ngazo zitapanda kutokana na hatua ya Urusi kuvamia Ukraine wiki jana.

Hii ni kwa sababu Kenya huagiza karibu asilimia 75 ya hitaji lake la tani 1.2 milioni ya ngano kila mwaka kutoka mataifa hayo.

Nchi ya Urusi ndio inaongoza katika uuzaji nje wa ngano ulimwenguni ilhali Ukraine inashikilia nafasi ya nne katika biashara hiyo.

Vita vilivyochacha kati ya mataifa hayo mawili, bila shaka vitaathiri shughuli za usafirishaji wa nafaka hiyo kuelekea mataifa ya kigeni. Hii ina maana kuwa mataifa hayo, Kenya ikiwemo, ambayo hutegemea ngano kutoka Urusi na Ukraine, yatakumbwa na uhaba mkubwa wa bidhaa hiyo.

Uhaba huo bila shaka utachochea kupanda kwa bei ya unga wa ngano na bidhaa nyingine ambazo hutengenezwa kutokana na unga wa zao hilo.

Ni majuzi tu ambapo bei ya mkate ilipanda kwa Sh5, kutoka Sh50 hadi Sh55 kwa mkate wa uzani wa gramu 400. Kwa hivyo, huenda bei ya bidhaa hii ambayo hutegemewa na Wakenya wengi wa mapato ya chini, ikapanda zaidi ikiwa Urusi haitakomesha mashambulio dhidi ya Ukraine.

Kando na ngano, Kenya pia huagiza bidhaa zingine kama mbolea na mafuta ya kupikia kutoka Urusi; ambayo bei zao pia zinatarajiwa kupanda kutokana na mzozo kati ya nchi hiyo na Ukraine.

Isitoshe, vita kati ya mataifa hayo mawili vitaathiri soko ya majani chai kutoka Kenya ikizingatiwa kuwa Urusi ni mojawapo ya mataifa ambayo hununua zao hili kwa wingi kutoka Kenya.

Kulingana na takwimu kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu Nchini (KNBS), Urusi ilinunua majani chai ya thamani ya Sh6.2 bilioni kuanzia Januari hadi Novemba mwaka jana, 2021.

Gharama ya maisha, nchini Kenya inatarajiwa kupanda kwa sababu vita hivyo, tayari vimechangia kupanda kwa mafuta ghafi yanayozalishwa kwa wingi nchini Urusi.

Inatarajiwa kuwa bei ya bidhaa hiyo itapanda hadi kufikia dola 150 (Sh16,000) kwa pipa kutoka bei ya sasa ya dola 94.20 (Sh9,500) kwa pipa endapo Amerika na mataifa washirika wake yataiwekea Urusi vikwazo.

Kwa hivyo, ili kuondoa hali ya sasa ambapo Kenya huagiza vyakula kutoka ng’ambo, serikali inafaa kutekeleza mipango maalum ya kukabiliana na changamoto zinazowazonga wakulima wa mazao ya chakula ili kuwezesha taifa hili kujitosheleza kwa chakula.

Sioni ni kwa nini Kenya iendelee kuagiza ngano kutoka Urusi, Ukraine, Misri na mataifa mengine ya badala ya kukumbatia sera zitakazowawezesha wakulima wa zao hilo kuimarisha uzalishaji.

Ngano hukuzwa kwa wingi katika kaunti za Narok, Uasin Gishu, Nakuru na Laikipia. Wakulima katika kaunti hizi wasaidiwe ili waweze kukumbatia kilimo cha kisiasa cha zao hili kwani hii ndio njia ya kipekee itakayowawezesha kuongeza uzalishaji.

Kilimo cha zao hili, na mazao mengine ya chakula, pia yaimarishwe kupitia ustawishaji wa kilimo cha unyunyiziaji.

Kenya ikomeshe kabisa huu mwenendo wa kutegemea vyakula vinavyoagizwa kutoka nje, ili isije ikakabiliwa na hatari kama ya sasa kufuatia mzozo kati ya Urusi na Ukraine.

  • Tags

You can share this post!

Walio wanene kupindukia kwenye hatari ya kuvunjika miguu...

Uchumi: Ahadi za Raila zakosa msingi

T L