• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
WALIOBOBEA: Beth Mugo: Aliacha alama katika sekta za Elimu, Afya

WALIOBOBEA: Beth Mugo: Aliacha alama katika sekta za Elimu, Afya

KWA HISANI YA KYB

KABLA ya kujiunga na siasa ambako aliacha alama isiyoweza kufutika katika haki za binadamu na katika sekta za elimu na afya, Beth Mugo alikuwa amefaulu katika biashara, haki ya jamii, uwezeshaji wa wanawake na habari.

Alihudumu kama mwalimu mkuu katika shule ya msingi ya Kiganjo kuanzia 1958 hadi 1959, kabla ya kujiunga na Runinga ya Sauti ya Kenya, sasa Shirika la Utangazaji la Kenya, ambako alishikilia nyadhifa tofauti kati ya 1964 na 1970.

Mnamo 1972, kwa ushirikiano na wengine, Mugo na mumewe Nicholas Muratha Mugo, walianzisha Beth Ltd, kampuni inayohusika na vito na bidhaa za kumbukumbu za Kiafrika.

Biashara hiyo ingali inaendelea.

Amehudumu kama mkurugenzi wa Hobby Hotels na majukumu mengine katika sekta ya kibinafsi wakati ambao nafasi nyingi za uongozi zilikuwa zimeshikiliwa na wanaume.

Pengine ni vigezo hivi vilivyomfanya ateuliwe waziri katika serikali ya Rais Mwai Kibaki.

Alikuwa kiongozi wa pili baada ya Profesa Anyang Nyong’o, kutangaza hadharani alikuwa na saratani akiwa waziri wa Afya ya Umma na Usafi ambapo alihusika pakubwa kupitishwa kwa sheria ya kuthibiti uvutaji wa sigara.

Mugo ni kifungua mimba katika familia ya watoto 12 wa James Muigai Ngengi na Minneh Ngina Muigai wanaotoka kijiji cha Ichaweri, Gatundu, kaunti ya Kiambu.

Aliishi na wazazi na ndugu zake katika familia kubwa iliyojumuisha rais wa kwanza wa Kenya, Mzee Kenyatta.

Mugo alisomea shule za msingi za Kahugu-ini na Ng’enda eneobunge la Gatundu kabla ya kwenda Mambere, Kikuyu, kaunti ya Kiambu.

Alijiunga na chuo cha mafunzo ya walimu cha Kambui Teachers College mwaka wa 1956 alipopata cheti cha Taifa cha Ualimu mwaka wa 1957.

Baada ya kuolewa 1959, Mugo alienda Amerika kwa masomo zaidi katika mpango wa elimu uliofanikishwa na Tom Mboya na Julius Gikonyo Kiano.

Aligombea kiti cha ubunge kwa mara ya kwanza 1992 kwa tiketi ya chama cha Democratic Party (DP) kilichoongozwa na Kibaki.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 1997 aligombea kwa tiketi ya chama cha Social Democratic Party (SDP) ambacho mgombea urais wake alikuwa Charity Ngilu na kushinda kiti cha ubunge cha Dagoretti kwa kura nyingi.

Mwaka wa 2002 alikuwa mwanachama wa National Alliance of Kenya (NAK) ambao uliungana na LDP kubuni Muungano wa National Rainbow Coalition (NARC).

Mugo alishinda tena na kuteuliwa waziri msaidizi wa Utalii na Wanyamapori.

Baadaye alihamishiwa wizara ya Elimu kama waziri msaidizi wa Elimu ya Msingi.

Alitetea kiti chake kwenye uchaguzi mkuu wa 2007 kwa tiketi ya chama cha Party of National Unity (PNU) na kushinda.

Wakati serikali ya muafaka wa kitaifa ilipoundwa baada ya upatanishi ghasia zilizokubwa nchi kufuatia matokeo ya kura ya urais kupingwa, Mugo aliteuliwa waziri wa Afya ya Umma ambapo alianzisha na kutekeleza mipango ya kuboresha afya ya umma ya Wakenya ikiwemo vita dhidi ya Ukimwi, Malaria, kukabiliana na vifo wakati wa uzazi na ujenzi wa vituo vya afya.

You can share this post!

JUNGU KUU: Hatua ya Mudavadi inaweza kumponza

KIGODA CHA PWANI: PAA yayumba kuhusu itakayeunga kwa urais

T L