• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:50 AM
WALIOBOBEA: Mudavadi ‘alilelewa’ na Moi ‘akafufuliwa’ na Raila

WALIOBOBEA: Mudavadi ‘alilelewa’ na Moi ‘akafufuliwa’ na Raila

KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK

WYCLIFFE Musalia Mudavadi alikuwa sehemu ya serikali ya kwanza ya muungano nchini Kenya, ambayo ilizinduliwa Aprili 2008 na kuongozwa na Rais Mwai Kibaki.

Aliteuliwa naibu waziri mkuu na waziri wa Serikali za Mikoa na kumfanya kiongozi wa upinzani aliyekuwa na nguvu zaidi bungeni na afisa wa pili aliyekuwa na cheo kikubwa baada ya kiongozi wa chama chake wakati huo Waziri Mkuu Raila Odinga.

Kwa mara ya pili ndani ya miaka 10, Mudavadi alijipata katika wadhifa mkubwa serikalini ambao hakuwa amechaguliwa kushikilia.

Mwaka wa 2002, mtangulizi wa Kibaki, Rais Daniel arap Moi alishangaza kwa kumteua kuwa makamu wa rais.

Na miaka iliyotangulia, akiwa na umri wa miaka 29, Mudavadi alikuwa amechaguliwa kuchukua nafasi ya baba yake kama mbunge wa Sabatia kabla ya kuteuliwa katika Baraza la Mawaziri.

Alipoteuliwa naibu waziri mkuu, mtazamo wa wengi ulikuwa kwamba alikuwa mtu wa bahati, ambaye hakuhitaji kushughulika kuingia uongozini kwa kuwa bahati ilionekana kumwendea alikokuwa.

Kuteuliwa kwa Mudavadi kulitokana na mkataba wa kugawana mamlaka uliobuni serikali ya muungano kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007.

Kabla ya uchaguzi mkuu wa 2007, taharuki ilikuwa imetanda kati ya vyama tofauti vya kisiasa.

Kufikia 2002, Wakenya walikuwa wakihitaji mabadiliko walipokinai utawala wa Moi chini ya chama cha Kenya African National Union (KANU).

Ili kuondoa Moi mamlakani, vyama vya upinzani viliungana kuunda muungano wa National Rainbow Coalition (NARC) na kumteua Kibaki kuwa mgombea urais wake.

Wimbi la kumpinga Moi lilikuwa na nguvu kiasi kwamba hata washirika wake wa karibu waliwazia kujitenga naye. Mudavadi alikuwa mmoja wa washirika hao ambaye alihamia upinzani, lakini kwa muda mfupi tu, kwani alirudi katika KANU.

Siku chache kabla ya uchaguzi mkuu, Moi alimteua Bw Mudavadi kuwa makamu rais wa saba wa Kenya. Moi alipomchagua Uhuru Kenyatta kuwa mrithi wake na kuacha nje wanasiasa waliokuwa na tajiriba pana zaidi, vibaraka kadhaa wa KANU walilalamika kwa kukihama chama hicho.

Moi alihakikisha Mudavadi alikuwa ‘mgombea mwenza’ wa Kenyatta kwenye uchaguzi mkuu wa 2002. Lakini walishindwa Mudavadi akiwa makamu rais kwa siku 90 tu. Aidha, alipoteza kiti cha ubunge cha Sabatia kwa Moses Akaranga aliyegombea kwa mara ya kwanza.

Muungano wa Narc uliposambaratika kufuatia kura ya maamuzi ya katiba ya 2005, Mudavadi alijiunga na Bw Odinga katika juhudi za kurejea katika siasa.

Odinga alikuwa ameunda ODM baada ya kuongoza upande uliopinga rasimu ya katiba.Huo ndio uliokuwa mwanzo wa ushirikiano wa kisiasa wa Odinga na Mudavadi.

Kwenye uchaguzi mkuu wa 2007, Mudavadi alikuwa ‘mgombea mwenza’ wa Bw Odinga na ghasia zilipozuka, alikuwa mmoja wa viongozi wanne wa ODM walioketi na wenzao wa chama cha PNU cha Kibaki kwa mazungumzo ya upatanisho. Mudavadi ni mmoja wa wabunge wa Sabatia waliohudumu kwa muda mrefu kutoka 1989 hadi 2002 na kutoka 2008 hadi 2013.

Mwaka wa 1993 aliteuliwa Waziri wa Fedha kuchukua nafasi ya Prof George Saitoti, ambako alikumbana na kashfa ya Goldenberg iliyopotezea serikali Sh80 bilioni kupitia ulaghai wa kuuza nje dhahabu feki.

Ingawa ilikuwa imeanza kabla ya Mudavadi kujiunga na wizara ya Fedha, Mudavadi alijipata akilaumiwa kwa kuhusika hadi akaondolewa lawama na tume ya uchunguzi iliyoongozwa na Jaji Samuel Bosire.

Mudavadi alizaliwa Septemba 21, 1960, Sabatia, wilaya ya Vihiga ( sasa Kaunti ya Vihiga). Kati ya 1980 na 1984, alisomea masuala ya Uchumi wa Ardhi katika Chuo Kikuu cha Nairobi ambapo alichezea timu ya raga ya chuo hicho, Mean Machine.

Baadaye alifanya kazi katika National Housing Corporation (NHC) kutoka 1984 hadi 1985 na kujiunga na sekta ya kibinafsi kabla ya kujitosa katika siasa mwaka wa 1989.

Aligombea urais katika uchaguzi mkuu wa 2013 kwa tikiti ya chama cha United Democratic Party na kuibuka wa tatu. Kwa wakati huu ndiye kiongozi wa chama cha Amani National Congress (ANC), alichounda 2015.

  • Tags

You can share this post!

Thibitisho uagizaji wa maziwa kutoka Uganda haujapigwa...

KIGODA CHA PWANI: Madai ya ‘mradi wa Joho’ yamtia doa...

T L