• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
WALIOBOBEA: Musikari aliiga Kibaki, akakabili ufisadi vikali

WALIOBOBEA: Musikari aliiga Kibaki, akakabili ufisadi vikali

KWA HISANI YA KENYA YEAR BOOK

MUSIKARI Nazi Kombo alikuwa mwanafunzi wa kidato cha sita mwaka wa 1966 wakati darasa lake lilimwalika waziri mpya wa Biashara na Viwanda, Mwai Kibaki, kutoa hotuba katika shule yao.

Mada ilihusu ukuaji wa uchumi wa Kenya katika Ruwaza Nambari 10 ya mwaka wa 1965.

Akitoa hotuba yake, Kibaki alikuwa na ufasaha mkubwa, akitaja takwimu bila kusoma popote.

Aliwaacha waliomsikiliza wakivutiwa na umilisi wake wa mada hiyo na alivyoiwasilisha.

Tangu siku hiyo, Kombo alikata kauli kumuiga Kibaki kwa kusomea uchumi katika chuo kikuu au kuteuliwa waziri siku moja katika maisha yake.

Ndoto ya Kombo akiwa shule ya upili ilitimia miaka 37 baadaye, mnamo Novemba 2004, wakati Rais Kibaki alipomteua waziri.

Mwanzoni alimteua kama Waziri wa Ustawi wa Mikoa na baadaye Serikali za Wilaya.

Kombo alijiunga na Baraza la Mawaziri akiapa kuangamiza ufisadi, msimamo ambao ulilandana vizuri na ajenda ya Kibaki.

Alichaguliwa mbunge kwa tikiti ya chama cha FORD-Kenya katika uchaguzi mkuu wa1992 na akajijenga kama mmoja wa waliopiga vita ufisadi.

Kombo atatambuliwa kwa kupigania kupitishwa kwa Sheria ya Vyama vya Kisiasa ya 2011 ambayo ilitoa mfumo wa usajili, usimamizi na ufadhili wa vyama vya kisiasa.

Aidha, anasifiwa kwa mchango wake wa kutunga sera kuhusu vita dhidi ya ufisadi kwingine katika Afrika na nchi za Caribbean alipokuwa katika bodi ya mataifa ya Afrika, Caribbean, Pacific na Muungano wa Ulaya (ACP-EU).

Wakati wa mahojiano kuhusu kitabu chake, Kombo alifichua kigezo kingine cha ajenda ya maendeleo ya Kibaki, ambacho hakikuweza kutekelezwa.

Kulingana na waziri huyo wa zamani, Kibaki hakuunga kubuniwa kwa kaunti 47 chini ya ugatuzi kwa kutegemea mipaka ya jamii na kisiasa.

Badala yake, Kibaki alitaka majimbo 10 au 15 kwa msingi wa kiuchumi na uwiano wa kitaifa.

Kombo alikumbuka Kibaki akionya Baraza la Mawaziri katika mkutano kwamba ingekuwa hatari kugawa nchi kwa maeneo madogo ambayo hayangejisimamia kiuchumi ili kutimiza maslahi ya wanasiasa.

Kwa mfano, alishangaa kwa nini Murang’a, Nyeri, Kirinyaga, Embu, Meru na Tharaka Nithi yanafaa kutenganishwa ilhali yanategemea shughuli sawa za uchumi na yanaweza kuwa eneo moja la kiuchumi.

Kibaki aliamini kuwa maeneo machache ya kiuchumi yangekuwa na manufaa kuliko maeneo mengi madogo.

Kombo na Kibaki walikuwa na uhusiano mwema wa kisiasa uliowaunganisha katika nyakati ngumu.

Chama cha FORD-Kenya ambacho kiliongozwa na Kijana Wamalwa kilikuwa kimeunda muungano na chama cha Kibaki cha Democratic Party kuelekea uchaguzi mkuu wa 2002.

Baada ya NARC kushinda uchaguzi wa mwaka huo, Wamalwa aliteuliwa Makamu wa Rais lakini akafariki miezi minane baada ya kuingia ofisini.

Kombo alichukua nafasi yake kama kiongozi wa Ford Kenya kisha mvutano ukaanza katika serikali ya NARC.

FORD-Kenya ilijiunga na DP, hatua iliyofanya Kombo kupoteza kiti chake cha eneobunge la Webuye kwenye uchaguzi mkuu wa 2007. Mnamo 2008 aliteuliwa mbunge.

Kombo alihusisha kushindwa kwake katika uchaguzi mkuu wa 2007 na “laana” ya siasa za Magharibi mwa Kenya ambazo ni za viongozi kuumbuana na kutengana kiasi kwamba haliwezi kuungana na kuwa na msimamo mmoja kwenye uchaguzi mkuu.

  • Tags

You can share this post!

Uhuru awaaga marais kabla astaafu Agosti

Ndege ya kwanza yapeleka miraa baada ya mkataba wa marais

T L