• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
WALIOBOBEA: Pandashuka, mafanikio ya Kenyatta katika siasa

WALIOBOBEA: Pandashuka, mafanikio ya Kenyatta katika siasa

Licha ya kupigiwa upatu ikidhaniwa angerithi himaya ya siasa ya baba yake na akiwa ametoka familia yenye jina kubwa na uwezo mkubwa wa kifedha, Uhuru alishindwa uchaguzini na Moses Mwihia aliyegombea kwa tikiti ya chama cha Social Democratic Party (SDP) kilichohusishwa na Anyang Nyong’o na Charity Ngilu.

Hii ilikuwa hata baada ya Moi kugawa Gatundu kuwa Gatundu Kaskazini na Gatundu Kusini hatua iliyochukuliwa ya kumrahisishia Uhuru ashinde kwa urais.

Baada ya kushindwa, Uhuru alijiondoa tena katika maisha ya umma hadi mwaka wa 1999 wakati ambao, Moi, aliyejitangaza kuwa profesa wa siasa, alipomteua Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii ya Kenya. Wakati huo, Uhuru alikuwa na umri wa miaka 38.

Ilivyotarajiwa, kulikuwa na minung’uniko miongoni mwa upinzani kwamba hakustahili kuteuliwa kwa wadhifa huo; kwamba hakuwa na ujuzi wa kusimamia shirika muhimu na la kimkakati kama hilo.

Hata hivyo, waliofahamu karata ya siasa ya Moi waliona kwamba alikuwa akilenga jambo kubwa; kwamba profesa huyo wa siasa alikuwa akimuandaa Uhuru kugombea kiti kikubwa cha kisiasa.

Mwaka wa 2001, Mark Too ‘alijiuzulu’ kama mbunge wa kuteuliwa, na nafasi yake ikachukuliwa na Uhuru ambaye mara moja aliteuliwa waziri wa serikali za wilaya na Rais Moi. Ikisimamia Baraza la Jiji la Nairobi na manispaa zote, wizara hiyo ilikuwa yenye nguvu zilizokuwa na mizizi kote nchini. Mwaka uliofuata Moi ambaye alikuwa akistaafu alimtangaza Uhuru kama aliyechagua kuwa mrithi wake na mgombea urais wa chama cha KANU kwenye uchaguzi mkuu wa 2002.

Uamuzi huo uligawanya chama cha KANU na kumfanya Uhuru kushindana na ‘baba’ yake, Kibaki — mgombeaji wa upinzani ambaye alikuwa amempa jina na ambaye watoto wake walikuwa marafiki na wale wa Kenyatta. Uhuru alishindwa na Kibaki lakini akawa mbunge wa Gatundu Kusini.

Hata hivyo, uchaguzi mkuu wa 2007 ulipokaribia, alitangaza kuwa hangegombea na akaamua kumuunga Kibaki aliyekuwa akisaka muhula wa pili kwa tikiti ya chama cha Party of National Unity dhidi ya Raila Odinga aliyegombea kwa tikiti ya chama cha Orange Democratic Movement.

Serikali ya muafaka wa kitaifa ilipoundwa baada ya ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2008, Uhuru aliteuliwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Biashara. Mnamo Januari 2009, aliteuliwa waziri wa fedha kuchukua nafasi ya Amos Kimunya.

Mnamo Desemba 2010, alitajwa na Mahakama ya Kimataifa kuhusu Uhalifu (ICC) kama mmoja wa Wakenya sita waliohusika na ghasia za baada ya uchaguzi wa 2008 akiwa na aliyekuwa waziri wa viwanda Henry Kosgey, William Ruto ambaye wakati huo alikuwa amesimamishwa kama waziri wa Elimu ya Juu, aliyekuwa Mkuu wa Utumishi wa Umma Francis Kirimi Muthaura, aliyekuwa kamishna wa polisi Mohammed Hussein Ali na mtangazaji wa redio Joshua Arap Sang.

Uhuru alijiuzulu kama waziri wa fedha lakini akaendelea kuwa Naibu Waziri Mkuu. Japo kuandamwa na kesi hiyo kulionekana kuathiri maisha yake ya kisiasa, haikuonekana kumtia hofu na kabla ya uchaguzi mkuu wa 2013 aliungana na Ruto kuunda muungano wa Jubilee wa vyama vya The National Alliance (TNA) na United Republican Party na wakashinda Bw Odinga.

Uhuru aliapishwa kuwa Rais wa nnne wa Jamhuri ya Kenya akawa ameiva kisiasa na akaongoza kwa miaka kumi hadi 2022 alipostaafu.

  • Tags

You can share this post!

Wanaraga wa Kabras Sugar wavunja rekodi ya KCB kutoshindwa...

JUNGU KUU: CASs: Ruto aiga Uhuru kuwatunuku wandani

T L