• Nairobi
  • Last Updated October 2nd, 2023 8:00 AM
Waliovamia shamba la familia ya Uhuru Kenyatta kukamatwa

Waliovamia shamba la familia ya Uhuru Kenyatta kukamatwa

NA SAMMY WAWERU

MSAKO wa wahuni waliovamia shamba la familia ya Rais mstaafu Uhuru Kenyatta Machi 2023, unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Akihutubia taifa kuhusu hali ya usalama nchini, Waziri wa Usalama wa Ndani Prof Kithure Kindiki alisema Jumatano, Mei 31, 2023 kwamba uvamizi wa shamba la rais huyo mstaafu ni hatia inayohitaji adhabu kali.

“Uvamizi huo ni kosa kubwa sana, na serikali haichukulii suala hilo kimzaha,” Waziri Kindiki alisema akihutubia wanahabari Harambee House, Nairobi.

Shamba la familia ya Bw Kenyatta, Northlands City, lililoko eneo la Ruiru, Kaunti ya Kiambu lilivamiwa wakati wa maandamano ya Azimio.

Ranchi hiyo ina mifugo na miti na kondoo zaidi ya 1, 000 waliibwa, kinara wa Azimio Raila Odinga akikashifu vikali tukio hilo.

Wavamizi pia walichoma shamba hilo.

Bw Odinga ambaye pia ni kiongozi wa ODM, alihusisha Naibu wa Rais Rigathi Gachagua na mbunge wa Kikuyu Kimani Ichungwa na uvamizi huo akisema wao ndio waliufadhili.

Baadhi ya miti iliyokatwa Northlands City ilitumika kuunda makazi ya muda. PICHA / SAMMY WAWERU

Kulingana na Prof Kindiki, uchunguzi ulianzishwa na wahusika wamekawia kukamatwa kwa sababu ya siasa kusakatwa katika mjadala huo.

“Hivi karibuni walioshiriki tutaanza kuwatia nguvuni, wafunguliwe mashtaka,” Waziri alitangaza.

Baadhi ya wanasiasa wa Kenya Kwanza, wamekuwa wakilaumu Bw Kenyatta wakidai ndiye alikuwa mfadhili wa maandamano ya Azimio ambayo yalisitishwa kurusu mazungumzo kuangazia malalamishi ya upinzani.

Mei 22, 2023 wakati wa Kongamano la Kitaifa la Wajumbe wa Jubilee, Kenyatta ambaye ni kiongozi wa chama hicho alivunja kimya chake kwa mara ya kwanza baada ya shamba la familia yake kuvamiwa.

Rais huyo mstaafu alieleza kushangazwa na wapinzani wake kuendelea kumchokoza, akisema; “Mimi niliwapokeza serikali kwa amani na mchana peupe ilhali wanaendelea kunichokoza.”

Alisema nia yake ni kuona taifa amani ikishamiri, ndiposa hakuona haja ya kuonyesha makali yake.

  • Tags

You can share this post!

Madampo kila kona yaharibu sura ya Nairobi

Serikali yakubali tope la Shakahola

T L