• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Wanawake wahalifu walivyomgeuza kiwete

Wanawake wahalifu walivyomgeuza kiwete

NA MWANGI MUIRURI

MNAMO Aprili 12, 2023 Bw George Muigai, 31, alikumbana na genge la wanawake wanne waliokuwa wamejihami kwa mapanga na visu katika mtaa wa Kiandutu ambapo alichapwa huku akiporwa hadi akawa mlemavu.

Muigai anakiri kwamba wanawake pia wamekuwa hatari katika visa vya ujambazi mitaani na wanashambulia na kuibia waathiriwa kwa mabavu sawa na wanaume.

“Nilikuwa nimemaliza kujivinjari katika klabu kimoja mjini Thika na nikaanza safari yangu kuelekea kwa nyumba yangu ya upangaji katika mtaa wa Kiandutu,” asema.

Anasema kwamba alielewa kwamba safari yake ya kilomita moja na nusu hadi kwa nyumba ingekuwa na changamoto zake lakini hakutazamia ziwe za kiwango cha kumweka hospitalini kwa miezi mitano, na hadi sasa akiwa bado akitumia mikongojo kutembea.

“Nilikuwa nimetoka kazi ya mjengo ambapo nilikuwa nimelipwa Sh800. Nikaamua kutembea katika baa moja ili kujivinjari kidogo huku nikiwa na mpango wa kuweka akiba ya Sh300. Hizo Sh300 nilizificha katika mfuko wa siri ulioshonwa katika suruali yangu ya ndani na ndipo nikaanza mwendo wa nyumbani,” asema.

Bw Muigai anasema kwamba alikuwa amefika mwanzoni mwa mtaa wa Kiandutu kupitia uwanja wa soko la Mbuzi na ndipo akaona wanawake wanne wakiwa wamesimama eneo lililokuwa na mwangaza mchache.

“Mimi nilifikiria ni wanawake tu waliokuwa wakisakata udaku wao wa kawaida na hata bila kuchukua tahadhari, nilipania kuwapita tu bila wasiwasi wowote,” anasema.

Lakini anasema kuwa alipowafikia, aliona wawili wamechomoa mapanga kutoka kwa nguo zao huku mwingine akiwa na kisu.

“Wa nne ambaye hakuwa amejihami ndiye alinisongea na akanitaka nimpe simu na pesa. Niliwaambia sikuwa na simu lakini nilikuwa na Sh30 kwenye mfuko,” aelezea.

Bw George Muigai akisimulia alivyokumbana na wanawake wahalifu waliomgeuza kiwete. PICHA|MWANGI MUIRURI

Bw Muigai anasema alishtukia amepigwa usoni kwa tumbo la upanga na akaona vimulimuli.

“Nilimsikia mmoja akitoa amri nikatwe kidogo kichwani ili nikiona damu inatoka nielezee nilikoficha pesa. Uafrika na utamaduni wa mababu ulinikaba na nikajiuliza itakuwa vipi mimi mwanamume ninapigwa na wanawake na ndipo niliamua kupigana,” asema.

Bw Muigai anasema kwamba alikuwa amejiweka chonjo kuanza vita lakini upanga ukamteremkia hadi kwa kichwa na alipojaribu kujikinga, akakatwa mkononi.

Bw Muigai anasema kwamba alianguka chini na akajipata anaangushiwa mateke mazito kila mahali na wanawake hao “na ndipo nilielewa maana ya msemo kwamba kile mwanamume anaweza akakifanya mwanamke anaweza akakifanya hata kwa ueledi zaidi”.

Muigai akiwa hoi chini, anasema hakupewa nafasi ya kurusha mateke wala ngumi kwa kuwa kila alipojaribu kuamka au kurusha, alikuwa akirejeshwa chini kwa kukatwa kwa upanga.

“Mimi nilivumilia aibu nisiuliwe na nikashuhudia kwa fahamu za umbali nikielekea kuzimia nikivuliwa nguo na ndipo nikajua hata ujanja wangu wa kuficha pesa ndani ya suruali ya ndani ulikuwa umefichuka…Hata walinivurta sehemu zangu za nyeti na kuzifanyia ucheshi, sikujiulizia kwa kuwa nilikuwa nikizidi kupoteza fahamu sababu ya kuvuja damu kwa wingi,” asema.

Bw Muigai anasema hajui jinsi alivyojipata katika hospitali ya Umma ya Thika “lakini nilipopata fahamu madaktari walinipongeza kwa kuwa na ujasiri wa kubakia hai kwa kuwa nilipowasilishwa kwao nilikuwa nimebakisha dakika chache tu niage dunia”.

Anasimulia kwamba alikaa katika hospitali hiyo kwa miezi mitano na baada ya kuachiliwa akielekea nyumbani akiwa ameabiri bodaboda mwendo wa saa 12 jioni, akahusika katika ajali ambapo gari lilimgonga pamoja na dereva wake na kuwaangusha kwa kishindo juu ya lami.

“Mimi tena ndiye huyo nilivunjika mguu wangu wa kulia, mkono wa kulia na nikarejeshwa hospitalini tena. Nililazwa tena kwa miezi miwili na kwa muda huo nilijiuliza maswali tele kuhusu maisha yangu na mikosi,” asema.

Anasema alikumbuka jinsi miaka 13 iliyopita alipata alama ya C+ katika mtihani wake wa Kidato cha Nne (KCSE) na amekuwa na ari ya kujiunga na taasisi ya kiufundi ili kujipa kozi ya kuunda mitambo ya stima.

“Lakini hali haijakuwa shwari kwangu kwa kuwa mamangu mzazi amekuwa akiugua mara kwa mara tangu babangu aliyekuwa akihudumu kama mwanabodaboda mjini Thika alipoaga dunia miaka 12 iliyopita baada ya kuhusika katika ajali na nimekuwa nikimsadia kulea watoto wetu wengine wanne,” asema.

Anasema kwamba alizokuwa ameficha kwenye chupi, alipania ziwe akiba kukata kiu cha masomo.

“Nikilipwa Sh800, nilikuwa namtumia mamangu Sh300, najivinjari na Sh200 na kujiwekea akiba ya Sh300 za kujifadhili kozi yangu. Lakini mpango huo wote umesambaratishwa na genge moja la wanawake mjini Thika na Kiandutu. Itabidi tu nipone ili nirejelee mpango wangu,” Muigai alia.

Sasa anamtaka mjumbe mwakilishi mwanamke wa Murang’a Bi Betty Maina amtembelee kama mwaathiriwa wa dhuluma za kijinsia na amsaidie kuafikia ndoto yake ya kujihami na kozi ili pate kazi ya maana.

mwangilink@gmailcom

  • Tags

You can share this post!

Besigye amshambulia Rais Museveni kwa kukwamilia uongozini

Wahuni wanaohangaisha walevi kwa pingu 

T L