• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Waziri Kindiki: Tutafanya maombi Shakahola kuondoa laana

Waziri Kindiki: Tutafanya maombi Shakahola kuondoa laana

NA SAMMY WAWERU

WAZIRI wa Usalama wa Ndani, Kithure Kindiki ametangaza kwamba serikali itaandaa maombi katika Msitu wa Shakahola, Malindi ili kuondolea taifa laana.

Akitaja maafa ya eneo hilo kama mojawapo ya matukio makuu nchini kuwahi kufanyika, Prof Kindiki alisema Jumapili, Juni 11, 2023 kuwa Shakahola inapaswa kutakaswa kwa njia ya sala.

Alisema maombi hayo yatasaidia kusafisha nchi na kuiondolea laana, kufuatia damu nyingi iliyomwagika.

Waziri alisema hafla hiyo itafanyika baada ya oparesheni ya ufukuzi maiti kukamilika.

“Tutafanya maombi ya makubwa (akimaanisha maombi ya kitaifa) kutakasa Shakahola. Yaliyofanyika humo ni laana na tunapaswa kuokoa nchi yetu,” aliahidi Prof Kindiki akizungumza katika ibada ya misa Methodist Church of Kenya, Marimanti, Tharaka Nithi.

Mchungaji tata Paul Mackenzie anahusishwa na maafa ya halaiki Shakahola, kupitia mafunzo potovu ya dini.

Miili zaidi ya 270 ya wafuasi wa kiongozi huyo wa Good News International Church, Kaunti ya Kilifi imefukuliwa.

“Shughuli ya kufukua maiti inaendelea, na kuna makaburi mengi tunayolenga. Kufikia sasa, tumefukua maiti 274,” Waziri Kindiki alisema.

Mnamo Juni 5, 2023, vikosi vya pamoja vya usalama, maafisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu na wadauhusika, walianza awamu ya tatu ya ufukuaji maiti.

Mackenzie anaendelea kuzuiliwa na polisi huku uchunguzi ukiendelea.

Pasta huyo anadaiwa kuhadaa wafuasi wake kufunga, bila kula wala kunywa, akiwaahidi kwamba hatua hiyo itawawezesha kukutana na Yesu.

“Iwezekanaje anayedanganganya wengine anaendelea kula na kunywa akidai yeye ni Mkristu? Mackenzie ni mhalifu na idadi ya watu alioua imepita ya mashambulizi ya kigaidi yaliyowahi kufanyika Kenya,” Bw Kindiki akakashifu mhubiri huyo.

Waziri aidha ameapa kuhakikisha kuwa Mackenzie anaozea jela.

Akivunja kimya chake kwa mara ya kwanza kuhusu suala la Shakahola, Juni 2023 Rais William Ruto alimtaja Mackenzie kama mhalifu sugu anayepaswa kuwa jela.

Mkasa wa Shakahola aidha umeonekana kuiamsha serikali, ikizindua jopokazi kupiga msasa makanisa, misikiti na maeneo ya kuabudu.

Prof Kindiki alisema serikali haitalegeza kamba kuainisha masuala ya dini nchini, ikiwemo kuweka sheria kali kudhibiti makanisa na misikiti.

  • Tags

You can share this post!

Ruto anavyomdhibiti Gachagua

Gachagua awaomba Wakenya kuvumilia ugumu wa maisha serikali...

T L