• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 9:55 AM
Yuko wapi mume wangu, Babu Owino? Fridah Ongili ataka majibu  

Yuko wapi mume wangu, Babu Owino? Fridah Ongili ataka majibu  

NA SAMMY WAWERU

MKE wa Mbunge wa Embakasi Mashariki, Pauli Ongili Owino maarufu kama Babu Owino, Bi Fridah Ongili amelalamikia kuendelea kuzuiliwa kinyume cha sheria na kufichwa kwa mumewe anayehoji hahisi vyema kiafya.

Kupitia video iliyochapishwa Jumatano, Julai 19, usiku na runinga ya Citizen, Facebook, Bi Owino aliteta kunyimwa haki kujua alipo mume wake.

Kulingana na mama huyo wa watoto wawili, mara ya mwisho kuwasiliana na Bw Owino ilikuwa Jumanne usiku, baada ya kutua katika Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Jomo Kenyatta (JKIA) kutoka Mombasa, akimuarifu amekamatwa na makachero wa DCI.

“Alinieleza atanipigia simu baadaye, na kufikia sasa sijawasiliana naye kwa sababu imezimwa,” Fridah alisema.

Kuthibitisha madai ya mkewe, Taifa Leo Dijitali ilipojaribu Alhamisi, Julai 20, 2023 kufikia mbunge huyo kwa njia ya simu ya mkono ilikuwa imezimwa.

Ni hali ambayo imemshinikiza kuzuru vituo mbalimbali vya polisi Nairobi, vikiwemo JKIA, Muthaiga, Gigiri, Kilimani, Kileleshwa na Embakasi.

Alisimulia, kabla kuelekezwa anakoshuku amezuiliwa, askari walimzungusha bila kumweleza ukweli wa mambo.

“Hatimaye, nilinong’onezewa amepelekwa Kituo cha Polisi cha Wang’uru, Mwea, Kirinyaga. Ninachohitaji ni kuona mume wangu nimpe chakula na dawa, hahisi vizuri. Nataka kuona mume wangu,” alisisitiza Bi Owino, akionekana kulengwa na machozi.

Alilalamikia kuzuiwa kumuona, akiashiria uwezekano wa kupelekwa katika kituo kingine cha polisi.

Ombi la mke wa mbunge huyo; ni muungano wa Azimio, ukiongozwa na kinara wake, Bw Raila Odinga kusaidia kuachiliwa kwa Babu Owino.

Ninaelewa serikali ndiyo inamzuilia mume wangu, ninaomba Bw Raila Odinga anisaidie kuachiliwa kwake, Fridah akahimiza.

Mbunge huyo wa Embakasi Mashariki, alikamatwa kufuatia maandamano ya upinzani yanayoendelea maeneo tofauti nchini hasa ikizingatiwa kuwa amekuwa miongoni mwa viongozi wa upinzani wanaoshiriki maandamano hayo kushinikiza serikali kushusha gharama ya maisha.

Licha ya Bw Odinga kuitisha maandamano hayo, pamoja na vinara wenza hawajulikani waliko.

Maandamano hayo yameratibiwa kuwa ya siku tatu kila wiki, kuanzia Jumatano hadi Ijumaa.

  • Tags

You can share this post!

Tuokoe nchi yetu

Raia wa Pakistan akamatwa kwa kumuua mkewe aliyezaa na...

T L