• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
ZARAA: Uwezo wa njugu kupunguza gharama mafuta ya kupikia

ZARAA: Uwezo wa njugu kupunguza gharama mafuta ya kupikia

NA SAMMY WAWERU

CHINI ya kipindi cha muda wa mwaka mmoja, bei ya mafuta ya kupikia imepanda kwa kiasi kikubwa.

Lita moja inauzwa kwa karibu Sh400, kutoka Sh100, na umekuwa mzigo mzito kwa mwananchi anayeendelea kulemewa na gharama ya maisha.

Mahangaiko hayo hata hivyo yanaweza kupunguzwa, endapo wakulima na wafanyabiashara watakumbatia mifumo ya kisasa kuongeza bidhaa thamani.

Ikiwa na makao yake makuu nchini India, kampuni ya Shreeja Health Care Products imetoa mchango mkubwa kusaidia kushusha gharama ya maisha nchini humo.

Katika Maonyesho ya Kimataifa ya Agritech Africa 2022 majuzi jijini Nairobi, Afisa Mkuu Mtendaji wa kampuni hiyo Mehul Vekariya alifumbua macho wahusika katika mtandao pana wa kilimo na uuzaji bidhaa za shambani.

Maonyesho yake yaliegemea jinsi ambavyo wakulima wa aina yoyote ile ya njugu wanaweza kuziongeza thamani, na kuteka soko lenye ushindani mkuu.

Kuanzia mbegu za alizeti (sunflower), haradali (mustard), njugu karanga, ufuta (sesame), mlozi (almond), mbegu za mti wa ‘walnut’, hadi soya, kupitia mfumo wa kukama mafuta, wakulima wanaweza kuvuna pakubwa.

Baadhi ya bidhaa hizo, zinakuzwa hapa nchini wakulima wakitaabika kupata soko. Vekariya ni mvumbuzi wa mashine inayokamua mafuta, na anasema italetea Wakenya afueni.

“Kuna mashine za matumizi ya nyumbani na zile za biashara,” asema.

Anasema Shreeja Health Care Products huunda aina tano ya mashine, ile ndogo ikiwa Sh – 400 Watt inayodondoa lita 1.5 kila baada ya saa mbili, nyingine ni Sh – 800 Watt ya lita 2.5 saa tatu. Mitambo mikubwa ina saizi ya Sh – 1200 Watt, Sh – 1600 na Sh – 2000 Watt.

Kilo 2.5 za njugu zinazalisha lita moja ya mafuta ya kupikia. Kilo moja ya njugu inauzwa Sh70, hivyo basi, mbili na nusu zitakuwa Sh175.

Ukitilia maanani kwamba lita moja ya mafuta dukani sasa hizi inauzwa karibu Sh400, inadhihirika mbinu hii inaleta nafuu.

“Baada ya kukama mafuta, maganda ya njugu ni malighafi bora kutengeneza chakula cha mifugo,” Vekariya aarifu.

Afisa Mkuu Mtendaji Shreeja Health Care Products, Mehul Vekariya, akionyesha mafuta yaliyokamuliwa kutoka kwa njugu. PICHA | SAMMY WAWERU

Ni teknolojia ambayo wakulima nchini wakiikumbatia, kwa wenye mifugo utawaondolea kero ya malisho ambayo bei yake haikamatiki.

“Maganda ya njugu ambayo wengi hutupa yamesheheni Protini na Fibre, madini muhimu kwa mifugo. Isitoshe, yanaweza kutumika kutengeneza dawa kukabiliana na wadudu shambani na fatalaiza,” aelezea mtaalamu huyo.

India ni kati ya mataifa ulimwenguni yaliyoimarika kiteknolojia na mifumo kuendeleza shughuli za kilimo na ufugaji.

Sanyal Desai, Afisa Mkuu Mtendaji Radeecal Communications, shirika lililoandaa maonyesho ya Agritech Africa kwa ushirikiano na Wizara ya Kilimo na Ufugaji, anasisitiza haja ya Kenya kukumbatia kikamilifu mifumo ya kisasa kuboresha kilimo.

“Kuna mseto wa teknolojia na mifumo bora kufanikisha kilimo, ili kuangazia usalama na uhaba wa chakula ikizingatiwa kuwa athari za tabianchi ni kero ya dunia nzima,” Desai asema, akihimiza Wakenya kutumia mianya ya maonyesho kama aliyoandaa kupata suluhu ya changamoto wanazopitia.

“Ninawashauri, msitegemee maji ya mvua pekee. Mvune maji msimu wa mvua, Kenya ni nchi yenye udongo bora kuendeleza zaraa. Mazao, yaongezwe thamani kuteka masoko yenye ushindani mkuu.”

  • Tags

You can share this post!

Wagombea waanza kuvuna walichopanda kipindi cha kampeni

Ufugaji farasi kwa ajili ya donge, starehe na michezo

T L