• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 9:55 AM
Ufugaji farasi kwa ajili ya donge, starehe na michezo

Ufugaji farasi kwa ajili ya donge, starehe na michezo

NA LABAAN SHABAAN

KATIKA shamba la ekari tatu Kitisuru, Kaunti ya Nairobi, kikosi cha Akilimali kinakuta farasi wakiwa katika shughuli tofauti.

Baadhi wanaoshwa na kuvishwa, wengine wanalishwa huku zaidi wakifanya mazoezi ya kuruka viunzi ugani.

Tunapoingia kukutana na mtunzaji na mkufunzi wa farasi katika kituo hiki cha Forward Equestrian Centre Isaac Macharia Mwangi, farasi kadhaa wanaondoka kwenda nyanjani wakiwa wanaendeshwa na watoto pamoja na watu wazima.

“Aghalabu huu ni uraibu wa watu wenye hadhi katika maisha na hasa wazungu wanaoishi Kenya. Karibuni tufurahie,” Mwangi anatupokea kwa tabasamu.

Forward Equestrian Centre ilibuniwa miaka 2 iliyopita na mraibu wa farasi aliyetaka kupanua tasnia hii kwa waraibu zaidi na kwa nia ya kujichumia donge nono kwenye biashara inayovutia wateja wa tabaka la juu.

Mmiliki wa shamba hili, Douglas Kimani Macharia, 50, anatueleza kuwa ilimgharimu angalau kima cha Sh6 milioni kuanza ufugaji huu.

Chumba cha kuwatunzia farasi na kuweka baadhi ya maforonya. PICHA | LABAAN SHABAAN

Pia, wao ni wanachama wa Muungano wa Wafugaji Farasi Kenya (HAK) ambapo wanapata mwelekeo wa kuboresha zaraa hii.

“Kuendesha farasi ni uraibu wangu. Nina nia ya kuwavutia watu zaidi kuchangamkia ufugaji na uendeshaji wa farasi kibiashara na kimichezo,” Kimani anaeleza.

Kuna farasi 25 wanaofugwa humu ambapo sita wanatumiwa kufunzia wateja kuendesha wanyama hawa.

Mkufunzi Isaac Mwangi anasema kuwa hususan wanafuga farasi aina ya thoroughbred ambao ni mwafaka kwa mashindano ya farasi.

“Tuna farasi wa kibinafsi. Hii ina maana kuwa unaleta farasi wako hapa tunakutunzia, tunamfunza na kadhalika. Mwezi mmoja kumtunza bila mafunzo unagharimu Sh40 000. Tunamfunza farasi kwa Sh3000 kwa kila awamu mara mbili kwa siku,” Mwangi anasema akidhihirisha mazoezi ya farasi hayafiki kikomo.

“Huyu farasi tuliyesimama naye hapa tulimnunua Sh700,000 na ukimvisha mavazi kikamilifu vifaa hivyo itapita Sh1 milioni. Sitakudanganya, farasi ni kama gari, wanaweza kuwa hata wa mamilioni ya pesa,” anaongeza.

Farasi vile vile huvalishwa viatu kuepuka baridi na majeraha wanapotembea ama wanaposhiriki michezo.

“Viatu bora vya farasi hugharimu Sh4,000 kwa jozi. Kwa jinsi farasi ana miguu minne basi atakuwa na pea mbili,” anasema Isaac.

Forward Equestrian Centre wana ratiba ya lishe ya farasi inayotengenezwa kwa ushauriano na daktari wao wa farasi.

Kila farasi ana mtindo wake wa malisho unaomfaa lakini wasimamizi wa shamba hili wanakiri gharama ya kulisha wanyama hawa imepanda mno.

“Kulisha farasi chakula cha kawaida kunagharimu kati ya Sh5,000 hadi Sh15,000 kwa mwezi. Ukiboresha lishe gharama inapanda zaidi,” Mwangi anasema.

Farasi huhitaji uangalizi wa hali ya juu kuhakikisha wana afya na katika hali nzuri ya kushiriki mashindano na kustarehesha waendeshaji.

Mwendeshaji farasi akiwa juu ya mnyama huyo. PICHA | LABAAN SHABAAN

Kwa mujibu wa muungano wa madaktari wa HAK, umakinifu wa chanjo ya magonjwa ya farasi, kichaa, pepopunda na homa ya farasi unahitajika.

Kadhalika, kama binadamu, farasi hupewa dawa ya minyoo kila baada ya miezi mitatu.

Wafugaji wananasihiwa kuondoa vinyesi vya farasi uwanjani kila mara kukata mzunguko wa minyoo. na ikiwezekana kuuza kama mbolea ama kuteketeza uchafu wa wanyama hawa.

Forward Equestrian Centre inalenga kufanya ufugaji wa farasi uwe wa kibinafsi kikamilifu ambapo watatunza farasi wanaomilikiwa na watu wengine bila kuruhusu wasio na farasi kuwatumia.

Miaka miwili baadaye wanasema wameanza kuvuna donge bila kutaja kiasi na wanaamini mustakabali wao ni angavu.

Walianza na farasi wawili na sasa wana fahari kuwa wameajiri wafanyakazi 17 ambao wanasimamia farasi 25.

  • Tags

You can share this post!

ZARAA: Uwezo wa njugu kupunguza gharama mafuta ya kupikia

Joho na Sonko walimana ngumi kituo cha kura

T L