• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
BENSON MATHEKA: Rais ahakikishe mawaziri matajiri wanajali mahasla

BENSON MATHEKA: Rais ahakikishe mawaziri matajiri wanajali mahasla

NA BENSON MATHEKA

KITU kimoja kilichoibuka katika mahojiano ya kuwapiga msasa mawaziri wateule wiki jana ni kwamba wote 22 ni matajiri wa kupigiwa mfano.

Ufichuzi wao kwamba ni mabilionea na mamilionea unawafanya kuonewa wivu na wakati huo huo kuibua maswali kuhusu kauli mbiu ya serikali ya Kenya Kwanza ya kujali mahasla, yaani walalahoi na kuinua hali zao za kiuchumi.

Sidhani kuna bilionea au milionea anayelala njaa au kutatizika kulipia karo watoto wake na kushindwa kumudu gharama ya matibabu kama walalahoi.

Kilichojitokeza ni kwamba tofauti kati ya walalahoi waliokuwa wakisakata densi na wanasiasa waliokuwa wakiwashangilia walipokuwa wakijifanya mahasla kuwaomba kura ni kama mchana na usiku, mashariki na magharibi, ardhi na mbingu, hawatakaribiana.

Itachukua kutembelewa na Roho Mtakatifu kwa Baraza la Mawaziri linaloelea katika utajiri wa jumula ya Sh15 bilioni, wasiojua makali ya njaa kuwa na nia ya dhati ya kuinua masikini.

Kwa sababu mahlsa ni wepesi wa kudanganyika, wataamini chochote wanachoambiwa na mabilionea hao kwamba wao ni wajumbe wa heri njema.

Hapa itahitaji mkubwa wao, Rais William Ruto, ambaye safari yake ya maisha inathibitisha alionja uhasla, kama walivyo baadhi ya mawaziri hao, kushika mjeledi kuwa tayari kuwagutusha mawaziri wake kila wakati wanapozama katika kina cha utajiri wao na kuchukulia walalahoi kama ganda la muwa.

Rais Ruto anafaa kuwapa mwongozo wa utendakazi unaoweka maslahi ya raia wa kawaida mbele, kati kati, na nyuma ya kila sera, mpango na mradi utakaoanzishwa na serikali yake.

Hii ndio njia ya pekee kuwafanya mahasla kuamini kuwa mabilionea na mamilionea alioteua kuunda serikali yake watamsaidia kutekeleza ajenda zake na sio kuwabeza na kuwadharau walipa ushuru kwa sababu ya hali yao duni ya kiuchumi.

  • Tags

You can share this post!

Mayatima wa Raila waingizwa baridi na Miguna, Kidero

Mkenya Tikolo aajiriwa kocha mkuu wa timu ya taifa ya...

T L