• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
Mayatima wa Raila waingizwa baridi na Miguna, Kidero

Mayatima wa Raila waingizwa baridi na Miguna, Kidero

WANDANI wa kiongozi wa ODM Raila Odinga katika eneo la Nyanza wameingiwa na hofu kwamba kustaafu kwake katika siasa kutasababisha migawanyiko ya kisiasa katika jamii ya Waluo.

Wakiongozwa na mwenyekiti wa ODM, Bw John Mbadi, viongozi hao wanamtaka waziri huyo mkuu wa zamani kusalia katika ulingo wa siasa, wakimtaja kama gundi inayoleta mshikamano eneo hilo.

Bw Mbadi, ambaye ni mbunge maalum, amemtetea Bw Odinga na familia yake ambao wamekemewa na wakosoaji wao wanaotaka kuwaondoa katika midani ya siasa.

Lakini, mbunge huyo na wenzake, wamewapuuzilia mbali mahasidi hao wakisema kushindwa kwa Bw Odinga katika uchaguzi mkuu wa Agosti 9 hakufai kutumiwa kama sababu ya kumsukuma aondoke siasani.

“Raila Odinga bado ndiye kinara wa siasa katika eneo hili la Luo Nyanza, ndiye gundi inayoshikamanisha jamii hii. Kuondoka kwaka siasa kutasababisha mgawanyiko miongoni mwa wafuasi wake sio tu hapa Nyanza bali kote nchini,” Bw Mbadi akasema Jumamosi.

“Wale ambao wanampiga vita Raila wajue kuwa hatutawaruhusu kugawanya jamii yetu kwa ajili ya manufaa yao kama watu binafsi. Ningependa kuwaambia peupe kwamba njama yao haitafaulu,” akaongeza.

Alikuwa akiwahutubia waombolezaji katika hafla ya mazishi ya Mzee Stanley Aluma, babaye Mbunge wa Homa Bay Mjini, Peter Kaluma katika kijiji cha Ndiru, wadi ya Rodi Kopany.

Viongozi wengine waliohudhuria mazishi hayo ni pamoja na kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, magavana Gladys Wanga (Homa Bay) na James Orengo (Siaya), maseneta Moses Kajwang (Homa Bay), Tom Ojienda (Kisumu), Oburu Oginga (Siaya) na Kennedy Oketch (Migori).

Wabunge wa mrengo wa Azimio waliokuwepo ni pamoja na Ong’ondo Were (Kasipul), Eve Obara (Kabondo Kasipul), Lilian Gogo (Rangwe), Felix Odiwuor (Lang’ata), Adipo Okuome (Karachuonyo) Antony Oluoch (Mathare), Roza Buyu (Kisumu Magharibi) na Mille Odhiambo (Suba Kaskazini).

Kwa pamoja, viongozi hao waliapa kumtetea Bw Odinga dhidi ya mashambulio kutoka kwa wale waliowataja kama “maadui wa umoja wa Nyanza”.

Bw Mbadi, na wenzake walisema haya siku chache baada ya wakili mbishani Miguna Miguna kudai kuwa analenga “kukomboa” Nyanza kwa kuyeyesha ushawishi wa Bw Odinga, na familia yake, ambao wamedhibiti siasa za eneo hilo tangu uhuru.

“Watu wetu wa Nyanza wamechangia pakubwa katika ukombozi wa kwanza na ule wa pili nchini Kenya na hata kupatikana kwa katiba ya sasa. Lakini hawajafaidi inavyostahiki kwa sababu ya siasa mbaya ya familia ya Odinga. Ninataka kuongoza kampeni ya kukomboa watu wetu ili wafaidi,” Bw Miguna akasema Ijumaa wiki jana kwenye mahojiano katika runinga ya NTV.

Aliyekuwa gavana wa Nairobi, Dkt Evans Kidero pia ametangaza vita vya kisiasa dhidi ya Bw Odinga katika eneo hilo.

Bw Musyoka pia anasemekana kutaka kurithi ngome hiyo ya kisiasa ya Bw Odinga.

Jana Jumapili, kiongozi huyo wa Wiper alitua jijini Kisumu alikohimiza umoja miongoni mwa viongozi na wakazi wa Nyanza.

Lakini Miguna Miguna na Dkt Kidero ndio wamewakera zaidi wandani wa Bw Odinga, kutokana na nia yao ya kufanya ‘mapinduzi’ ya kisiasa dhidi ya kiongozi huyo wa ODM.

Mwezi Septemba, Dkt Kidero alitoa wito kwa wanasiasa wa Nyanza waliokwazwa kisiasa kuungana naye (Kidero) kuunda chama kipya kitakachoyeyusha umaarufu wa ODM katika eneo la Luo Nyanza.

“Viongozi ambao wamejitolea mhanga kuvumisha ODM wamesalitiwa kwa sababu Raila anachukulia chama hicho kama mali yake ya kibinfsi. Ninawaomba tuungane kuunda chombo ambacho kitatusaidia kutetea masilahi yetu katika ngazi ya kitaifa,” akasema kupitia taarifa fupi aliyoweka katika ukurasa wake wa Facebook.

Lakini Jumamosi, Bw Mbadi alipuuzilia mbali juhudi za Dkt Kidero akisema kuwa chama ambacho gavana huyo wa zamani ananuia kuunda hakitapata ushawishi wowote eneo la Nyanza.

“Hawezi kuwa kinara wetu. Hajahitimu kuwa kiongozi wa jamii yetu katika nyanja yoyote. Kiongozi wetu angali Raila Amolo Odinga,” akasema.

Wadadisi wanasema wandani wa Bw Odinga wameingiwa na hofu kwamba akiondoka katika ulingo wa siasa, wao ndio watakaopoteza mazuri mengi.

“Wengi wa wanasiasa hawa wamekuwa wakining’nia kwenye ‘koti’ la Raila kupata nafasi ya kuingia bunge, kwa kisingizio cha kumsaidia Odinga kafanikisha ndoto yake ya Ikulu. Hii ndiyo maana wameingiwa na kiwewe baada ya Kidero na wengine kutoa tangazo la ukombozi wa kisiasa Nyanza,” anasema aliyekuwa mwenyekiti wa Mamlaka ya Ustawi wa Eneo la Ziwa (LBDA), Odoyo Owidi.

  • Tags

You can share this post!

Urusi sasa yalenga vituo vya umeme nchini Ukraine

BENSON MATHEKA: Rais ahakikishe mawaziri matajiri wanajali...

T L