• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 12:58 PM
CECIL ODONGO: Ruto aondoe Keynan kamati ya mazungumzo na upinzani

CECIL ODONGO: Ruto aondoe Keynan kamati ya mazungumzo na upinzani

NA CECIL ODONGO

RAIS William Ruto anafaa kuondoa jina la mbunge wa Eldas, Bw Adan Keynan, katika kamati ya mazungumzo baina ya upinzani na serikali, kusaka suluhisho kwa baadhi ya matatizo yaliyosukuma upinzani kuandaa maandamano mwezi jana.

Kamati hiyo ilibuniwa kutokana na ombi la Rais Ruto kushughulikia masuala yaliyoibuliwa na muungano wa upinzani Azimio, wakati maandamano yalichacha Machi. Wiki jana, kamati hiyo iliafikiana kuhusu baadhi ya masuala na kuacha mengine tata, ambayo sasa yataamuliwa na Rais Ruto na kinara wa upinzani Raila Odinga. Kati ya masuala hayo ni uwepo wa Bw Keynan, ambaye ni mbunge wa Jubilee, kati ya wanachama wa mrengo tawala wa muungano wa Kenya Kwanza (KKA).

Pia upande wa KKA unalalamikia kujumuishwa kwa mbunge wa Pokot Kusini, Bw David Pkosing, kwenye orodha hiyo. Bw Pkosing alichaguliwa kwa tikiti ya KUP, inayoongozwa na aliyekuwa Gavana wa Pokot Magharibi, Bw John Lonyangapuo. Wabunge wa Azimio walidai kujumuishwa kwa Bw Keynan katika orodha ya wanachama wa Kenya Kwanza haukustahili, kwa sababu chama kilichomdhamini kipo kwenye muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya (Azimio). Bw Keynan ndiye mbunge ambaye amehudumu kwa muda mrefu zaidi bungeni; alichaguliwa mara ya kwanza mnamo 1997.

Anahudumu muhula wake wa sita baada ya kushinda pembamba katika uchaguzi mkuu uliopita. Matokeo ya kura eneobunge lake yaligubikwa na ghasia huku akitolewa kijasho na mwaniaji wa ODM, Bw Omar Boraya. Hata hivyo, huenda kujumuishwa kwake kulifanywa kimakusudi kama mkakati wa KKA kutia doa mazungumzo na upinzani.

Jubilee ipo katika Azimio na Bw Keynan mwenyewe hajajiuzulu kutoka chama hicho ili kusaka ubunge kwa mara nyingine. Iweje sasa atawakilisha serikali ilhali ni mbunge wa upinzani? Kuna kanuni iliyowekwa ya chama kujiondoa katika muungano wa Azimio na hilo linaweza kufanyika tu baada ya miezi sita, ambayo sasa yameshapita.

Hata hivyo, sheria inasisitiza kuwa utaratibu unastahili kufuatwa ili ngazi zote za uongozi wa muungano zifahamishwe pamoja na msajili wa vyama vya kisiasa. Jubilee bado haijaandikia Azimio kuwa inataka kujiondoa.

Kwa Bw Pkosing, Azimio wapo sawa kumjumuisha kwani KUP bado ni chama tanzu ndani ya muungano huo kama tu Jubilee. Iwapo serikali inataka upinzani utupilie maandamano ambayo yatakuwa yakirejelewa Mei 2, iwe na nia njema kuhusu mazungumzo. Kumjumuisha mwanasiasa wa upinzani kuwakilisha serikali ni dharau na kejeli.

  • Tags

You can share this post!

Kontena kutumika kuhifadhi miili baada ya mochari kujaa

CHARLES WASONGA: Serikali, maafisa wa polisi wasivuruge...

T L