• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
CECIL ODONGO: Ruto na Raila hawawezi kutatua jinamizi la uskwota katika maeneo ya Pwani

CECIL ODONGO: Ruto na Raila hawawezi kutatua jinamizi la uskwota katika maeneo ya Pwani

NA CECIL ODONGO

VIONGOZI wa kisiasa hawafai kutumia suala la ardhi kuvutia kura za wakazi wa Pwani ilhali wakiingia mamlakani wanalisahau na kumakinikia masuala mengine.

Katika chaguzi za nyuma, suala hilo limekuwa likitumiwa kuvutia kura za eneo hilo ilhali hakuna utatuzi wowote wa maana kwalo hadi leo. Kinaya ni kuwa wanasiasa Pwani nao wamegawanyika kuhusu suala hilo wakiunga mirengo inayochangia kutoshughulikiwa kwa uskwota ambao ni tatizo la tangu jadi.

Katika kampeni zake ukanda wa Pwani, Naibu Rais, Dkt William Ruto amekuwa akijisawiri kuwa ndiye dawa tosha ya uskwota Pwani. Hii ni licha ya kuwa katika chaguzi za 2013 na 2017, utawala wa Jubilee uliahidi kuwa ungelitatua ilhali hadi leo hakuna lililofanyika.

Je, kwa nini Dkt Ruto hakushirikiana na Rais Kenyatta hasa katika awamu ya kwanza ya utawala wao kumaliza uskwota na sasa anataka Wapwani waamini atalishughulikia akiwa Rais. Dkt Ruto mwenyewe anamiliki maelfu ya ekari za ardhi Pwani na hivi majuzi alisema zaidi ya ekari 2,500 anazomiliki Taita Taveta alinunua kutoka kwa mbunge wa zamani wa Taveta, Bw Basil Criticos baada ya kumsaidia kulipa mkopo wa benki.

Hakuna asiyefahamu kuhusu utata unaozunguka ardhi anazomiliki Bw Criticos na jinsi alivyochangia tatizo la uskwota Pwani

Kwa hivyo, Dkt Ruto anayemiliki ardhi maeneo mengine nchini hawezi kusuluhisha suala hilo kama hakufanya hivyo akiwa Naibu Rais hasa kwa sababu alinunua ardhi kutoka kwa waliochangia uskwota Pwani.

Kwa upande mwingine, kinara wa ODM Raila Odinga naye amemteua Gavana wa Mombasa, Hassan Joho kama waziri ya Ardhi iwapo atafaulu kuwa rais. Hata hivyo, Bw Odinga amekuwa na mazoea ya kutumia suala hili kila mwaka wa uchaguzi ilhali alipokuwa waziri mkuu, mwandani wake James Orengo, akiwa waziri wa Ardhi hakutatua uskwota.

Kwa kifupi, Dkt Ruto na Bw Odinga wanawahadaa wakazi wa Pwani kuhusu kutatua masuala ya ardhi na wanafahamu vyema kuwa wao ni mateka wa mabwenyenye wanaomiliki ekari kadhaa za ardhi Pwani na wamechangia uskwota miaka nenda miaka rudi.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Tusifanyie suala la ardhi mchezo kama ilivyo sasa

WANDERI KAMAU: Kinaya cha ‘ubabe’ wa kijeshi...

T L