• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
CHARLES WASONGA: Ruto aimarishe miradi ya unyunyiziaji kukuza mazao

CHARLES WASONGA: Ruto aimarishe miradi ya unyunyiziaji kukuza mazao

UZINDUZI wa Bwawa la Thiba katika Kaunti ya Kirinyaga wiki jana umeleta mwamko mpya katika kilimo cha mpunga katika eneo hilo.

Bila shaka mradi huo, uliogharimu Sh7.8 bilioni, utawafaidi pakubwa wakulima wa zao hilo kwenye mashamba ya Mpango wa Unyunyiziaji wa Mwea.

Kwa kuwa asilimia 75 ya mchele unaozalishwa nchini hutoka Mwea, mradi huo utachangia kuimarika kwa uzalishaji wa zao hilo kwa manufaa ya taifa kwa ujumla.

Bwawa hilo lenye uwezo wa kuhifadhi lita 15.6 milioni za maji sasa litawezesha eneo la ukubwa wa ekari 10,000 zaidi kutumika katika upanzi wa mpunga.

Wakati huu, ardhi ya ukubwa wa ekari 25,000 katika eneo la Mwea ndio inatumika katika uzalishaji wa mchele.

Hii ina maana kuwa wakulima wakianza kutumia maji ya bwawa hili watakuza mpunga katika mashamba ya ukubwa wa ekari 35,000, ishara kwamba uzalishaji utaimarika zaidi ya ulivyo sasa.

Rais William Ruto amezindua mradi huu wakati ambapo zaidi ya Wakenya milioni nne katika kaunti 24 wanakabiliwa na baa la njaa.

Kulingana na Mamlaka ya Kitaifa ya Kupambana na Majanga (NDMA), kwa kiwango kikubwa changamoto hii imesababishwa na kiangazi kikali kinachotokana na mabadiliko ya tabia nchini.

Funzo kwa Serikali ya Dkt Ruto ni kwamba inafaa kuelekeza juhudi zake katika kuanzisha miradi ya ujenzi wa mabwawa makubwa kama vile Thiba, ili kupiga jeki kilimo cha unyunyiziaji.

Miradi ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer, katika kaunti ya Elgeyo Marakwet pia ifufuliwe.Kiangazi cha muda mrefu ambacho kimeshuhudiwa nchini tangu mwaka 2021, kinafaa kuipa serikali msukumo wa kuwekeza fedha nyingi katika kilimo cha unyunyiziaji badala ya kilimo cha kutegemea mvua.

Hii ndio njia ya pekee itakayowezesha taifa hili kuzalisha chakula cha kutosheleza mahitaji ya wananchi na hivyo kuwakinga na madhila yanayowazonga wakati huu.

Kenya haifai kutegemea chakula kinachoagizwa kutoka nje ilhali ina uwezo wa kuzalisha chakula hicho kupitia kilimo cha unyunyiziaji.

Kwa mfano, kulingana na ripoti ya 2021 kuhusu uchunguzi wa Hali ya Uchumi nchini, Kenya inahitaji tani 400,000 za mchele kila mwaka kutosheleza mahitaji ya wananchi.

Lakini Kenya ilizalisha tani 100,000 pekee ya zao hilo mwaka huo, sehemu kubwa ikitoka katika mashamba yaliyoko chini ya usimamizi wa Mpango wa Unyunyiziaji wa Mwea.

Hii ina maana kuwa jumla ya tani 300,000 za mchele ziliagizwa kutoka mataifa ya nje, kama vile Misri na Pakistan.

Nadhani uzalishaji mchele utaimarika mwaka ujao kupitia uzinduzi wa Bwawa la Thiba.

Vile vile, Kenya ilizalisha magunia 38.8 milioni ya mahindi mwaka huo ilhali inahitaji magunia 45.6 milioni, ili kutosheleza mahitaji ya raia wake.

Hii ina maana kuwa serikali ililazimika kutumia mabilioni ya fedha za umma kuagiza karibu tani milioni saba za mahindi ili kutosheleza mahitaji ya raia.

Mojawapo ya sababu zilizochangia tatizo hili ni kufeli kwa mradi wa uzalishaji chakula kupitia kilimo cha unyunyiziaji cha Galana Kulala.

Mradi huo ambao ulianzishwa na Serikali ya Jubilee mnamo Julai, 2015 ulilenga kuzalisha magunia 40 milioni ya mahindi kila mwaka baada ya kukamilika kwake mnamo 2018.

Kwa hivyo, Rais Ruto anafaa kujitwika wajibu wa kufufua miradi kama hii, kote nchini ambayo ilianzishwa na watangulizi wake lakini ikafeli kupitia usimamamizi mbaya na ufisadi.

  • Tags

You can share this post!

SHINA LA UHAI: Changamoto katika afya ya akili zabainika...

Wandani wa Uhuru wasema hawajutii kuunga Azimio

T L