• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 6:07 PM
SHINA LA UHAI: Changamoto katika afya ya akili zabainika wazi

SHINA LA UHAI: Changamoto katika afya ya akili zabainika wazi

NA WANGU KANURI

JOAN Chepkorir aligundua hali haikuwa shwari alipompoteza binamu yake akiwa shule ya upili.

Uchungu wa kumpoteza mwanafamilia huyo ulimfanya kujihisi mpweke, kuchanganyikiwa, mwenye uchungu mwingi moyoni.

Hakuweza kuenda kumzika binamuye kwa kuzingatia sheria za shule.

Kupata nafasi ya kuzungumza na mwalimu wake ambaye alikuwa mwanasaikolojia kulimsaidia kujua kuwa kifo cha binamuye kilikuwa kichochezi cha msongo wa mawazo ambao ulianza akiwa shule ya msingi.

“Nilinyanyaswa sana na wanafunzi wa shule hiyo na juhudi zangu za kueleza wazazi wangu nilichokuwa nikipitia ziligonga mwamba,” anaeleza.

“Nilipowaelezea wanafamilia, wengi wao walidhani ni mzaha na eti nilikuwa natafuta vijisababu ili nisiende shuleni. Sasa wakati binamu yangu aliaga dunia, nilihisi sina mtu aliyenielewa na nikajitenga,” anahadithia Chepkorir.

Baada ya kumaliza shule na kujiunga na chuo kikuu, Chepkorir aliweza kuendelea vyema hadi shangazi yake mwingine aliyekuwa akimpenda na kumweleza aliyokuwa akipitia bila kumshtumu akaaga dunia.

Kifo chake kilileta kumbukumbu za kifo cha binamuye na unyanyasaji aliopitia akiwa shule ya msingi.

“Nilikosa hamu ya maisha. Nikawa siendi darasani. Sikuwa mchangamfu kama awali. Kazi nilizokuwa nafanya kwa kawaida ikawa zinanilemea,” anaeleza.

Mkufunzi mmoja aliyeona mabadiliko yake alimshauri kumuona mtaalamu wa saikolojia ambaye alimpa dawa lakini zilikuwa ghali sana na hangeweza kuzigharamia kwa sababu hakuwa ameelezea wazazi wake.

“Nilikuwa nimejaribu kuwaeleza kuwa sikuwa najihisi vyema lakini walinipuuza. Kwa hivyo sikuwaeleza nilipokuwa nameza tembe,” asema.

Hata hivyo, Chepkorir aliweza kusaidiwa na dadake mkubwa aliyemlipia matibabu na hata akampa nafasi ya kujieleza bila kushutumiwa.

Chepkorir anasema kuwa hata ingawa alipata afueni, juhudi zake za kueleza wazazi wake kuhusu ugonjwa wa msongo wa mawazo bado hazikufaulu huku akishukuru sana walimu na dadake waliomfaa wakati huo.

Kisa chake ni moja kati ya vingi vya Wakenya wanaopata changamoto tele wanapotafuta ushauri au matibabu ya matatizo ya kiakili.

Huku ulimwengu ukiadhimisha ugonjwa huo mapema wiki jana, vikwazo kama hivi vilionyesha kuchangia sana kukosa afueni kwa mgonjwa.

Dkt Jacqueline Anundo, mtaalamu wa afya ya akili katika hospitali ya RFH anaeleza kuwa Kenya hurekodi visa vingi vya magonjwa ya msongo wa mawazo, wasiwasi (anxiety disorders) na matumizi ya dawa za kulevya.

Hata hivyo, changamoto ambazo wagonjwa hawa hupitia ni kutotafuta matibabu kutoka kwa wataalamu mapema hivi kuishia kwenda kwa watu wasio na ujuzi wa magonjwa ya akili.

“Kuna wale ambao hawasemi lolote kuhusiana na wanachopitia huku wakiishia kujitoa uhai au kupata mawazo ya kujitia kitanzi mambo yanapowawia vigumu,” anasema.

Licha ya magonjwa haya ya akili kutotambulika bayana, Dkt Anundo anasema kuwa unyanyapaa umechangia pakubwa dhidi ya kupata ushauri kwa wagonjwa wa akili.

Huku ikiwa nadra sana kumsikia mtu akisema kuwa anapokea matibabu ya magonjwa haya haswa kazini, Dkt Anundo anasema wagonjwa wengi huogopa kufutwa kazi au kutopandishwa cheo wanapojulikana wanaugua magonjwa haya.

Changamoto nyingine huwa pesa. Gharama ya matibabu ya magonjwa ya akili huwa ghali mno huku nyakati zingine mgonjwa akihitajika kumeza tembe ambazo hazigharamiwi na bima ya afya.

“Watu wengi pia hawaangazii afya yao ya akili kwa makini huku wanapougua wanadhani kuwa hawapaswi kugharamia matibabu na kutumia pesa hizo kujiendeleza kimaisha.”

Huku ikimgharimu mtu Sh4,000-Sh5,000 kila saa anapozungumza na mshauri wa masuala ya magonjwa ya akili, Dkt Anundo anasema kutotambua ugonjwa gani wa akili mgonjwa anao huchangia katika kupata matibabu yasiyofaa.

“Wakati mwingine mtu aliyepata tukio la ugonjwa wa akili anaweza kuwa na kingamwili iliyo chini hivyo kuugua kila mara na kushindwa kula vizuri. Mgonjwa huyu anapoenda hospitalini huangaziwa magonjwa yote huku afya yake ya akili ikiwa imepuuzwa,” anaeleza.

Ili wagonjwa wa akili waweze kupata afueni haraka, Kagondu Junior, mshauri wa masuala ya afya ya akili anasema kuwa watu walio karibu sana na mgonjwa huyo wanapaswa kutoa huduma kwa upendo.

“Wanapaswa kuwa wenye rehema na kuwapa nafasi ya kujieleza bila kuwashtumu wala kuwakaripia. Vile vile, wanapaswa kuwasaidia kushirikiana na watu wengine kwani wagonjwa hawa hupendelea sana kukaa peke yao,” anasema.

Kuwashirikisha wagonjwa hao na wengine wanaougua magonjwa tofauti ya akili huwapa motisha na pia huwapa mazingira ya kujieleza na ya kusikia wagonjwa wengine.

Licha ya magonjwa ya akili kuchukuliwa kuwa uendawazimu, Kagondu anasema kuwa kutokuwa na ujuzi na maarifa kuhusu magonjwa haya huchangia pakubwa katika jinsi mtu humfaa mgonjwa.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linaeleza kuwa nchini Kenya mtu mmoja kati ya wanne huugua magonjwa ya akili huku msongo wa mawazo na matumizi ya dawa za kulevya yakirekodi idadi kubwa.

Hata hivyo, licha ya kuwepo kwa wataalamu 400 wa magonjwa ya akili, changamoto kubwa kwa wagonjwa hao ni kutopata huduma nzuri na kutotambulika mapema kwa magonjwa hayo.

Inakadiriwa kuwa bilioni 12 za siku za kazi hupotezwa kila mwaka sababu ya wafanyikazi kuugua magonjwa ya akili huku ripoti ya WHO kuhusiana na Afya ya Akili ikionyesha kuwa asilimia 15 ya wafanyikazi huugua magonjwa ya akili.

Ripoti ya shirika hilo ya mwaka wa 2017 ilionyesha kuwa Kenya ilikuwa nambari tano Barani Afrika zilizo na idadi kubwa ya visa vya msongo wa mawazo.

  • Tags

You can share this post!

Makwapa yangu yamekuwa meusi

CHARLES WASONGA: Ruto aimarishe miradi ya unyunyiziaji...

T L