• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:50 AM
CHARLES WASONGA: Uteuzi tata wa Igathe huenda ukamkosesha ugavana Nairobi

CHARLES WASONGA: Uteuzi tata wa Igathe huenda ukamkosesha ugavana Nairobi

NA CHARLES WASONGA

UAMUZI wa muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya kumwidhinisha Bw Polycarp Igathe, dakika za mwisho, kuwa mgombea ugavana katika Kaunti ya Nairobi huenda ukachangia muungano huo kushindwa kutwaa kiti hicho Agosti 9.

Wakuu wa muungano huo hawakutenda haki kwa kuwashinikiza Bw Fred Ngatia na Mbunge wa Westlands, Tim Wanyoyi wajiondoe kinyang’anyironi ili wampishe Bw Igathe ambaye awali hakuwa ameaonyesha nia ya kuwania kiti hicho.

Hii ni kwa sababu Bw Wanyonyi alijitosa katika kivumbi cha ugavana miaka miwili huku Bw Ngatia, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Kitaifa cha Wenye Biashara na Viwanda (KNCCI) alianza kukimezea mate kiti hicho mapema mwaka huu.

Wawili hao wamekuwa wakiendesha kampeni zao huku Bw Igathe akiendelea kuchapa kazi kama Afisa Mkuu wa Masuala ya Kibiashara katika Benki ya Equity.

Hadi Ijumaa wiki jana, wafuasi wa Azimio, wale wa muungano wa Kenya Kwanza na wakazi wa Nairobi, kwa jumla walikuwa wameamini kuwa mmoja kati ya Wanyonyi na Ngatia ndiye angeteuliwa kuwania ugavana wa Nairobi.

Wawili hao walikuwa wakiuza sera zao kwa wakazi wa Nairobi kupitia majukwaa mbalimbali, wakijiandaa kupambana na mwaniaji wa Kenya Kwanza, Seneta Johnson Sakaja.

Bw Wanyonyi alitaka kuwania kiti hicho kwa tiketi ya ODM huku Bw Ngatia akisaka tiketi ya chama tawala cha Jubilee.

Sasa swali langu ni je, ni sifa gani wakuu wa Azimio; Rais Uhuru Kenyatta na Raila Odinga, waliona ndani ya Bw Igathe ndipo ikawashawishi kuwa ndiye anayeweza kuletea muungano huo ushindi?

Je, atajipa umaarufu wa kutosha ndani ya muda wa miezi mitatu ijayo kabla ya wakazi wa Nairobi kuelekea debeni kuchagua gavana mpya ilhali hajawa akifanya kampeni yoyote hapo awali?

Ikiwa kweli Jubilee ilitaka kumdhamini Igathe kuwania ugavana wa Nairobi chini ya mwavuli wa muungano wa Azimio, ingemshauri aanze kampeni za mapema ili kujiuza kwa wapiga-kura alivyofanya Bw Ngatia.

Rais Kenyatta na Bw Odinga wangeelewana mapema kuhusu suala hilo muhimu la kudhamini mgombeaji wa ugavana wa Nairobi badala ya kujivuta hadi Ijumaa wiki jana; wakati ambapo Wanyonyi na Ngatia walikuwa wametumia rasilimali nyingi kufanya kampeni.

Ninakubali kwamba Bw Igathe ni mwaniaji aliyehitimu kuwa gavana wa Nairobi, kutokana na tajriba ya usimamizi aliyopata katika kampuni ya Vivo na Benki ya Equity.

Lakini namna ambavyo Rais Kenyatta na Bw Odinga wamemwasilisha kwa wakazi wa Nairobi inaibua fikra kwamba huenda vinara hao wa Azimio wanaongozwa na ajenda fiche.

Ingawa Bw Igathe anaweza kuwa gavana ambaye atawafaa wakazi wa Nairobi, kuidhinishwa kwake katika mkutano wa faragha katika Ikulu ya Nairobi kunamfanya kuwa “mradi” watu fulani wenye ushawishi serikali, almaarufu “Deep State”.

Dhana hii itamfaa Bw Sakaja katika kampeni zake kwa sababu itakuwa rahisi kwamba kuwashawishi wakazi wa Nairobi kwamba wanafaa kumkataa Bw Igathe.

Wapiga kura wa Nairobi watashawishika kwa urahisi na kauli hiyo hali ambayo itawafanya kumkataa Bw Igathe debeni Agosti 9, hata kama manifesto yake huenda ikawa bora kuliko ile ya Bw Sakaja.

Wapiga kura wamepevuka. Hawatakubali vigogo wa kisiasa kuwaelekeza kuwapigia kura wawaniaji fulani kinyume na matakwa yao.

Walidhihirisha hili katika chaguzi za mchujo zilizoendeshwa na vyama vya United Democratic Alliance (UDA) na ODM zilizokamilika juzi.

  • Tags

You can share this post!

JIJUE DADA: ‘Coil’ isipokaa vizuri utahisi uchungu...

Mbogo asita kumuunga mkono Sonko Mombasa

T L