• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Mbogo asita kumuunga mkono Sonko Mombasa

Mbogo asita kumuunga mkono Sonko Mombasa

NA WINNIE ATIENO

ALIYEKUWA Gavana wa Nairobi Mike Sonko huenda akapata pigo baada ya Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo kusema hakutia saini makubaliano ya kuwa mgombea mwenza wake wa kiti cha ugavana Mombasa kwenye uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Bw Mbogo alisema hakutia saini mkataba huo akisubiri uamuzi wa wapiga kura wake wampe mwelekeo.Hata hivyo alisema yuko tayari kugombania kiti chake cha ubunge wa Kisauni iwapo wafuasi wake watakubali.

“Nitafuata mwongozo kutoka kwenu mkitaka nisalie kama mbunge ama niwe mgombea mwenza wa Bw Sonko. Sijatia saini mkataba, nilikataa kutia saini nikasema lazima nirudi kwa watu wangu, niombe radhi zao, nisikize maoni yao. Mkisema barabara iko sawa sitarudi nyuma,” alisema.

Alisema anapigana vita kuikomboa Mombasa.

“Lakini sitaweza peke yangu, hawa mabwana wameungana. Tumeona juzi mgombea wa ugavana Bw Suleiman Shahbal amejiuzulu na kumuunga mkono mbunge wa Mvita Abdulswamad Nassir,” alisema Bw Mbogo.

Alitoa mfano wa uchaguzi wa 2013, Dkt William Ruto na chama chake cha URP aliungana na kinara wa TNA Bw Uhuru Kenyatta wakaungana na kuunda chama cha Jubilee walichotumia kuwania urais na wakashinda.

“Dkt Ruto alikubali kuwa naibu wa Bw Kenyatta na hii leo, miaka 10 baadaye anagombania urais. Sijafanya maamuzi, nyinyi ndio mtanipa mwongozo watu wangu wa Kisauni sababu lengo letu ni kumaliza watu ambao wanataka kutunyonya damu kama kunguni,” alisema.

Bw Mbogo alisema chini ya uongozi wa Gavana Hassan Joho, Mombasa haijanufaika na ugatuzi akimshtumu gavana huyo kwa kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo.

“Ninawauliza kama mko tayari kwa Bw Mbogo kuungana na Bw Sonko. Mimi niko tayari kwa lolote, mkiniambia nirudi ubunge nitarudi. Mimi ninasikiza maoni yenu. Mko tayari tukomboe Mombasa na Bw Sonko? Ikiwa mtanipa radhi zenu, huu si muungano wa naibu gavana wa kawaida, nitakuwa na asilimia 60 ya serikali kumaanisha bado tutatimiza malengo yetu,,” alisema.

Mbunge huyo wa Kisauni alipewa asilimia 60 ya uongozi wa kaunti katika makubaliano yaliyosimamiwa na Kiongozi wa Wiper Bw Kalonzo Musyoka ambapo Bw Sonko alipewa tikiti ya kuwania ugavana wa Mombasa.

Wengine wanaogombania ugavana ni pamoja na naibu gavana Dkt William Kingi (Pamoja African Alliance), aliyekuwa seneta wa Mombasa Bw Hassan Omar (United Democratic Alliance) na aliyekuwa mbunge wa Nyali Bw Hezron Awiti (VDP).

Baada ya Bw Sonko kukubaliana na Bw Mbogo kuwania ugavana wa Mombasa, hisia mseto ziliiibuka huku mbunge huyo akishtumiwa kushawishiwa kuacha azma yake.

Baadhi ya wakazi wa Mombasa na watetezi wa haki za kibinadamu walipinga hatua hiyo wakisema Bw Sonko ambaye alibanduliwa na bunge la kaunti ya Nairobi na hafai kugombea ugavana wa Mombasa kutokana na madai ya ufisadi dhidi yake.

Wakiongozwa na Bw Khelef Khalifa, watetezi hao walisema awali tikiti hiyo ilikuwa imepewa kwa Bw Mbogo ambaye ameshurutishwa kuwa mgombea mwenza wa Bw Sonko.

Kwenye makubaliano yao, katika ugawaji wa mamlaka Bw Sonko atampa Bw Mbogo asilimia 60 ya serikali watakayobuni.

  • Tags

You can share this post!

CHARLES WASONGA: Uteuzi tata wa Igathe huenda ukamkosesha...

Ukraine yaomba Urusi kukubali mazungumzo

T L