• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
CHARLES WASONGA: Wabunge watekeleze wajibu wao bila miegemeo ya kisiasa

CHARLES WASONGA: Wabunge watekeleze wajibu wao bila miegemeo ya kisiasa

NA CHARLES WASONGA

BUNGE la 11 lililaumiwa mno kwa kutumiwa na serikali ya Jubilee kupitisha miswada iliyoendeleza utawala mbaya na kuathiri Wakenya.

Kwa mfano, mnamo Desemba 18, 2014, Bunge lilipitisha Mswada wa Marekebisho ya Sheria za Usalama katika kikao kilichosheheni fujo na makabiliano kati ya wabunge wa mirengo ya Jubilee na wale wa muungano wa upinzani, CORD, wakati huo.

Sehemu kadha za mswada zilisheheni mapendekezo ambayo yalihujumu uhuru wa vyombo vya habari na haki ya Wakenya kujieleza, jambo ambalo ni kinyume cha vipengele 34 na 35 vya Katiba, mtawalia.

Serikali ilijitetea kwa kudai kuwa ilidhamini mswada huo kwa lengo la kupambana na ongezeko la visa vya mashambulio ya kigaidi, ambavyo vilikuwa tishio kwa usalama wa nchini.

Kwa kutumia wingi wa idadi ya wabunge wa Jubilee bungeni wakati huo (216), pamoja na Spika Justin Muturi aliyechaguliwa kwa usaidizi wa mrengo huo, serikali ilifaulu kupitisha mswada huo wenye mapendekezo dhalimu.

Rais Uhuru Kenyatta, akitiwa shime na naibu wake William Ruto, alitia saini mswada kuwa sheria dakika chache tu baada ya kupitishwa bungeni katika kikao kilichojivuta hadi usiku.

Hata hivyo, mahakama ilibatilisha sehemu nane za sheria hiyo kwa misingi ya kukiuka Katiba.Mswada mwingine ambao athari zake zinaumiza Wakenya hadi sasa ni ule wa Fedha wa 2016, uliopendekeza kuwa petrol, dizeli na mafuta taa zitozwe ushuru wa bidhaa (VAT) wa kiwango cha Sh 16 kwa lita moja.

Mswada huo pia ulidhaminiwa na serikali na kuwasilishwa bungeni na aliyekuwa Kiongozi wa Wengi, Aden Duale.Kuanzishwa kwa ushuru huo, na nyinginezo, ndio zimechangia bei ya juu ya mafuta nchini kwa sasa na kupanda kwa gharama ya maisha.

Nimetoa kumbukumbu hizi ili Wakenya waelewe hatari inayowakodolea macho, kufuatia hatua ya Rais mteule Dkt Ruto kuvutia baadhi ya wabunge wa mrengo wa Azimio la Umoja-One Kenya wajiunge na Kenya Kwanza.

Sikubaliani na kauli ya Dkt Ruto kwamba hatua hiyo ni ya kumwezesha kufanikisha ahadi alizotoa kwa Wakenya wakati wa kampeni za kusaka kura.

Lengo lake kuu la “kununua” wabunge hao wa Azimio ni kulemaza upinzani ili aweze kuendeleza utawala mbaya kwa kupitisha miswada kidikteta na kulemaza sauti za wakosoaji.

Kwenye hotuba aliyotoa ukumbi wa Bomas wiki jana baada ya kutangazwa mshindi, Dkt Ruto aliahidi kufanya kazi na upinzani mradi utatathmini utendakazi wa serikali kwa manufaa ya Wakenya.

Lakini unafiki wake sasa unajitokeza katika juhudi hizo zake za kudhoofisha nguvu ya upinzani ndani na nje ya Bunge.

  • Tags

You can share this post!

BENSON MATHEKA: Kenya Kwanza haifai kusuta Azimio kwenda...

Chebukati achapisha rasmi majina ya wabunge 286 walioshinda...

T L