• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
DOUGLAS MUTUA: EAC ibuni jopo la viongozi wasifika kutatua mizozo kati ya wanachama

DOUGLAS MUTUA: EAC ibuni jopo la viongozi wasifika kutatua mizozo kati ya wanachama

NA DOUGLAS MUTUA

UWEZEKANO wa kuzuka vita kati ya mataifa wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni habari zisizopaswa kusikika kamwe.

Nchi bwanachama – Kenya, Uganda, Tanzania, Rwanda, Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) – zinapaswa kuwa kielelezo cha amani barani.

Pamoja na kwamba zina maslahi ya kiuchumi na kijamii yanayoshabihiana, zina lugha moja inayoyaunganisha: Kiswahili.Hata hivyo, kutishiana vita kati ya Rwanda na DRC, sikwambii na vitisho vya kufukuziana mabalozi, kumeondoa matumaini ya watu wengi waliotarajia umoja na udugu udumu.

Si siri kwamba uhasama kama huo umewahi kushuhudiwa kati ya Rwanda na Uganda, kiasi cha kufungiana mpaka.

Kumewahi pia kuzuka hali ya kutoelewana kati ya Kenya na Tanzania, mpaka wa pamoja ukafungwa na mzozo wa kidiplomasia ukatishia kupandisha joto eneo hili.

Kenya pia imewahi kukosana na Uganda kuhusu masuala ya kibiashara; tusiusahau mzozo wa Kisiwa cha Migingo ambacho mpaka sasa hatujui kinamilikiwa na nani!

Vilevile, mataifa ya Rwanda na Burundi yamewahi kuhasimiana kiasi cha Rwanda kutishia kuivamia Burundi kijeshi.

Tofauti kati ya mizozo mingine na yote ambayo inaihusisha Rwanda ni kwamba, hakuna tishio la kivita. Ni muhimu tujiulize iwapo Rwanda ni mwanachama mwenzetu anayefaa. Imekuwaje kwamba taifa dogo kama hilo ndilo linaloyatishia mengine kwa vita ilhali linajua anga ikinuka baruti linaweza kuangamizwa kwa njia rahisi?

Kabisa sipendekezi Rwanda ipokonywe uanachama wa EAC, hasa kwa kuwa nauchukulia kama muungano wa ndugu wapendanao unaopaswa kuboreshwa.

Hata hivyo, mazoea yake ya kutishia kuzua vita yanapaswa kutafutiwa suluhu ya kudumu. Labda ni athari za vita vya ndani kwa ndani ambavyo ni kiungo kikuu cha historia yake.

Katika mzozo wa juzi, Rwanda imedai DRC imeishambulia kwa makombora ya roketi na kuwateka nyara wanajeshi wake wawili, ikatishia kujibu kijeshi iwapo itashambuliwa tena.

Nayo DRC imeilaumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa asili ya Kitutsi, M23, wanaoendesha shughuli zao mashariki mwa DRC. Rwanda imelaumiwa mara kadha kwa kuyaunga mkono makundi ya waasi yanayopigana na majeshi ya DRC.

Mgogoro kama huu, hasa kwa kuwa DRC imejiunga na EAC, unapaswa kusuluhishwa na Jumuiya hiyo, ambayo sasa mwenyekiti wake ni Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Kocha Ralf Rangnick aanza kazi ya ukocha kambini mwa...

Zelensky: Urusi sasa imeteka asilimia 20 ya taifa la Ukraine

T L