• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 8:57 PM
Zelensky: Urusi sasa imeteka asilimia 20 ya taifa la Ukraine

Zelensky: Urusi sasa imeteka asilimia 20 ya taifa la Ukraine

NA MASHIRIKA

KYIV, UKRAINE

RAIS wa Ukraine Volodymyr Zelensky amefichua kuwa wanajeshi wa Urusi wanadhibiti asilimia 20 ya nchi yake siku 100 tangu wavamie nchi hiyo.

Rais huyo aliyekuwa akihutubia bunge la Luxembourg kwa njia ya video Ijumaa, alisema kuwa eneo la Ukraine linalodhibitiwa na Urusi ni kubwa kuliko Ubelgiji, Luxembourg na Uholanzi kwa pamoja.

“Hadi leo, karibu asilimia 20 ya nchi yetu inadhibitiwa na wavamizi; hii ikiwa ni karibu kilomita 125,000. Aidha, takriban kilomita 300,000 mraba zimechafuliwa na mabomu ya kutegwa ardhini na vifaa visivyolipuka,” alieleza Rais Zelensky.

“Vile vile, takriban raia milioni 12 wa Ukraine wamekuwa wakimbizi wa ndani. Zaidi ya watu milioni 5, wengi wao wakiwa wanawake na watoto, wamekimbilia nje ya nchi,” akaongeza.

Vikosi vya Urusi vimekuwa vikizidisha mashambulizi dhidi ya mji wa Severodonetsk katika eneo la Donbas mashariki mwa taifa hilo.

Severodonetsk ni mji wa mashariki kabisa ulio chini ya udhibiti wa Ukraine.Gavana wake Serhiy Haidai alisema Urusi inajaribu kuvunja ngome ya ulinzi katika mji huo “kutoka pande zote.”

Msemaji wa jeshi la Ukraine alieleza kuwa Kyiv inafanya kila juhudi kuzuia maadui, hata kama wapiganaji wake 100 wanauawa kila siku Severodonetsk.

Urusi kwa sasa inadhibiti sehemu kadha za Ukraine kikiwemo kisiwa cha Crimea ilichoteka 2014 na maeneo ya mashariki Donetsk na Luhansk, maarufu kama ukanda wa Donbas, inayowinda.

Baada ya kushindwa katika azma yake ya kuteka jiji kuu Kyiv, majeshi ya Urusi yameelekeza juhudi zote katika kuteka eneo la mashariki la Donbas.

Mapigano makali sasa yako Severodonetsk katika eneo la Donbas ambapo asilimia 80 tayari imetwaliwa na Urusi lakini jeshi la Ukraine limeweka upinzani mkali.

“Kuna miji mingine pia ambapo mashambulio makali kama hayo yanafanywa na Urusi. Jeshi la Urusi linatumia nguvu zake zote za kijeshi, halijali binadamu,” alisema Zelenskiy.

Ingawa Urusi inakanusha kuwalenga raia katika mashambulio yake, inakiri kuwa inalenga miundomsingi inayotumiwa kuingiza zana kutoka mataifa ya Magharibi kama vile reli.

Rais Zelenskiy alisema Ukraine inatarajia kupokea silaha zaidi kutoka mataifa rafiki baada ya Amerika kutoa ahadi ya kutuma msaada.

Urusi imeshutumu Amerika kwa kuchochea vita hivyo baada ya ahadi hiyo ya silaha zenye thamani ya dola milioni 700 kwa Ukraine ambazo zitajumuisha roketi zinazoweza kurushwa kutoka umbali wa kilomita 80.

Haya yanafanyika wakati ambapo Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu Watoto (Unicef) linasema kuwa takriban watoto 100 wameuawa ndani ya mwezi mmoja uliopita.

Athari za vita hivyo zinandelea kushuhudiwa katika nchi mbalimbali duniani.

Serikali ya Chad imetangaza hali ya dharura ya chakula kutokana uhaba wa nafaka uliosababishwa na vita vya Ukraine.

Serikali ya kijeshi nchini humo inasema, hali ya chakula imekuwa mbaya mno na misaada ya kiutu inahitajika mara moja.

Rais wa Umoja wa Afrika Macky Sall jana Ijumaa alifanya mazungumzo na Rais wa Urusi Vladimir Putin mjini Sochi ili kutoa wito wa kuondolewa kwa vikwazo vya usafirishaji wa nafaka na mbolea.

  • Tags

You can share this post!

DOUGLAS MUTUA: EAC ibuni jopo la viongozi wasifika kutatua...

Rais Suluhu ampa Lissu marupurupu yake ya ubunge

T L