• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 11:33 PM
DOUGLAS MUTUA: Kenya itumie ushawishi wake ipasavyo Afrika ya Mashariki

DOUGLAS MUTUA: Kenya itumie ushawishi wake ipasavyo Afrika ya Mashariki

NA DOUGLAS MUTUA

KWA mataifa mengi ya eneo la Afrika Mashariki na Kati, Kenya ni baniani mbaya ambaye kiatu chake ni dawa.

Japo hapendwi na mataifa hayo, baniani huyu ana ushawishi unaotambuliwa kote, hivyo hutumika ikibidi.

Ni kutokana na mtizamo huu ambapo taifa la Somalia limeilalamikia Kenya kwa kulitambua eneo la Somaliland lililojitenga nalo.

Tatizo lilianza pale Ikulu ya Nairobi ilimwalika mwakilishi wa Somaliland kwenye karamu ya mabalozi wanaotumika nchini Kenya.

Somalia ilihisi kudharauliwa na Kenya.

Balozi wa Somalia, Bw Mohamoud Ahmed Nur ‘Tarzan’, aliondoka kwenye karamu hiyo kwa vishindo akisema Kenya haikupaswa kuipa Somaliland hadhi ya taifa huru.

Eneo la Somaliland lilijitenga na Somalia 1991, na limekuwa likiendesha shughuli zake za kiutawala kama taifa huru.

Limetambuliwa na Taiwan pekee, kisiwa kilichojitenga kama Somalialnd, na ambacho Uchina inadai ni sehemu yake.

Eneo la Somaliland lina serikali, majeshi, polisi, na ni tulivu likilinganishwa na Somalia, ambayo haijawa imara tangu 1991 serikali ya Rais Siad Barre ilipopinduliwa.

Matatizo kati ya Kenya na Somalia yalianza 2020 wakati kiongozi wa Somaliland, Bw Muse Bihi, alitembelea Kenya.

Somalia ilikuja juu na kukatiza uhusiano wa kidiplomasia kati yake na Kenya, ikaipiga marufuku miraa ya Kenya.

Mataifa hayo yalirejesha uhusiano huo mnamo Agosti 2021, ila marufuku hayo bado yalisalia.

Kulikuwa na matumaini kwamba, uhusiano huo ungedumu kwa kuwa uliendelea hata baada ya mzozo kati ya mataifa yote mawili kutatuliwa na mahakama ya kimataifa kwa njia isiyoridhisha Kenya. Ni muhimu ieleweke kwamba, Rais Bihi alizuru Djibouti na Ethiopia, lakini Somalia haikulalamika kama ilivyofanya alipozuru Kenya.

Tukio hilo la hivi majuzi zaidi linatishia kuendeleza mzozo wa kidiplomasia kati ya Kenya na Somalia kwani limetokea siku chache baada ya Somalia kuwa na utawala mpya.

Kenya inapaswa kuwa angalifu inapohusiana na taifa lolote ili uhusiano huo usiathiri maslahi yake kwa njia yoyote ile.

Haijalitambua eneo la Somaliland kama nchi huru, hivyo haikuhitaji kabisa kuhatarisha uhusiano wake na Somalia kwa kuliweka katika hadhi sawa na nchi hiyo.

Lakini tukio hilo halishangazi; Rais Kenyatta amejizingira kwa wataalamu wasioonekana kujua mambo mengi ya kimsingi kuhusu fani zao, hivyo hawaishi kumpotosha na kumfedhehesha.

[email protected]

  • Tags

You can share this post!

Mong’are atolewa jasho na digrii yake

GUMZO: Pogba kutia wino Juve mwezi Julai

T L