• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 7:55 PM
JURGEN NAMBEKA: Ahadi za maji Pwani zipungue na miradi iliyopo ikamilishwe

JURGEN NAMBEKA: Ahadi za maji Pwani zipungue na miradi iliyopo ikamilishwe

NA JURGEN NAMBEKA

WIKI jana serikali ilitangaza kuwa ingeshirikiana na kampuni za kibinafsi kutekeleza mradi wa Sh300 bilioni wa kukabiliana na uhaba wa maji ukanda wa Pwani.

Kulingana na Shirika la Ustawi wa Maji Pwani(CWWDA), kwa kima hicho malilio ya wakazi yatakamilika.

Licha ya wazo hilo kuwa la kuvutia na lenye kuwapa Wapwani matumaini ya kupata maji safi ya kunywa, hilo litatimia tu iwapo mradi utatekelezwa kwa uadilifu.

Kulingana na mwenyekiti mpya wa bodi ya CWWDA, Bw Daniel Mwaringa, ushirikiano baina ya serikali na sekta ya kibinafsi kutawezesha taasisi hiyo kukabiliana na tatizo la maji Pwani.

Kwa kufuatilia kwa karibu mradi huo, kaunti zote sita za Pwani zingefaidika na maji; jambo ambalo kwa sasa ni hekaya ya abunwasi kwani miradi imekuwa ikiendelea kwa muda, ila mifereji haijatoka hata tone kwa takriban miaka 20.

Kwa mujibu wa Bw Mwaringa, miradi ya maji iliyokuwa imeorodheshwa kutekelezwa itagharimu kitita kikubwa cha fedha.
Ndiposa CWWDA inalenga ushirikiano kutafuta fedha za kutekelezea mradi huo.

Kati ya miradi inayoangaziwa ni ule wa bwawa la Mwache lililoko Kaunti ya Kwale, ambalo inatarajiwa litagharimu Sh25 bilioni.

Mradi huo, ambao zabuni yake ilitolewa mnamo 2018, unatarajiwa kutoa suluhu la uhaba sugu wa maji katika kaunti za Mombasa, Kilifi na Kwale. Swali ni je, miaka mitano baadaye mbona mradi haujakamilika?

Kulingana na Meneja Msimamizi, Mhandisi Martin Tsuma, mradi huo ambao unatarajiwa kukamilika Agosti umetekelezwa asilimia 25 pekee kufikia sasa.

Suala ibuka ni kuwa, iwapo ujenzi ulianza 2018 baada ya zabuni kutolewa, na sasa miaka minne baadaye ni asilimia 25 pekee imekamilika, utakuwa umekwisha kufikia Agosti ?

Licha ya mradi huo kutoa msaada mkubwa wa maji kwa wakazi wa kaunti hizo tatu, heri serikali ingewekeza fedha hizo katika shughuli nyingine badala ya kuanzisha mradi na kutoa ahadi chungu nzima, na kisha inakosa kutimiza.

Uchumi wa nchi ulivyo hafifu wakati huu, serikali itatoa kweli Sh300 bilioni kwa miradi ya maji ya eneo la Pwani pekee ilhali kuna sehemu nyingine nchini.

Hata sekta ya kibinafsi, ambayo ndiyo inategemewa pakubwa kutoka ufadhili, huenda pia ikasitasita kuchangia kutokana na historia mbaya ya matumizi ya fedha.

Ni wazo zuri kutoa ahadi ya miradi, ila ni vyema kukamilisha miradi iliyoko kabla kuahidi mingine – iwe midogo au mikubwa.

Badala ya CWWDA kuahidi ruwaza kubwa ya Sh300 bilioni, wakamilishe bwawa la Mwache kuwapa afueni Wapwani wanaohangaika kwa kukosa maji.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Sababu za watoto kuhepa JSS zibainike

KINYUA KING’ORI: Raila apuuze usaliti wa wabunge...

T L