• Nairobi
  • Last Updated May 22nd, 2024 4:47 PM
TAHARIRI: Sababu za watoto kuhepa JSS zibainike

TAHARIRI: Sababu za watoto kuhepa JSS zibainike

NA MHARIRI

RIPOTI kwamba wanafunzi zaidi ya 200,000 wamekosa kujiunga na Gredi 7 katika shule za Sekondari ya Msingi (JSS), inafaa kushtua serikali.

Hiyo inamaanisha kuwa asilimia 15 ya wanafunzi 1,253,577 waliofaa kujiunga na JSS ‘wamehepa’.

Kwa mujibu wa Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu, wizara yake inashirikiana na machifu kusaka watoto hao ambao hawajajiunga na Gredi 7 tangu wenzao kuripoti Januari 30, 2023.

Wizara ya Elimu pia imefichua kuwa imeanzisha uchunguzi kwa lengo la kunasa wanafunzi ambao wamekataa kujiunga na JSS na badala yake wamejisajili kuwa watahiniwa wa Mtihani wa Darasa la Nane (KCPE).

Usajili wa watahiniwa watakaofanya mtihani wa KCPE mwaka huu ulianza wiki mbili zilizopita na utakamilika Machi 30.
Kulingana na ripoti, baadhi ya wazazi wamekuwa wakihonga wakuu wa shule za msingi ili kuwezesha watoto wao kujiunga na Darasa la Nane.

Wizara ya Elimu sasa inakagua rekodi ili kunasa wanafunzi waliohepa Mfumo wa Umilisi na Utendaji (CBC) na kukumbatia mfumo wa zamani wa 8:4:4 ambao unaelekea kuisha katika shule za msingi kufikia Desemba, 2023.

Badala ya kupoteza rasilimali na muda mwingi kukagua rekodi na hata kuwinda walimu wanaoruhusu wanafunzi wa JSS kujiunga na Darasa la Nane, serikali inafaa kuchunguza kiini cha wazazi kutorosha watoto wao.

Hatua ya wazazi kujikokota kupeleka watoto wao JSS ni ishara kwamba Wakenya wengi wangali hawaelewi vyema mfumo wa CBC. Serikali haijatoa elimu ya kutosha kuelimisha umma kuhusu na hatima ya watoto CBC.

Ukweli ni kwamba hata serikali yenyewe inaonekana kutoelewa vyema mfumo wa CBC.

Tangu kuanzishwa kwa mfumo wa CBC, serikali imeunda majopokazi mawili kutoa mwelekeo wake na majopokazi hayo yameonekana kutoa ripoti zinazokinzana. Jopokazi lililobuniwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta lilipendekeza kuwa wanafunzi wa JSS wasomee katika shule za upili.

Ripoti ya awali ya jopokazi lililoundwa na Rais Ruto lilipendekeza wanafunzi wa Gredi 7 wasomee katika shule za msingi.
Jopokazi hilo la Rais Ruto lenye wanajopo 42, linatarajiwa kutoa ripoti yake mwezi ujao wa Machi.

Inaonekana kwamba baadhi ya Wakenya wanaotorosha watoto wao wanahofia kuwa ripoti ya mwisho ya jopokazi hilo huenda ikatoa mapendekezo tofauti ambayo huenda yakaathiri watoto wao ambao tayari wako JSS.

Taarifa iliyotolewa na wizara ya Elimu kuwa mwongozo unaotumika sasa kuendesha JSS ni wa muda mfupi, imeongezea wazazi wasiwasi.

Kulingana na wizara ya Elimu, mwongozo wa kudumu utatolewa baada ya ripoti ya mwisho kutolewa. Serikali ijilaumu kwa kuletea wazazi hali ya sintofahamu kuhusu CBC.

  • Tags

You can share this post!

Dawa dhidi ya kikohozi kutengenezwa kwa utando wa konokono

JURGEN NAMBEKA: Ahadi za maji Pwani zipungue na miradi...

T L