• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 8:50 AM
KINYUA BIN KINGORI: Rais ni kiongozi wa Wakenya wote si jamii au eneo lake

KINYUA BIN KINGORI: Rais ni kiongozi wa Wakenya wote si jamii au eneo lake

Na KINYUA BIN KINGORI

WAKATI huu viongozi wa kisiasa wameanza mapema kampeni zao kwa kuzuru maeneo mbalimbali nchini, ili kushawishi wananchi kuwaunga mkono katika kinyanganyiro cha urais, itakuwa bora tujitenge na kauli za chuki au majivuno.

Tayari uchaguzi mkuu wa 2022 umeonyesha dalili za mapema kwamba washindani wakuu watakuwa Naibu Rais Dkt William wa UDA na kinara wa ODM Raila Odinga ambaye ni mwanasiasa mkongwe na mkomavu.

Wanasiasa wanaovumisha kampeni za wagombeaji hao wakuu wanafaa kuwa makini na wapevu wanapotoa matamshi katika majukwaa ya sirini au hadharani, maana wengine wanatupa maneno ovyo bila kuyachuja na kuishia kumponza kigogo wanayepigia debe.

Majuzi mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed ambaye ni mtetezi sugu wa Odinga na chama cha ODM, amesikika katika video iliyosambazwa mitandaoni akijigamba eti kinara huyo akichaguliwa kuwa Rais mwakani, basi serikali itakuwa yao (kwa maana ya watu wa nyanza) huku Wakenya wengine wakiwemo wa Mlima Kenya wakibakia wageni serikalini.

Matamshi kama hayo yakitumiwa na mahasidi wa Odinga kisiasa yatabomoa juhudi ambazo kinara wa chungwa ametia katika kupata ushawishi kote nchini ikiwemo eneo la Mlima Kenya.Japo Wakenya ni werevu kiasi cha kujua kiongozi watakayemchagua kuwa rais wa tano wa taifa hili, iwe ni Ruto au Odinga atakayeibuka mshindi katiba imemwajibisha kuhakikisha serikali yake inawahudumia wananchi wote na kuimarisha maisha yao bila kuzingatia kabila au mrengo wao wa kisiasa.

Kauli ya Junet haifai kamwe kuachwa bila kukosolewa, maana huenda raia wachache waliokuwa wamebadili mtazamo wao juu ya kinara wa ODM na kushawishika kumuunga mkono katika uchaguzi wa 2022, wakatiwa hofu na matamshi hayo potovu na kughairi nia yao.

Wanasiasa waelewe kwamba mwaka ujao wananchi watapigia kura kiongozi atakayesaidia kufufua uchumi, kuboresha miundo msingi, kuimarisha maisha yao na matarajio mengine, wala si kuogopa vitisho au kutiwa hofu juu ya mgombeaji fulani.

Kutetea kiongozi unayependelea ni haki ya kila mfuasi, hata hivyo, ili kupiga jeki ushawishi wake mashinani tukomeshe propaganda na uzushi.Bali tukite katika kuhamasisha umma kuhusu sera na mbinu atakazobuni mgombea huyo kuokoa uchumi wetu na kustawisha taifa akiwa Rais.

Siasa chafu na matamshi ya kupotosha yanayoweza kuchangia kueneza hofu na mgawanyiko kwa wakenya yanafaa kupuuzwa.Viongozi wasiopima kauli zao wakataliwe na hawafai kushirikishwa katika kampeni za kuvumisha wagombeaji wa kisiasa.

Je, ikiwa kiongozi hutoa matamshi kiholehola kwa nini awe mstari wa mbele katika kampeni? .Uchaguzi ujao hata kutolewe matamshi mabaya kivipi , wananchi ndio wataamua ni kiongozi yupi atakayekuwa Rais wao ,na wataendesha kampeni kwa amani na umoja kwa kuwapa nafasi ya kuwasikiliza wagombezi wote bila kuzingatia vyama ili kuchuja mwenye sera na maono yanayoweza kuaminika na kutimizika.

You can share this post!

LEONARD ONYANGO: Utafiti kuhusu hatari ya Ziwa Victoria...

Kilimo champa ajira na kumlipia karo ya chuoni

T L