• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 7:50 AM
LEONARD ONYANGO: Utafiti kuhusu hatari ya Ziwa Victoria usipuuzwe

LEONARD ONYANGO: Utafiti kuhusu hatari ya Ziwa Victoria usipuuzwe

Na LEONARD ONYANGO

MATOKEO ya utafiti yaliyotolewa wiki jana, yanayoonyesha kuwa maji ya Ziwa Victoria yanachangia katika ongezeko la visa vya kansa ya ini, yanashtua.

Kwa mujibu wa utafiti huo, vimelea vya rangi ya kijani vinavyoelea juu ya maji ya Ziwa Victoria ni bakteria hatari wanaosababisha ugonjwa wa saratani.Vimelea hao green algae hutoa sumu aina ya cyanotoxins ambayo hudhuru ini, kwa mujibu wa wanasayansi walioanza kufanya utafiti huo mnamo 2018.

Wanasayansi hao wanatoka vyuo vikuu vya Maseno, Moi na Masinde Muliro kwa ushirikiano wa Taasisi ya Utafiti wa Matibabu Nchini (Kemri).Katika miaka ya karibuni kumekuwa na ongezeko la vimelea hivyo, kiasi kwamba vimebadili ‘rangi’ ya maji.

Ukizuru ufuko wa Ziwa Victoria katika eneo la Dunga, Kaunti ya Kisumu, utabaini kwamba vimelea hivyo vimebadili rangi ya maji – utadhani ni machafu.Utafiti huo unashtua, kwa sababu idadi kubwa ya wakazi wa Nyanza na maeneo mengine ya nchi yanayopakana na Ziwa Victoria, hutegemea maji hayo kwa matumizi ya kila siku.

Matokeo ya uchunguzi wa wanasayansi hao yanazua hofu kwamba ukanda wa Nyanza – ambao una sehemu kubwa ya Ziwa Victoria – ni eneo hatari zaidi kwa afya nchini Kenya.Hii inatokana na ukweli kwamba kanda hiyo tayari linazongwa na maambukizi ya juu ya magonjwa kadha hatari, kama vile malaria na virusi vya HIV.

Zaidi ya asilimia 50 ya maambukizi ya malaria nchini yanashuhudiwa Nyanza pamoja na eneo la Magharibi.Maambukizi hayo ya juu ya malaria yametokana na kuwepo kwa Ziwa Victoria, ambalo hutoa mazingira mwafaka kwa mbu kuzaana.

Wakati huo huo, kaunti za Homa Bay, Migori, Kisumu na Siaya ni miongoni mwa gatuzi zilizo na maambukizi ya juu mno ya virusi vya HIV. Ziwa Victoria pia limelaumiwa kwa kuchangia katika kiwango hicho cha juu cha HIV, ambayo husababisha ugonjwa wa Ukimwi.

Ufichuzi kuwa maji ya Ziwa Victoria yanasababisha kansa ya ini, unafaa kuzua wasiwasi miongoni mwa viongozi wa Nyanza na maeneo mengine yanayopakana na ziwa hilo, na wale wa serikali.Takwimu za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) zinaonyesha kwamba, kati ya vifo 10,000 ambavyo hutokea humu nchini watu 42 (asilimia 0.42) waliaga kutokana na saratani ya ini.

Hii inamaanisha kuwa, kuna uwezekano mkubwa wakazi wa maeneo yanayopakana na Ziwa Victoria wamekuwa wakifariki kimyakimya, kutokana na kansa hii.Utafiti huo unafaa kuzindua serikali kuchukua hatua za haraka, ili kunusuru mamilioni ya watu wanaoishi karibu na Ziwa Victoria dhidi ya maradhi hatari ya saratani ya ini.

Badala ya kupiga domo la siasa kila uchao, viongozi wa Nyanza na maeneo jirani ya ziwa hilo hawana budi kushinikiza serikali ya kitaifa na kaunti kuhakikisha kuwa, wakazi wanapata maji salama yasiyo na green algae.

Wabunge watumie fedha za kustawisha maeneobunge (NG-CDF) kununua vifaa vya kusafisha maji hayo ya ziwa, au kuchimba visima ili kuwaepusha watu na maradhi hayo sugu ambayo ni ghali kutibu.

You can share this post!

Bondia Ajowi kutetea hadhi ya Hit Squad

KINYUA BIN KINGORI: Rais ni kiongozi wa Wakenya wote si...

T L