• Nairobi
  • Last Updated May 20th, 2024 8:28 PM
KINYUA BIN KINGORI: Wakenya wasipuuze chanjo ya corona kusaidia kupunguza makali ya virusi

KINYUA BIN KINGORI: Wakenya wasipuuze chanjo ya corona kusaidia kupunguza makali ya virusi

Na KINYUA BIN KINGORI

KWANZA, natumia safu hii kuwatumia wasomaji wa makala hii, Taifa Leo na Taifa Jumapili kwa jumla salamu za heri njema ya Krismasi kesho kutwa.

Visa vya corona vinazidi kuongezeka na kuna baadhi ya wazazi ambao wamekataa kupokea chanjo kwa visingizio visivyo na mbele wala nyuma. Wanatumia uvumi kuwatia hofu hata watoto wao wanaotaka kuchanjwa. Wakati serikali kupitia Wizara ya Afya imejitolea kuhakikisha imepata chanjo toshelezi kuhakikishia wananchi usalama wao, kuna wazazi ambao hawaoni umuhimu wa juhudi hizo kwa kupuuza amri ya serikali kuwataka wananchi wote kuchanjwa.

Wakati huu wa likizo fupi ya Disemba, ambapo shule zote zimefungwa, ni wajibu wa wazazi na jamii kujitolea kuhakikisha wamewaepushia watoto maambukizi ya corona kwa kuchanjwa na kuwapa hamasisho kuelewa umuhimu wa kuzingatia masharti yaliyowekwa kuzuia maambukizi.

Watilie maanani uvaaji wa barakoa, kunawa mikono miongoni mwa tahadhari nyingine zinazostahili. Inavunja moyo kuona baadhi ya watu wakubwa ambao juhudi zao ndizo tu zinazoweza kufaulisha vita vya kupambana na maambukizi hasa baada ya virusi vya Omicron kubainika kusambaa nchini, wakipuuza tahadhari.

Virusi vya Omicron vimethibitishwa nchini na ripoti ya Shirika la Afya Duniani (WHO), imetangaza kuwa vimesambaa katika mataifa 90 kote ulimwenguni. Wazazi wawe makini na kulinda watoto wao dhidi ya maambukizi hasa wakiwa likizoni ili kuzuia janga litakalofanya nchi kufungwa na kuathiri tena kalenda ya masomo.

Serikali ishirikiane na machifu na wazee wa mitaa kuhakikisha kuwa wananchi wanajilinda.

You can share this post!

VALENTINE OBARA: ‘Tosha’ ya Joho si hakikisho ya...

Nchi chache Afrika zatenga fedha za kutosha kwa sekta ya...

T L